Mzize kimataifaMzize kimataifa

KIMATAIFA moto unawaka kwa wawakilishi wa Tanzania ngoma kuzidi kupigwa huku kila timu ikipambana kufikia malengo yao ndani ya dakika 90 za ushindani kwa wachezaji kuvuja jasho kusaka ushindi wakitumia mbinu za benchi la ufundi.

Chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi Yanga inayodhaminiwa na SportPesa kete yake ya kwanza haikuwa kinyonge hivyo hesabu kubwa ni kuelekea kwenye mchezo wa pili unaotarajiwa kuchezwa wikiendi.

Dube kimataifa
KWENYE anga la kimataifa Prince Dube amefunga bao la kwanza akiwa na uzi wa Yanga, Ligi ya Mabingwa Afrika. Source: Yanga.

Katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex Agosti 17 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Vital’O 0-4 Yanga. Ushindi huo umewapa mkwanja wa shilingi milioni 20 ikiwa ni zawadi ya goli la mama ambaye kila bao ananunua kwa milioni tano kuwapa hamasa wachezaji kutafuta ushindi kimataifa.

Ikumbukwe kwamba mabao kwenye mchezo huo yamefungwa na Prince Dube dakika ya 6, Clatous Chama dakika ya 67, Clement Mzize dakika ya 74 na chuma cha nne ni mali ya Aziz Ki dakika ya 90 kwa mkwaju wa penalti.

JOB NA MKWANJA

Nyota wa Yanga ambaye ni beki Dickson Job hakuanza kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O ya Burundi ila amebainisha kuwa alikuwa akiwaambia wachezaji wafunge mabao mengi zaidi.

Job ambaye ni nahodha msaidizi alishuhudia Bakari Nondo akianza kikosi cha kwanza kutimiza majukumu ya timu hiyo inayepeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.

“Nilikuwa ninafurahi pale ambapo tunafunga mabao na niliwaambia wachezaji kuwa tuongeze mabao mengi zaidi kwa kuwa ili kupata fedha nyingi mabao mengi yanahitajika. Lakini kikubwa ambacho tunahitaji ni ushindi.”

HIKI HAPA KIKOSI KILICHOANZA KIMATAIFA KWA YANGA

YANGA kimataifa
KWENYE Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga ilianza kwa ushindi kimataifa. Source: Yanga.

Djigui Diarra

Yao Kouassi

Nickson Kibabage

Bakari Nondo

Ibrahim Bacca

Khalid Aucho

Maxi Nzengeli

Mudathir Yahya

Prince Dube

Aziz Ki

Clatous Chama

WACHEZAJI WA AKIBA

Mshery, Job, Jonas Mkude, Nkane, Abuya, Pacome, Aziz Amdambwile, Kennedy Musonda, Clement Mzize.

CHAMA NA BAO LAKE YANGA

Clatous kimataifa
Clatous kimataifa amefunga bao la kwanza akiwa na uzi wa Yanga Ligi ya Mabingwa Afrika. Source: Yanga.

Kiungo Chama alifunga bao la kwanza akiwa na uzi wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika alipotumia dakika 68 uwanjani. Kiungo huyo ambaye aliibuka hapo akitokea Simba amesema kuwa ni furaha kwake kufunga.

“NI furaha kwangu kufunga bao la kwanza kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hakika ni jambo linalofurahisha ukizingatia kwama ni bao langu la kwanza nikiwa ni Mwananchi.”

AZAM FC WAKOMBA MILIONI TANO

Blanco
Blanco wa Azam FC kimataifa amefunga bao dhidi ya APR. Source: Azam FC.

Matajiri wa Dar, Azam FC wamekomba milioni tano ya goli la mama kwa ushindi kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR wakiwa Uwanja wa Azam Complex ilikuwa ni Agosti 18 2024.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Yusuph Dabo ameweka wazi kuwa wana uwezo wakupata matokeo ugenini dhidi ya APR katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na uimara wa kikosi Chao.

Katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Azam Complex baada ya dakika 90 ubao ulisoma Azam FC 1-0 APR. Anaitwa Jhonier Blanco alipachika bao pekee la ushindi dakika ya 55. Penalti hiyo ilisababishwa na kiungo Feisal Salum ambaye alichezewa faulo akiwa ndanj ya 18.

Dabo amesema: “Tulikuwa na muda wakupata matokeo na niliwaambia wachezaji kuwa ukipata nafasi ya kufunga fanya hivyo ikishindikana itakuwa ni muda wakutoa pasi kwa mwingine.

“APR ni timu ngumu kufungika kwani haijafungwa mabao mengi kutokana na uimara wao katika ulinzi bado tuna nafasi yakupata matokeo ugenini kwa kuwa tuna kikosi imara na cha ushindani.”

NENO LA APR
Kocha Mkuu wa APR ya Rwanda Darko Novic amesema kuwa ni mchezo uliokuwa wazi na walihitaji kupata ushindi mwisho wakapoteza kwa kukosa nafasi ambazo walitengeneza.

“Ulikuwa ni mchezo wenye ushindani lakini tulikosa nafasi ambazo tulizipata mwisho tukafungwa kwa penalti ambayo imewapa ushindi hivyo tutafanya maandalizi mchezo ujao.”

KIKOSI KAZI CHA DABO KILICHOANZA

Mohamed Mustafa

Lusajo Mwaikenda

Pascal Msindo

Yeison Fuentes

Yannick Bangala

Adolf Mtasigwa

James Akamiko

Franck Tiesse

Jhonier Blanco

Fei Toto

COASTAL UNION WAPOTEZA

Wagosi wa Kaya, Coastal Union kutoka Tanga kwenye mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho walipoteza wakiwa ugenini katika mchezo uliochezwa Agosti 17.

Kwenye mchezo huo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Bravos 3-0 Coastal Union hivyo kibarua ni kikubwa kwa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mchezo wa marudio unaotarajiwa kuchezwa wikiendi ijayo.

Ili kupata nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata ni lazima Coastal Union ipate ushindi wa mabao kuanzia manne ikiwa nyumbani kwa kuwa mchezo wa kwanza imepoteza ikiwa ugenini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Share this: