
NGOMA bado mbichi ndani ya Bongo kutokana na sakata la mwamba Clatous Chama na Aziz Ki kuzua sura mpya huku mashindano makubwa yakiwa mbele yanawatazama kwa ajili ya kuukaribisha msimu mpya wa 2024/25.
Ipo wazi kwamba miamba hawa wawili kila mmoja kwa nyakati zake mkataba wake umegota mwisho kilichopo kwa sasa ni mazungumzo na timu hizo ili kuongeza dili jingine kwa ajili ya kufanya kazi kwa mara nyingine tena.
Aziz Ki wa Yanga mkataba wake umegota mwisho msimu wa 2023/24 na hajaongeza kandarasi mpya. Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga alibainisha kwamba mkataba wa nyota huyo umekwishwa na wanafanya jitihada kuzungumza naye ili aongeze mkataba mwingine.
“Kuna wachezaji ambao mikataba yao inakwisha ikiwemo na Aziz, hajaongeza mkataba lakini tupo kwenye mazungumzo naye tunaamini kwamba kila kitu kitakuwa sawa kikubwa ni kuwa na subira.Ni mchezaji mzuri hilo linajulikana.”
SAKATA LA CHAMA
Kuhusu Chama taarifa zinaeleza kuwa mvutano mkubwa ni suala la maslahi kwa pande zote mbili hivyo mpaka anaondoka kuelekea Zambia alikuwa hajasaini mkataba mpya kwa mujibu wa taarifa ambavyo zinaeleza.
Ikumbukwe kwamba hivi karibuni Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alibainisha kuwa kuna wachezaji ambao mikataba yao inaisha na wapo ambao wataondoka.
KUWANIA KUFUZU KOMBE LA DUNIA
Wakati ligi nyingi zimegota mwisho kuna mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia ambapo timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilikuwa na kazi ya kufanya dhidi ya Zambia ugenini.
Mchezo huo uliochezwa Juni 11 2024 Stars ilishinda kwa bao 1-0 huku mtupiaji akiwa ni Wazir Junior. Bao hilo la ushindi lilifungwa dakika ya 5 lilidumu mpaka mwisho wa mchezo.
MWENDO WA KUNDI LA STARS
Tanzania ipo kundi E ambapo vinara ni Morocco wenye pointi 6 baada ya kucheza mechi mbili ambazo ni dakika 180 huku Tanzania ikiwa nafasi ya pili na pointi 6 baada ya kucheza mechi tatu ambazo ni dakika 270.
Niger nafasi ya tatu, Zambia nafasi ya nne hizi zote zina pointi tatu huku Congo nafasi ya tano na Ertrea nafasi ya sita hazijakusanya pointi kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.

CECAFA INAPIGA HODI
Timu za Tanzania zinazoshiriki michuano ya kimataifa ya CAF zitapata nafasi ya kujiandaa na msimu mpya kwa kucheza na timu za Zambia, Sudan, Rwanda, Kenya na Uganda ambapo kati ya Julai 6 hadi 16 mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika.
Habari za uhakika zinaonyesha Yanga, Azam FC, Simba na Coastal Union zitashiriki michuano ya Cecafa dhidi ya timu kutoka katika mataifa hayo ambayo yatashiriki.
Cecafa ni Baraza lenye wanachama 12 ikiwemo Zanzibar ambapo timu nne zitakazoshiriki Caf Champions na Caf Confederation Cup zitacheza dhidi ya Al Hilal, Al Merreikh na Hai Ak Wadi za Sudan, Red Arrow ya Zambia na TP Mazembe ya DRC.
Michuano hiyo ambayo itakuwa kabla ya kuanza kwa msimu mpya itashirikisha timu 16 na itapigwa Tanzania. Timu nyingine ni Nyasa Big Bullets ya Malawi, SC Villa ya Uganda, APR (Rwanda), Gor Mahia (Kenya), Vital’O (Burundi), JKU (Zanzibar) na El Merreikh Bentiu (Sudan Kusini).
NGAO YA JAMII HII HAPA

Ngoma ya Cecafa ikipigwa kinachofuata ni kituo cha kusaka Ngao ya Jamii ambapo taji hilo msimu wa 2023/24 lilikwenda mikononi mwa Simba iliyokuwa inanolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira.
Ni Agosti 8 hadi 11 2024 itakuwa ambapo ni timu nne zitashiriki taji hilo lililo kwa mfumo wa ligi. Yanga, Azam FC, Simba na Coastal Union hizi zitashiriki kuwania taji hilo ikiwa ni mwanzo wa msimu mpya wa 2024/25.
Hivyo mwanzo wa msimu mpya unatarajiwa kuwa na kasi kubwa kwa kila timu kupambania malengo ya kufanya vizuri. Ipo wazi kwamba msimu wa 2023/24 Yanga ambao wanadhaminiwa na SportPesa wamekuwa na mwendo mzuri kwenye mashindano waliyoshiriki.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika wamegotea hatua ya robo fainali huku kwenye CRDB Federation walifika fainali na kuchukua taji hilo mbele ya Azam FC ambayo imemaliza ligi ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 69.

