
YANGA kila siku ni sherehe ndivyo unavyoweza kusema kwani Jumamosi hii ya Juni 15 wana jambo lingine kubwa kutoka kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB Bank msimu huu uliomalizika wa 2023/24.
Yanga ambao wanapewa jeuri kubwa na udhamini wa Kampuni ya michezo ya SportPesa wanatarajia kufanya tukio kubwa la uzinduzi wa kitabu cha Yanga kinachotarajiwa kuzinduliwa kuendana na uthibitisho wa uongozi wa Yanga huku kitabu hiko kikitarajiwa kukusanya taarifa nyingi muhimu kuhusu klabu hiyo bila kuacha chochote.
Ni wazi kwamba kwa msimu wa huu wa 2023/24 Yanga wamekuwa na wakati mzuri wakitwaa taji la Ligi Kuu Bara, CRDB Federation Cup na kufanikiwa kuandika rekodi ya kihistoria ya kutinga hatua ya Robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mashindano hayo yaanze kuchezwa katika mfumo mpya.
Mafanikio hayo yote ya Wananchi yamefanikiwa kupatikana kutokana na uongozi makini wa Rais wa Yanga, Injini Hersi Said, Kamati ya utendaji ya timu hiyo, wachezaji na hasa kiongozi wa benchi la ufundi Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.
ALI KAMWE AFUNGUKA MAZITO KITABU CHA YANGA

Ali Kamwe ambaye ni Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa jambo hilo la uzinduzi wa kitabu limekuwa likisubiriwa kwa shauku kubwa na maandalizi yake yamefanyika kwa umakini mkubwa ili kuwapa yale yaliyo muhimu mashabiki na wanachama wa timu hiyo.
“Hili ni jambo la kihistoria tunakwenda kufanya, Yanga ni klabu yenye miaka 89 na kuna mengi ambayo wanachama na mashabiki wanahitaji kuyajua, kazi hii tumeanza kuifanya miezi saba iliyopita na safari hii hatujaacha chochote.
“Mashabiki na Wanachama wanahitaji kupata kile kilicho bora na tunaamini kupitia hiki kitabu kuna simulizi nyingi nzuri watakutana nazo ambazo zinaeleza namna ilivyokuwa tangu kuanzishwa timu hii, mafanikio yake na ukuaji wake mpaka sasa.”
ISHU YA MKUTANO MKUU WA YANGA

Tukio la uzinduzi wa kitabu hiki ni mfululizo wa matukio mengi makubwa ambayo timu hiyo wameyafanya katika siku za hivi karibuni, ikumbukwe kuwa timu hiyo imetoka katika tukio kubwa la mkutano wao mkuu wa mwaka uliofanyika Juni 9, mwaka huu.
Kupitia mkutano huo mkuu wanachama walifanya mapitio ya tathimini ya mafanikio yao kwa msimu uliopita wa 2023/24, huku pia wakipitisha bajeti yao ya msimu mpya wa 2024/25 ambapo waliweka wazi kuwa inatarajiwa kuwa Shilingi Bilioni 24.5
JEMEDARI AFUNGUKA BAJETI YA YANGA

Kufuatia bajeti hiyo wadau mbalimbali wametoa maoni yao juu ya mrejesho wa kikao hicho ambapo miongoni mwa wale waliotoa maoni yao ni mchambuzi wa masuala ya michezo, Jemedari Said.
Jemedari kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa Instagram aliandika: “Kwenye mkutano mkuu wa kawaida wa mwaka wa klabu ya Yanga wakati wa kusoma mapato na matumizi, ambayo yalisomwa na Mkurugenzi wa Fedha kulikuwa na hoja ya msingi kwenye bajeti ni kwamba Kamati ya Utendaji inapotumia 1.09B zaidi ya ‘budget’ iliyopitishwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka jana, imepata wapi baraka za wanachama kutumia zaidi?
“Kwa sasa Yanga ni taasisi sio ya kibiashara. Tafsiri ya pesa iliyotumika zaidi haiwezi kuitwa hasara ila ni pesa iliyotumika kinyume na maelekezo ya wenye timu yaani wanachama.
“Kwa hiyo kwa klabu ambayo haina watu waoga tulitegemea wanachama wahoji kwamba Kamati ya Utendaji ilipata wapi mamlaka ya kutumia zaidi ya kile walichopitisha wanachama kwenye bajeti mkutano wa mwaka jana?
“Mfano serikali inapotumia pesa zaidi ya ile iliyopitishwa na bunge hatusemi nchi imepata hasara ila tunasema serikali imekosa nidhamu ya matumizi ya fedha. Na hapo inakuja hoja kwamba ilipata wapi mamlaka ya kutumia zaidi ya kilichopitishwa na bunge?
“UOGA WA KUHOJI. Hii nchi haiwezi kusogea kama watu wote wanajikomba, uongozi unapofanya makosa hakuna anayehoji. Hili ni tatizo kubwa sana katika nchi, bahati mbaya sana lipo kila mahala na wachache wenye uwezo wa kuhoji wanaonekana wana chuki.”

