Yanga yapiga mkwara mzito robo fainali, yatupilia mbali hofu
Rekodi mpya yaandikwa huku wakiwatibulia rekodi wababe Al Alhly hatua za makundi
Wachezaji wapewa majukumu makubwa kuyatimiza ndani ya uwanja kitaifa na kimataifa
WAWAKILISHI wa Tanzania Yanga wameweka wazi kuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hawana hofu na mpinzani yoyote watakayekutana naye katika hatua ya robo fainali watapambana kupata matokeo chanya ndani ya uwanja kutinga hatua ya nusu fainali.

Kikosi cha Yanga ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya kucheza jumla ya mechi 15 kimekusanya pointi 43 na namba moja kwa utupiaji ni kiungo Aziz KI mwenye mabao 10 kibindoni baada ya kucheza mechi 12.
YANGA WANAJAMBO LAO KWENYE LIGI
Ipo wazi kwamba Yanga ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wanadhaminiwa na Kampuni ya SportPesa ambayo imeleta mapinduzi makubwa kwenye soka la Tanzania kutokana na uwekezaji wake mkubwa katika anga la michezo na kubadili maisha ya wengi.
Msimu wa 2023/24 uongozi wa Yanga kupitia kwa Ofisa Habari wao Ali Kamwe umebainisha kwamba malengo ni kuwa bora zaidi katika ushindani tofauti na msimu uliopita kwa kupata mataji mengi zaidi.
“Tunahitaji kupata ushindi kwenye mechi ambazo tunacheza na hilo linawezekana, kikubwa ni kuwa tayari kwa mashabiki kuwa nasi bega kwa bega wachezaji wanatambua kwamba tunahitaji mataji kama ambavyo tulifanya msimu uliopita.
“Inawezekana licha ya kuwa kazi kuwa ngumu na ushindani kwenye ligi ni mkubwa lakini tupo tayari na tunaamini kwamba tutafanya vizuri,”.
REKODI MPYA YAANDIKWA
Yanga iliandika rekodi mpya ya kutinga hatua ya robo fainali baada ya kucheza mechi tano ilipokusanya pointi 8 kibindoni ambazo hizo ndizo inazo mpaka sasa baada ya kukosa pointi kwenye funga kazi dhidi ya Al Ahly, Waarabu wa Misri mchezo uliochezwa Machi Mosi 2024.

Licha ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 ugenini rekodi zinaonyesha kwamba Yanga kwenye kundi D wakati vinara Al Ahly wakiwa hawajapoteza mchezo baada ya kucheza mechi sita ni bao moja pekee walifungwa na mtupiaji anatoka Yanga ambaye ni Pacome kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
KUHUSU WAPINZANI WAO ROBO FAINALI
Kamwe Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa kwa hatua ambayo wamefika hawana hofu na timu yoyote ile watakayokutana nayo kwenye hatua ya robo fainali kama wangekuwa wanaruhusa kuna timu wangeichagua wamalizane nayo mapema.
“Tulikuwa na mipango kila hatua ilikuwa ni kufika hatua ya makundi tukafanikiwa kisha ikawa ni kufika robo fainali imekuwa sasa kwenye hatua hii mpinzani yoyote tutapambana naye, tupo tayari na wachezaji wapo tayari.
“Ingekuwa ni unamchagua mpinzani kwenye timu hizo 8 kuna timu ambayo tungeichagua tumalizane nayo mapema lakini kwa kuwa ni kanuni acha iwe hivyo tunaheshimu,”.
HAWA WATAKUTANA NAO ROBO FAINALI
Kutoka kundi D na pointi 8 kibindoni inaweza kukutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao ni vinara wa kundi A na pointi 13, Asec Mimosas ya Ivory Coast walimaliza wakiwa nafasi ya kwanza kundi B na pointi 11 wengine ni Petro Luanda ya Angola walimaliza wakiwa nafasi ya kwanza kundi C na pointi 12.
Nani atakuwa nani itafahamika Machi 12 ambapo droo inatarajiwa kuchezwa na kila mbabe atajua mbabe wake atakuwa nani kwenye hatua hiyo kubwa kimataifa.
MECHI ZAO HATUA YA MAKUNDI
Yanga ni kundi D mchezo wa kwanza hatua ya makundi ilikuwa Novemba 24 2023 ilishuhudia ubao ukisoma CR Belouizdad 3-0 Yanga
ilikuwa Desemba 2 2023 ubao wa Uwanja wa Mkapa uliposoma Yanga 1-1 Al Ahly, Pacome Zouzuoa alifunga bao dakika ya 90 lile la Al Ahly lilifungwa na Percy Tau.
Kete ya tatu ilikuwa ni Desemba 8 2023 ilishuhudia ubao ukisoma Medeama 1-1 Yanga, bao la Medeama lilifungwa na Jonathan Sowah dakika ya 27 kwa mkwaju wa penalti na lile la Yanga lilifungwa na Pacome dakika ya 36.
Kazi ya nne ilikuwa ni Desemba 20 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 3-0 Medeama ni mabao ya Pacome dakika ya 33, Bakari Nondo dakika ya 61 na bao la tatu ni mali ya Mudathir Yahya alipachika dakika ya 66.
2024 walirejea uwanjani kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika walianza na Yanga 4-0 CR Belouizdad Uwanja wa Mkapa Februari 24, mabao ya Mudathir dakika ya 43, Aziz Ki dakika ya 46, Kennedy Musonda dakika ya 48 na bao lililowapeleka Yanga robo fainali lilifungwa na Joseph Guede dakika ya 84.
Machi Mosi ulikuwa ni mchezo wa kukamilisha hatua ya makundi dhidi ya Al Ahly walipoteza kwa kufungwa bao 1-0 ugenini mtupiaji alikuwa ni Hassan El Shahat dakika ya 46.
