yangasc------------------------------------------ (-)yangasc------------------------------------------ (-)

WAKIJIANDAA na mchezo wao wa kesho Ijumaa dhidi ya Namungo, uongozi wa Yanga umetamba kuwa umejipanga kuhakikisha unaendeleza kasi ya vipigo na kuvuna pointi zote 12 kwenye mwezi huu Machi.

Mabingwa hao watetezi wenye udhamini mnono wa Kampuni ya michezo ya SportPesa wataingia katika mchezo huu wakiwa wametoka kupoteza kwa kipigo cha bao 1-0 mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulipigwa nchini Misri.

Licha ya kipigo hiko tayari Yanga walikuwa wamefanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali ya mashindano hayo ambapo wamefanya hivyo kwa mara ya kwanza katika historia ya klabi hiyo.

Kwenye Ligi Kuu Bara Yanga wanatarajia kuingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi mfululizo katika michezo yao ya ligi kuu iliyopita.

MSIMAMO WA LIGI KUU MPAKA SASA

azamtvsports-------------------------------------------
Msimamo wa Ligi Kuu Bara kabla ya michezo ya jana Jumatano

Yanga waliochini ya udhamini wa Kampuni ya SportPesa wanaendelea kutamba mpaka sasa ambapo kwenye msimamo wa ligi wamekusanya pointi 43 baada ya kucheza michezo 16.

Vinara wa ligi mpaka sasa ni Azam ambao wamekusanya pointi 44 katika michezo 20 ambayo wamecheza (Michezo minne zaidi).

Simba wanakamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kukusanya pointi 36 katika michezo 16 ambayo wamecheza mpaka sasa, hii ni baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Tanzania Prisons jana Jumatano.

KOCHA MKUU WA YANGA GAMONDI ANASEMAJE?

yangasc------------------------------------------ (-)
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi

Kuelekea mchezo wa kesho Ijumaa Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Argentina, Miguel Gamondi amesema mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo ya sushindi.

Gamondi amesema mara zote wanapokutana na Namungo mchezo unakuwa mgumu, na hili lilithibitishwa na ushindi wa bao 1-0 walioupata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza, lakini wamejipanga kuwakabili.

Kuhusu hali ya kikosi chao, Gamondi amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na wapo tayari kwa mchezo huo ambao lengo ni kuhakikisha wanapata ushindi.

“Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Namungo, mara zote tunapokutana inakuwa mechi ngumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Gamondi.

MSAFARA WA KIKOSI

yangasc------------------------------------------
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi na mchezaji Azizi Ki 

Kikosi cha Yanga leo Jumatano asubuhi kilitarajiwa kuanza safari ya kuelekea mkoani Lindi tayari kwa mchezo wao huo wa kesho Ijumaa wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo, ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa.

Kabla ya kuondoka kikosi kiliendelea na programu za mazoezi ya mwisho kwenye kambi yao ya Avic Town, Kigamboni kwa ajili ya kujiweka tayari kwa mchezo huo.

Taarifa ya Yanga ilieleza kuwa wameondoka na kikosi kamili kuelekea Lindi ambapo taarifa hiyo pia iliendelea kueleza kuwa kwa sasa kila mchezo wameupa umuhimu mkubwa na alama tatu ndio malengo yao wakitarajia kuvuna pointi 12.

Uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa unafahamu Namungo ipo kwenye kiwango bora kwa sasa na watakuwa kwenye uwanja wa ugenini, lakini wamejipanga kuwakabili.

OFISA HABARI WA YANGA, ALLY KAMWE ATOA TAMKO

yangasc------------------------------------------ (-)
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema wameweka mikakati mizito ya kuhakikisha wanakusanya pointi zote 12 katika michezo yao ya mwezi huu Machi.

Ally amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo huo wa kesho Ijumaa na lengo lao kubwa litakuwa kupata pointi tatu muhimu.

Pamoja na hayo, Ally amechukua nafasi hiyo kuwaomba mashabiki wao kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanasafiri na kujitokeza kwa wingi kesho Ijumaa mkoani Lindi kwa ajili ya kuispoti timu yao.

“Baada ya kumaliza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo tunasubiri kujua ni nani tutapangwa naye kwenye Robo Fainali, tunarejea kwenye Ligi Kuu na ratiba yetu inaanza Ijumaa tutashuka dimbani kuikabili Namungo kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao utapigwa katika Uwanja wa Majaliwa.”

“Tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kutusapoti kama amabavyo imekuwa kawaida yao,” amesema Ally.

 

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.