Ligi Kuu ya Tanzania bara inakaribia kumalizika ambapo kesho Juni 6 pamoja na Ijumaa Juni 9,2023 timu zote 16 zitashuka dimbani kusaka ushindi ambao unaweza kubadili msimamo lakini pia kuboresha takwimu zao za msimu wa 2022/23, ikiwemo Yanga, simba, Azam Fc na Singida Big Stars.
Kwa timu zilizopo juu ambazo ni Yanga Bingwa) na Simba (mshindi wa pili) kwao hakuna kitakachoathirika hata kupitia matokeo yoyote watakayoyapata bali ni kuboresha alama walizonazo lakini kwa Azam Fc na Singida Big Stars wao wanafukuzana wakitofautiana alama tatu hivyo mechi mbili zinaweza kumshusha mmoja na kumpandisha mmoja lakini hazitowaondoa katika nne bora.
Klabu hizo nne za juu zimeshakamilisha safu ya timu zitakazo iwakilisha Tanzania bara kwenye michuano ya Afrika,lakini bado kuna mchakato unaoendelea kwa timu ambazo hazijawa na uhakika wa kusalia katika Ligi Kuu msimu ujao.
Wakati heka heka zikiendelea kwa Klabu nyinginezo, tunafahamu msimu unapomalizika huwa zinatolewa tuzo kwa wachezaji waliofanya vizuri kuliko wengine hivyo mechi zilizosalia pia zinatumiwa na nyota hao katika kuhakikisha kwamba wanaboresha takwimu zao zinazochagiza kupata ushindi kwenye vinyang’anyiro walivyoteuliwa.
Mfano tukianzia kwenye eneo la walinda mlango kinara kwa kufanya vyema ni Djigui Diarra wa Yanga na amekuwa muhimili katika milingoti mitatu yatimu ya Wananchi ambapo ndani ya msimu huu ndiye kinara wa kucheza mechi nyingi pasipo kuruhusu mabao(Clean Sheets 16).
Diarra ambaye ni raia wa Mali,ameendeleza alipoishia msimu uliopita ambapo alipewa tuzo ya kipa bora wa msimu wa 2021/22 ambapo hakuruhusu bao katika michezo 15 (Clean Sheets 15) za Ligi Kuu ya Tanzania bara hivyo msimu huu ameipiku rekodi yake ya msimu uliopita.
Msimu uliopita Diarra aliwapiku AbdulTwalib Msheri aliyemaliza na Clean Sheets 12 naye Aishi Manula alimaliza msimu akiwa na Clean Sheets 11.
Katika msimu huu Diarra anachuana na Aishi Manula wa Simba ambaye hajaruhusu bao katika michezo 14 msimu huu naye Bennedict Haule wa Singida Big Stars ambaye hajaruhusu bao katika michezo 12 ya Ligi Kuu Tanzania bara.
Upande wa mabeki wapo Henock Inonga, Mohamed Hussein na Shomari Kapombe wote kutoka Simba na Dickson Job na Bakari Mwamnyeto na hawa ndio wanaowania tuzo ya beki bora msimu unaomalizika.
Henock Inonga ndiye beki bora wa msimu uliopita katika Ligi Kuu,na msimu huu ameendeleza kile alichokifanya kwa kuwa muhimili katika enelo la ulinzi wa kati na kuifanya Simba kuwa timu iliyoruhusu bao chache zaidi katika NBC Premier League sawa na Yanga(15).
Amekuwa mchezaji wa mfano katika kuzuia,kutoa maelekezo kwa wenzake hata pale ambapo Joash Onyango hakuwa katika kiwango kizuri lakini Inonga yeye alikuwa kiongozi na kufuta madhaifu hayo.
Shomari Kapombe amehusika kwenye mabao takribani matano(Assist) vilevile hakuwa na ingia toka kwenye kikosi cha Simba,takwimu zake zinambeba naye amekuwa na msimu mzuri sana.
Mohamed Hussein Zimbwe Jr katika moja ya mabeki bora wa kushoto jina lake halitosahaulika na msimu wa 2018/19 alipewa tuzo ya mchezaji bora,hajawahi kushuka katika kiwango bali amekuwa akipata changamoto tu ,nayeye amehusika kwenye mabao matano msimu huu.
Dickson Job wa Yanga,huu ni msimu ambao amebadilishiwa majukumu yake ya beki wa kati na akapelekwa pembeni(upande ambao amekuwa akitumika zaidi Djuma Shaaban na Kibwana Shomari) na mara zote amefaulu mtihani wa Kocha Nasreddine Nabi,ni beki bora kwenye eneo la kulinda,kuzuia mashambulizi .
Ukiachana na hao walio orodheshwa kuwania tuzo ya beki bora, lakini kwa Azam Fc walikuwa na Daniel Amoah ambaye amekuwa na uwezo binafsi,jitihada,na amedhihirisha ni moja ya mabeki hodari wa kati katika Ligi Kuu msimu huu.
Bakari Mwamnyeto wa Yanga yeye alipitia changamoto mwanzo wa msimu kutokana na matatizo ya kifamilia jambo ambalo lilisababisha kukaa benchi kwa kipindi Fulani, lakini kadri muda ulivyosogea alirejesha ubora wake na ndiye nahodha wa Yanga wa mfano na ameuongoza ukuta wa Yanga kuwa imara na wameruhusu bao 15 tu msimu huu.
Idara ya Viungo, Saido Ntibazonkiza wa Simba anazo takwimu bora sana, amehusika katika mabao 22, akifunga magoli 10 na pasi za mabao 22.
Ntibazokinza ameonyesha anao uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi tena, tangu akiwa katika Klabu ya Geita Gold na katika dirisha dogo akajiunga na Simba ambapo moja kwa moja akachukua nafasi na kufanya makubwa hadi sasa.
Ukimzungumzia Saido basi hutoacha kumzungumzia kinara wa pasi za mabao katika klabu ya Simba, Clatous Chama. Mchezaji huyu ndiye pekee mwenye assist 16, lakini hutoacha kumtaja Muzamiru Yassin aliyehusika kwenye mabao 8, na ndiye injini ya Simba katika idara ya kiungo cha uzuiaji.
Stephane Aziz Ki wa Yanga takwimu zake zinambeba katika eneo hili ambapo katika michezo 23 ya Ligi Kuu amehusika katika mabao 13, amefunga magoli 9, na kutengeneza nafasi 4, jambo ambalo linadhihirisha pia amekuwa na mchango mzuri licha ya kuanzia benchi katika michezo kadhaa na Klabu yake ndio bingwa wa msimu.
Nyota mwingine ambaye haimbwi sana ni Khalid Aucho. Mchezaji huyu raia wa Uganda, ndiye mtu ambaye aliyeifanya Yanga itulie katika idara ya kiungo. Uwezo wake wa kuituliza timu, kupiga pasi za usahihi fupifupi na ndefu umewafanya Yanga wawe na utulivu sana katika eneo la kati kati na timu kushambulia kwa namna wanavyotaka.
Pale Azam kuna kiungo anayejulikana kama James Akaminko ambaye inawezekana ndiye kiungo bora wa ukabaji katika Ligi Kuu Tanzania bara.
Singida Big Stars inaye kiungo wa kibrazil, Bruno Gomes mwenye bao 9 na kutengeneza bao moja na ametajwa kuwania tuzo ya kiungo bora na baada ya kuwa na msimu mzuri anahusishwa zaidi na Klabu za Kariakoo(Simba na Yanga) tunaweza kumtaja kuwa moja ya wachezaji bora sana katika idara hiyo msimu huu.
Amedhihirisha katika mechi kadhaa kubwa lakini na hata nyinginezo kwa bahati mbaya Azam Fc hawakuwa na msimu bora katika maeneo mbalimbali lakini kama mchezaji alifanya makukumu yake kwa kiwango cha juu.
Idara ya ushambuliaji ukimtazama Fiston Mayele unaweza kumtaja ndiye mashinde ya kupachika mabao na ndiye kinara kwa kuweka kambani bao 16 na hiyo ni rekodi yake katika Ligi Kuu ambapo msimu uliopita licha ya kutotwaa tuzo ya ufungaji bora lakini alifikisha idadi hiyo.
Iwapo Moses Phiri asingekumbwa na majeraha leo tungekuwa tunazungumza mengine kwakuwa katika kipindi alichokuwa na afya yake alishapachika bao 10 na alifukuzana vilivyo na kinara Fiston Mayele.
Pale Azam yupo Prince Dube mwenye mabao 6 na ametoa assist 4. Mchezaji huyu ni mshambuliaji wa daraja la juu na inawezekana katika mechi hizi mbili za kumaliza msimu zikaboresha takwimu zake.
Mechi hizi zote za NBC Premier League za kesho kati ya Mbeya City VS Yanga, Ihefu VS Geita Gold, Simba VS Polisi Tanzania, Mtibwa VS Kagera, Singida BS VS Ruvu Shooting, Prisons VS KMC, Coastal Union VS Azam, Namungo VS Dodoma zipo kwenye Sportpesa.co.tz.

