- Yanga SC ikimalizana na JKT Tanzania kwa kupata ushindi itakata tiketi kutinga hatua ya fainali ambapo itakuwa inasubiri mshindi kati ya Simba SC ama Singida Black Stars.
- Simba SC ikipata ushindi dhidi ya Singida Black Stars, Kariakoo Dabi itapigwa kwenye mchezo wa fainali ya CRDB Federation Cup
- JKT Tanzania wamegomea unyonge hesabu zao kupata ushindi mbele ya Yanga SC.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga SC amebainisha kuwa kwenye tuzo ya ufungaji bora wachezaji wa timu hiyo wanafunga mabao mazuri kuliko wapinzani wao ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara 2024/25 huku hesabu kubwa zikiwa kwenye mchezo wa nusu fainali CRDB Federation Cup utakaowakutanisha Yanga SC vs JKT Tanzania Mei 18 ambapo Kariakoo Dabi yanukia ikiwa timu za Kariakoo zitapata matokeo kwenye mechi zao.

Yanga SC inayonolewa na Kocha Mkuu Miloud Hamdi, Mei 18 2025 itakuwa na kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa saa 10:00 jioni huku wakiwa ni mabingwa watetezi. Ikiwa Yanga SC itapata ushindi kwenye mchezo huo Kariakoo Dabi inaweza kunukia kwenye fainali endapo Simba SC itapata matokeo kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars.
Mei 16 2025 msafara wa Yanga SC ulitia timu Tanga kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. Wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho ambacho tayari kimeanza maandalizi ya mwisho ni Khalid Aucho, Pacome, Djigui Diarra, Jonas Mkude, Dennis Nkane ikiwa ni miongoni mwa waliopo.
Yanga SC na JKT Tanzania mechi yao ya mwisho
Wababe hawa wawili mechi yao ya mwisho kukutana ilikuwa kwenye ligi mchezo uliochezwa Uwanja wa Isahmuyo baada ya dakika 90 ubao ulisoma JKT Tanzania 0-0 Yanga SC. Waligawana pointi mojamoja. Ipo wazi kwamba JKT Tanzania ni timu pekee ambayo iliambulia pointi moja mbele ya Yanga SC kwa kuwa baada ya hapo kwenye mechi zilizofuata Yanga SC haikupata sare tena ndani ya ligi.

Mchezo huo ulichezwa Februari 10 2025, rekodi zinaonyesha kuwa ziliongezwa jumla ya dakika 9 kwa kuwa kipindi cha kwanza ziliongezwa tatu na kipindi cha pili ziliongezwa dakika 6.
Inahusiana na hii:Wakali Yanga wamepeta dakika 1,800, kazi inaendelea – SportPesa Tanzania
JKT Tanzania wanataka ushindi mbele ya Yanga SC
JKT Tanzania, kupitia kwa Ofisa Habari, Masau Bwire wamebainisha kuwa hesabu kubwa ni kupata ushindi mbele ya Yanga SC kwa kuwa wana kikosi imara cha ushindani na malengo ni kutwaa taji hilo.
Bwire ameweka wazi kuwa kukosa kwao taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 kunawapa nguvu kuongeza ushindani kwenye CRDB Federation Cup ili wacheze mashindano ya kimataifa.
“Tumekosa ubingwa msimu wa 2024/25 haya yalikuwa malengo yetu mwanzo wa msimu ila kwa kuwa tupo kwenye CRDB Federation Cup huku tutapambana kupata matokeo na kutwaa ubingwa.”
Yanga SC kuhusu nusu fainali dhidi ya JKT Tanzania
Kamwe amebainisha kuwa kwenye mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania wataingia kwa tahadhari kutafuta matokeo mazuri kwa kuwa wanaamini wanakutana na timu yenye ushindani.
“Mchezo wetu wa nusu fainali CRDB Cup tunahitaji ushindi na tutaingia kwa nidhamu kubwa kuwakabili wapinzani wetu. Ikiwat imu imepambana mpaka kufika nusu fainali hiyo ni imara na bora hivyo tukishinda tutaanza hesabu kuelekea fainali.”
Kuhusu ufungaji bora ndani ya ligi 2024/25
Rekodi zinaonyesha kuwa 2023/24 tuzo ya ufungaji bora ilikuwa mikononi mwa kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Aziz Ki ambaye alifunga jumla ya mabao 21 na alitoa pasi 8 za mabao baada ya kucheza jumla ya mechi 27.

Msimu wa 2024/24 Ki ambaye alitwaa tuzo ya mchezaji bora na jina lake kutajwa kwenye kikosi bora na Yanga SC ilitwaa ubingwa wa ligi bado yupo ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi akiendelea kutimiza majukumu yake.
Ni mabao 9 kafunga akitengeneza jumla ya pasi 7 za mabao akihusika kwenye mabao 16 kati ya mabao 71 ambayo yamefungwa na timu hiyo inayoongoza ligi na pointi zake kibindoni ni 73 baada ya kucheza mechi 27.
Huyu hapa kinara mbio za ufungaji bora 2024/25
Kinara wa utupiaji kwa sasa ni Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC mwenye mabao 15 akiwa katengeneza pasi saba za mabao akihusika kwenye mabao 22 kati ya 62 yaliyofungwa na Simba SC.

Kwa upande wa kikosi cha Yanga SC kuna mastaa wawili ambao wametupia mabao 13, Clement Mzize ambaye ni mzawa na Prince Dube rai awa Zimbabwe hawa wote wamekuwa imara kwenye kufunga mabao.
Kamwe amesema kuwa mabao ambayo yanafungwa na wachezaji wa Yanga SC ni ya viwango vikubwa yanavutia kuyatazama na hakuna mfungaji kukaa peke yake na mlinda mlango kisha anachagua eneo la kufunga.
“Kwenye hili la ufungaji bora unaona kwamba ni kazi kubwa inafanywa na wafungaji wetu, mabao ambayo yanafungwa na wachezaji wetu yanafurahisha na ni mazuri kwa kuwa hayatokani na mfungaji kusimama yeye mwenyewe na mlinda mlango huku wachezaji wengine wakiwapisha.
“Haya ni mabao ambayo yanafungwa kwa mipango mizuri ya wachezaji na wafurahi kufanya kazi kubwa wakiwa uwanjani na bado vita inaendelea.”
Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC mwenye mabao 15 kati ya hayo ni mabao sita kafunga kwa mikwaju ya penati, mabao 14 kafunga kwa mguu wa kulia na bao moja kafunga kwa pigo la kichwa ndani ya ligi ilikuwa mchezo dhidi ya Pamba Jiji, Uwanja wa KMC Complex.

