Joshua Mutale BudoJoshua Mutale Budo
  • Dakika 270 kukamilika kwa Simba SC kushuka uwanjani kusaka pointi tatu ambazo zinasakwa na wapinzani wao kwenye mechi za viporo.
  • Pamba Jiji wanahasira kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza wabainisha kuwa hawashuki daraja.
  • Simba SC mwendo wao uleule msako wa ushindi ndani ya dakika 90 watangaza vita nzito uwanjani.

Kivumbi kingine kinatarajiwa kupigwa Mei 8 2025 Uwanja wa KMC Complex kwa wababe wawili kuvaana uwanjani Simba SC vs Pamba Jiji. Msako wa pointi tatu uwanjani ikiwa ni mchezo wa tatu mfululizo kwa Simba SC utakaokamilisha dakika 270.

Ateba KMC
Ateba mshambuliaji wa Simba SC mwenye mabao 10 ndani ya ligi msimu wa 2024/25. Source: Simba SC.

Ikumbukwe kwamba huu ni mchezo wa mzunguko wa pili baada ya ule wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, ubao kusoma Pamba Jiji 0-1 Simba SC.

Ngoma ilipigwa Novemba 22 2024 kwa wababe hawa wawili kuvuja jasho uwanjani na shujaa alikuwa ni Leoenl Ateba ambaye alifunga bao la ushindi likiwapa Simba SC pointi tatu mazima. Simba SC inacheza mechi zake za viporo ilianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC kisha kete iliyofuata ilikuwa JKT Tanzania 0-1 Simba SC.

Ugumu kwenye nafasi

Wababe hawa wawili wanakutana kila mmoja akiwa kwenye nafasi ngumu katika kutimiza jambo lake analolipigia hesabu.

Kibu Prosper
Kibu Prosper kiungo mshambuliaji wa Simba SC 2024/25. Source: Simba SC.

Simba SC inapiga hesabu za kutwaa taji la Ligi Kuu Bara ambalo lipo mikononi mwa Yanga SC yenye pointi 70 kibindoni baada ya kucheza mechi 26.

Ni mechi 24 Simba SC imecheza ikiwa na pointi 63 ndani ya msimu wa 2024/25 na ilitoka kuvuna pointi tatu dhidi ya JKT Tanzania mchezo uliochezwa Mei 5 2025 Uwanja wa Isamuhyo, Mbweni Dar.

Safu ya ushambuliaji ya Simba SC ni mabao 55 imetupia kimiani ikiwa nit imu namba mbili kwa timu zenye mabao mengi na katika hay oni mabao 51 wachezaji wa timu hiyo walifunga wakiwa ndani ya 18 na mabao manne wametupia wakiwa nje ya 18.

Neno la kocha msaidizi Seleman Matola

Seleman Matola, kocha msaidizi wa Simba SC amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Pamba Jiji wanauchukulia kwa umakini mkubwa malengo ni kupata pointi tatu.

“Tumetoka kupata ushindi kwenye mchezo wetu ulIopita dhidi ya JKT Tanzania ambao ulikuwa mgumu. Matokeo yaliyopita tumesahau kuna mazuri na makosa ambayo tunayafanyia kazi.

“Muhimu ni kuona kwamba tunapata matoke dhidi ya Pamba Jiji kwani hautakuwa mchezo mwepesi kutokana na uimara wa mpinzani wetu kwani naye anahitaji pointi tatu.Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwapa nguvu wachezaji uwanjani.”

Pamba Jiji vita yao

Pamba Jiji inapambana kubaki ndani ya ligi ikiepuka kikombe cha kucheza play off ama kushuka jumlajumla kwa kuwa haipo kwenye nafasi nzuri ndani ya msimamo.

Pamba Jiji'
Pamba Jiji wakiwa kwenye mazoezi ya mwisho Uwanja wa KMC Complex. Source: Pamba Jiji.

Baada ya kucheza mechi 26 kibindoni ina pointi 27 ikiwa nafasi ya 13 katika msimamo ambayo ni nafasi yakucheza play off ikiwa itasalia hapo mpaka mzunguko wa pili ukigota mwisho.

Mechi ambazo ilipata ushindi ni 6, sare ilikuwa kwenye mechi 9 na mechi 11 ilipoteza ndani ya msimu huku safu ya ushambuliaji ikitupia mabao 17 na ukuta umeruhusu mabao 27.

Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Pamba Jiji waliruhusu bao moja wakipoteza pointi tatu wakiwa nyumbani hivyo hesabu zao itakuwa kwenye kulipa kisasi kuelekea mchezo wa mzunguko wa pili.

Neno la Pamba Jiji

Fred Felix Kocha Mkuu wa Pamba Jiji ameweka wazi kuwa wanatambua ugumu wa mchezo wao dhidi ya Simba SC ila wana imani kuwa hawatashuka daraja.

“Tunatambua ugumu wa mchezo lakini vijana wangu wako tayari kwa ajili ya kupambana na niwaote wasiwasi Wanamwanza na mashabiki wa Pamba Jiji kuwa timu hii haishuki daraja.”

Wachezaji wakuchungwa

Ahoua Jean

Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids kahusika kwenye mabao 19  kati ya 55 yaliyofungwa na timu hiyo, kafunga 12 na pasi 7 za mabao.

Kaseke ana maseke

Deus Kaseke
Deus Kaseke nyota wa Pamba Jiji mwenye uzoefu na ligi kwenye maandalizi ya mwisho. Source: Pamba Jiji.

Pamba Jiji ambao ni mabingwa wa Muungano 1990 wanaye nyota Deus Kaseke ambaye huyu ana uzoefu mkubwa na mechi kubwa aliwahi kucheza Yanga SC ambao ni watani wa jadi wa Simba SC. Sio mchezaji wakubezwa kutokana na makeke yake kwenye kubadilisha usomaji wa ubao wa matokeo.

Mei ratiba ipo namna hii

KMC vs Simba SC, Mei 11 2025, Uwanja wa KMC Complex.

Mei 12 2025

Tanzania Prisons vs Coastal Union, Uwanja wa Sokoine.

Kagera Sugar vs Mashujaa FC, Uwanja wa Kaitaba.

Hizi hapa kupigwa Mei 13 2025

JKT Tanzania vs Fountain Gate, Uwanja wa Isamuhyo.

KenGold FC vs Pamba Jiji, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Yanga SC vs Namungo, Uwanja wa KMC Complex.

Azam FC vs Dodoma Jiji, Uwanja wa Azam Complex

Mei 14 2025

Tabora United vs KMC, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Simba SC vs Singida Black Stars, Uwanja wa KMC Complex.

Share this: