- Mkandaji Kibu Dennis kiungo wa Simba SC mwenye mabao mawili ndani ya ligi anatajwa kuwa kwenye rada ya timu Ulaya.
- Mkali wa mabao ndani ya Singida Black Stars, Jonathan anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga SC.
- Nyota aliyecheza Yanga SC na Simba SC Jean Baleke kwenye anga za Namungo.
Thamani ya wachezaji huongezeka kulingana na kile wanachofanya ndani ya uwanja jambo ambalo linafanya baadhi ya wachezaji kutoka ndani ya Ligi Kuu Bara saini zao kuwindwa na timu za Bongo na Ulaya.

Maisha ya mchezaji ni mpira ambapo akipata timu mpya ni fursa kwake kupata changamoto mpya ikiwa atabaki ataongezewa mshahara kulingana na makubaliano kwenye mkataba wake.
Hapa tunakuletea baadhi ya orodha ya wachezaji ndani ya ligi wanaotajwa kuwa kwenye rada ya timu mbalimbali Bongo na Ulaya ikiwa ni tetesi namna hii:-
Feisal Salum
Feisal Salum ni mkali wa pasi za mwisho ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa mzawa mwenye kasi kubwa kwenye eneo hilo. Sio kutengeneza pasi za mwisho pekee bali hata kufunga anajua huku mguu wake wenye nguvu zaidi ukiwa ni ule wa kulia ndani ya uwanja.
Kiungo wa mpira Feisal Salum katengeneza jumla ya pasi 13 za mabao na pasi yake ya kwanza alitoa kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex ilikuwa dakika ya 19 alimpa kiungo mshambuliaji Idd Nado.
Ipo wazi kwamba Nado ni mfungaji wa bao la kwanza ndani ya kikosi cha Azam FC kwenye ligi msimu wa 2024/25 alipachika bao hilo dhidi ya KMC mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex wakiwa kwenye msako wa pointi tatu muhimu zilizokwenda Azam FC.
Kiungo Fei kwenye ligi katupia jumla ya mabao manne. Azam FC imetupia jumla ya mabao 43 hivyo Fei kahusika kwenye mabao 17. Ukuta wa Azam FC umeruhusu mabao 17 yakufungwa.
Ikumbukwe kwamba 2023/24 Feisal yeye alifunga jumla ya mabao 19 alikuwa ni mzawa namba moja kufunga mabao mengi, mabao 15 yamesalia kwa Fei kuvunja rekodi yake mwenyewe aliyoandika msimu uliopita. Nyota huyu anatajwa pia kuwa kwenye rada za Simba SC.
Aziz Ki

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz Ki anatajwa kuwa miongoni mwa nyota ambao watasepa ndani ya ligi namba nne kwa ubora Afrika msimu utakapogota mwisho kutokana na ofa ambazo zipo mezani. Inaelezwa kuwa Kaizer Chiefs wanahitaji huduma ya kiungo huyo mwenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto.
Tetesi zinaeleza kuwa Aziz huenda akapewa mkono wa asante ndani ya Yanga SC kutokana na dau kubwa ambalo limewekwa na mbali na Kaizer Chiefs inaelezwa kuwa kuna timu kutoka Uarabuni nayo inahitaji saini ya nyota huyo wa Yanga SC.
Clement Mzize
Mshambuliaji namba moja ndani ya ligi kwenye eneo la utupiaji akiwa na mabao 13 Clement Mzize yeye anatajwa kuwa kwenye hesabu za Wydad Casablanca ya Morocco. Mzize ni chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Miloud Hamdi ndani ya kikosi cha Yanga.
Taarifa zinaeleza kuwa nyota huyo amekuwa akipigiwa chapuo na Wydad kwa muda mrefu wakiwa wanahitaji saini yake kutokana na uwezo alionao kwenye eneo la ufungaji jambo linaloongeza nguvu kwake kuwa kwenye hesabu za saini yake kuwindwa.
Jean Baleke

Mshambuliaji huyu wa zamani wa Yanga na Simba anatajwa kuwa kwenye rada za Namungo ambao walikuwa wakitajwa kuhitaji huduma yake kwenye dirisha dogo na mpango kazi huo ukashindikana kwake kuibuka huko.
Kwa sasa yupo huru baada ya kupewa mkono wa asante ndani ya kikosi cha Yanga, Akiwa na uzi wa Yanga alipachika bao moja pekee ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union wakikomba pointi tatu ugenini.
Kibu Dennis

Kiungo mshambuliaji wa Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu,Fadlu Davids ni chaguo la kwanza akiwa fiti. Ilikuwa inatajwa kwamba watani zao wa jadi Yanga SC walikuwa wanahitaji huduma yake jambo ambalo likawafanya wamuongezee mkataba kuendelea kuwa ndani ya Simba SC.
Alipata timu Ulaya ambayo ilikuwa inahitaji huduma yake mpango huo ulikwama. Kwenye ligi kafunga mabao mawili ilikuwa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.
Inaelezwa kuwa timu mbalimbali zinatajwa kuwa kwenye hesabu za kuinasa saini ya Kibu ambaye ni mchezaji mwenye nguvu akiwa uwanjani katika kutimiza majukumu yake.
Jonathan Sowah
Mshambuliaji namba moja ndani ya kikosi cha Singida Black Stars akiwa katuma jumla ya mabao 11 msimu wa 2024/25. Kwenye mabao ambayo amefunga Sowah hayo 11 alimtungua pia kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra katika mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.
Kwenye mchezo huo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 2-1 Singida Black Stars, pointi tatu zilibaki kwa Yanga SC inayoongoza ligi ikiwa na poiti 70 na Singida Black Stars walipoteza pointi tatu mazima huyu anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga SC.

