AZAM FC V Yanga, Mzizima Dabi inatarajiwa kuwakutanisha wanaume 22 ndani ya uwanja katika dakika 90 za kazi kusaka pointi tatu muhimu huku kiungo mshambuliaji Khalid Aucho akikosekana kwa kuwa alipata maumivu ya nyama za paja kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa KMC Complex.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa mechi zake mbili za hivi karibuni ilipata ushindi ilikuwa dhidi ya Tabora United 0-3 Yanga na ule dhidi ya Coastal Union, huku Azam FC ikipata ushindi dhidi ya Ken Gold kwa mabao 2-0 na ilipoteza dhidi ya Singida Black Stars kwa kufungwa bao 1-0.
AZAM FC V YANGA REKODI

Azam FC kwenye msimamo ni nafasi ya tatu baada yakucheza mechi 25 kibindoni ina pointi 51. Safu ya ushambuliaji imetupia mabao 38 na ukuta umeruhusu kufungwa jumla ya mabao 13 ikiwa ni timu namba tatu kuruhusu mabao machache ndani ya ligi.
Ushindi kwa Azam FC ni kwenye mechi 15 mchezo wake wa kwanza kukomba pointi tatu ilikuwa dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex na mtupiaji wa bao la kwanza ni Idd Nado dakika ya 19 akitumia pasi ya Feisal Salum waliposepa na pointi tatu mazima ugenini.
Kwenye mechi 6 matajiri hawa wa Dar waligawana pointi mojamoja huku wakipoteza jumla ya mechi nne waliposhuka uwanjani kwenye msako wa pointi tatu muhimu. Gibrill Sillah alikuwa mfungaji wa bao pekee la ushindi kwa Azam FC Uwanja wa Azam Complex mzunguko wa kwanza. Yanga wataingia kwa hesabu za kulipa kisasi na Azam FC kulinda rekodi.
MKALI WA PASI ZA MWISHO
Kwa wababe hawa wawili kinara wa pasi za mwisho ni kiungo Feisal Salum ambaye yupo ndani ya kikosi cha Azam FC akiwa katoa jumla ya pasi 12 ambazo zilileta mabao ndani ya timu hiyo na katupia jumla ya mabao manne.

Fei kahusika kwenye mabao 16 kati ya 38 yaliyofungwa na timu hiyo, msimu wa 2023/24 alifunga mabao 19 akiwa ni mtupiaji namba mbili ndani ya ligi na kinara alikuwa ni Aziz Ki wa Yanga ambaye alitupia mabao 21.
YANGA REKODI ZAO HIZI HAPA
Yanga chini ya Kocha Mkuu,Miloud Hamdi ni vinara kwenye ligi wakiwa na pointi 64 baada ya kucheza jumla ya mechi 24 ndani ya msimu wa 2024/25. Safu ya ushambuliaji ya Yanga ni namba moja katika kutupia mabao mengi ambayo ni 62.
Ushindi ni kwenye mechi 21, sare moja ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania, walipoteza mechi mbili ilikuwa dhidi ya Tabora United na timu ya kwanza kukomba pointi tatu mazima ni Azam FC kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Ukuta wa Yanga unaongozwa na Dickson Job ni namba mbili kwa kuruhusu mabao machache ambayo ni 9, timu namba kwa kufungwa mabao machache kwa sasa ni Simba ikiwa imetunguliwa mabao 8 baada yakucheza mechi 22.
WAKALI WA NYAVU YANGA

Wakali wakucheka na nyavu ndani ya kikosi cha Yanga ni washambuliaji wawili ambao wote wametupia mabao 11 ndani ya uwanja kwenye mechi za ushindani ambazo walishuka uwanjani msako wa pointi tatu muhimu.
Prince Dube mchezaji wa zamani wa Azam FC na Clement Mzize ambaye ni mshambuliaji mzawa mwenye mabao mengi ndani ya ligi msimu wa 2024/25 ambao una ushindani mkubwa.
KEN GOLD V TANZANIA PRISONS
Ken Gold FC dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Sokoine. Ken Gold kwenye msimamo wa ligi ipo nafasi ya 16 wakiwa kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja na pointi zao 21. Imecheza mechi 25 ushindi mechi tatu, sare 7 kupoteza kwenye mechi 15.
Safu ya ushambuliaji ya Ken Gold yenye Obrey Chirwa imetupia mabao 15 na ukuta umeruhusu mabao 45 ikiwa ni timu namba mbili kufungwa mabao mengi vinara wakiwa ni Fountain Gate ambao wameruhusu mabao 47.

Inakutana na Tanzania Prisons ambayo ipo nafasi ya 15 na pointi 21 baada yakucheza mechi 25, ushindi katika mechi tano, sare 6 ikipoteza kwenye mechi 14 safu ya ushambuliaji imetupia mabao 15 na ukuta umeruhusu mabao 34.
DODOMA JIJI V KAGERA SUGAR
Dodoma Jiji dhidi ya Kagera Sugar mchezo huu unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kwenye msako wa pointi tatu muhimu. Dodoma Jiji wenyeji baada yakucheza mechi 25 ni pointi 31 wamekusanya wakiwa nafasi ya 7 kwenye msimamo.
Ushindi katika mechi 8 wakigawana pointi mojamoja katika mechi 7 huku wakipoteza pointi tatu kwenye jumla ya mechi 10 ndani ya ligi msimu wa 2024/25.
Safu ya ushambuliaji imetupia jumla ya mabao 27 huku ukuta ukiruhusu kufungwa mabao 35. Inakutana na wapinzani wao Kagera Sugar chini ya Kocha Mkuu, Juma Kaseja ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa zamani wa Simba, Yanga, KMC.

Ni mechi 25 Kagera Sugar imeshuka uwanjani, ikipata ushindi katika mechi 5, iligawana pointi mojamoja kwenye mechi 7 na ilipoteza mechi 13 kibindoni ina pointi zake 22 ikiwa nafasi ya 14 ipo kwenye mstari wa kucheza play off.

