Jonathan IkangaJonathan Ikanga

YANGA hawacheki na yoyote huku wamebainisha kuwa ingizo lao jipya katika dirisha dogo 2025 hatakuwa sehemu ya mechi za kimataifa na atakuwa hapo kwa kazi maalumu kupima umri wa wachezaji ambao wamegoma kustaafu.

Ni Jonathan Ikangalombo ni ingizo jipya ndani ya Yanga akiwa ni mchezaji wa pili kutambulishwa ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Sead Ramovic.

Aziz Stephan
Aziz Stephan kiungo wa Yanga kwenye majukumu yake kimataifa: Source: Yanga.

Yanga inayodhaminiwa na SportPesa imekuwa na mwendelezo mzuri kwenye mechi zake za hivi karibuni kwa kuwa katika mechi sita mfululizo za ligi na kimataifa haijapoteza zaidi ya kuambulia matokeo ya ushindi katika mechi tano na sare mchezo mmoja dhidi ya TP Mazembe ugenini.

Tayari wachezaji wote wapya waliotambulishwa ndani ya Yanga kwenye dirisha dogo wameanza kazi na wachezaji wengine lakini Jonathan hatakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya MC Alger ambao ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sababu kubwa ya nyota huyo ambaye ni winga kutokuwa kwenye mpango kazi wa kikosi hicho kinachosaka nafasi ya kucheza robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ni kushiriki mashindano hayo kwenye hatua ya awali.

Kwa mujibu wa Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wamekamilisha usajili wa wachezaji wawili wapya kwenye dirisha dogo ambapo mmoja atatumika kwenye mechi za kimataifa na mwingine hatacheza.

Israel
Israel Mwenda beki wa Yanga ambaye ni ingizo jipya kwenye dirisha dogo. Source: Yanga.

“Tumefanya usajili wa wachezaji wawili kwenye dirisha dogo ikiwa ni Israel Mwenda na Jonathan, Mwenda ikiwa mwalimu ataona ameingia kwenye mfumo basi atamtumia lakini huyu Jonathan hatacheza.

“Alicheza mashindano haya ya kimataifa akiwa na AS Vita kwenye hatua ya awali hivyo kanuni hazimruhusu kucheza, huyu yupo kwa ajili ya kazi maalumu kupima umri wa watu ambao hawataki kustaafu.”

DILI LA FEISAL

Fei Toto
Fei Toto kiungo wa Azam FC 2025 akiwa kwenye majukumu yake. Source: Azam FC.

Wakati dirisha la usajili likipamba moto kiungo namba moja kwa pasi za mwisho Bongo Feisal Salum alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Simba mpaka usajili unafungwa dili hilo limeonekana kuwa gumu.

Taarifa zilikuwa zinaeleza kuwa mabosi wa Simba walikuwa wanahitaji huduma yake ila dau kumpata Feisal mwenye mkataba na Azam FC lilikuwa zito jambo ambalo lilisababisha mpango kazi huo usitimie kwenye dirisha dogo hivyo labda mpaka dirisha kubwa mpango kazi unaweza kuendelea.

Ikumbukwe kwamba Feisal ni namba moja kwa nyota wenye pasi nyingi Bongo akiwa ametoa jumla ya pasi tisa za mabao na katupia mabao manne akiwa amehusika kwenye mabao 13 ndani ya Azam FC iliyofunga jumla ya mabao 25.

Azam FC kwenye msimamo ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 16 huku safu ya ushambuliaji ikiwa imetupia mabao 25 ndani ya ligi namba sita kwa ubora Afrika.

HAWA HAPA THANK YOU

Bangala Azam
Yannick Bangala beki wa zamani wa Azam FC. Source: Azam FC.

Mabosi wa Azam FC wamewapa mkono wa asante nyota wao wawili hivyo hawatakuwa nao kwenye kikosi hicho kwenye mechi za mzunguko wa pili unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.

Ni beki wa kazi Yanick Bangala ambaye aliibuka hapo akitokea kikosi cha Yanga huyu hatakuwa sehemu ya mzunguko wa pili kwa matajiri wa Dar na nyota mwingine ni Sidibe ambao hawa wote kwenye mzunguko wa kwanza hawakuwa na nafasi kikosi cha kwanza katika mechi za ushindani.

BURUDANI YA LIGI INARUDI

Pamba na Prisons
Wachezaji wa Pamba na Prisons kwenye moja ya mchezo wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25. Source: Pamba Jiji.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) imebainisha kuwa ile burudani ya ligi ambayo ilitarajiwa kurejea Machi Mosi 2025 itarejea Februari ambapo ilipangwa hivyo kutokana na ratiba ya michuano ya Kombe la Mapinduzi na fainali  fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani , (CHAN).

Taarifa hiyo iliyotolewa Januari 15 2025 ilieleza kuwa michezo ya Ligi Kuu Bara, (NBC), itarejea katika juma la kwanza Februari 2025 kwa michezo ya viporo kabla ya kuendelea na michezo ya mzunguko wa 17. Tarehe na ratiba iliyofanyiwa maboresho itatangazwa hivi karibuni.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mabadiliko hayo yamekuja baada ya Shirikisho la Soka Afrika, (CAF) kusogeza mbele fainali za CHAN kutoka Februari hadi Agosti 2025 hivyo kutoa nafasi kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuendelea na michezo ya Ligi Kuu ya NBC ambayo ilisimama kupisha fainali hizo.

 

Share this: