SIMBA inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids imeweka wazi kuwa inakwenda kukutana na mpinzani mgumu ndani ya dakika 90 kutokana na mwendo wake wa kupata matokeo mazuri kwenye mechi za nyumbani ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwa hawatafuata kinyonge.
Wakiwa na kumbukumbu ya kupata matokeo chanya kwenye mchezo waliocheza nao Bravos, Uwanja wa Mkapa Novemba 24 2024 ubao uliposoma Simba 1-0 Bravos, watakabiliana nao kwa mara nyingine, wakiwa ugenini.

Tayari kikosi cha Simba kimeanza safari kuelekea Angola kwa mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Januari 12 2025 kwa wababe hao kutoka kundi A kusaka pointi tatu muhimu katika kusaka tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali huku kocha akisema kuwa ni mchezo mgumu kwao.
“Tunakwenda kucheza mchezo mgumu hasa ukizingatia kwamba wapinzani wetu Bravos wamekuwa na mwendo mzuri kwenye mechi ambazo wanacheza wakiwa nyumbani hivyo tunakwenda kwa tahadhari na malengo ni kuona kwamba tunapata ushindi.
“Wachezaji wamekuwa wakijituma hilo tunajivunia na wanastahili pongezi licha ya ugumu ambao upo kwenye mechi zetu wamekuwa wakifanya vizuri na tunapata matokeo, bado tuna kazi kubwa ambayo tunakwenda kuifanya, kikubwa ni utayari na tunaamini kwamba tutapambana ili kupata kile tunachokifuta.”
Bravos kwenye makundi ni nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita huku Simba ni nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa bado haijakata tiketi kutinga hatua yar obo fainali hata mpinzani wake wa mwisho Constatine aliye kinara naye ana pointi 9.
HUU HAPA MSAFARA WA SIMBA
MAKIPA

Mousa Camara, Hussen Abel na Ally Salim
MABEKI HAWA HAPA
Karabou Chamou, Che Malone, Abdulazack Hamza, Zimbwe Jr, Shomari Kapombe, Kelvin Kijili
VIUNGO HAWA HAPA
Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Yusuph Kagoma, Elie Mpanzu, Augustine Okejapha, Kibu Dennis, Deborah Mavambo, Ladack Chasambi, Awesu Awesu, Jean Ahoua, Edwin Balua
HAWA HAPA KUIKOSA BRAVOS

Katika msafara huo kuna baadhi ya wachezaji ambao hawapo kwenye kikosi ikiwa ni Aishi Manula ambaye ni kipa mshambuliaji Steven Mukwala, beki wa kazi David Kameta, Joshua Mutale ambaye ni kiungo hivyo hawatakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Bravos kimataifa.
SEMAJI TAMBO TUPU

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasilano Simba amesema kuwa wanakwenda kukabiliana na Bravos wakitambua ni moja ya timu ngumu na wapo tayari kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
“Tunawafuata wapinzani wetu Bravos na tunajua kwamba sio timu nyepesi ukizingatia kwamba imekusanya pointi sita na kwenye mechi zao za nyumbani wamekuwa wakipata matokeo mazuri hilo lipo wazi kabisa.
“Kikubwa ni mashabiki kuwa watulivu kuelekea kwenye mchezo wetu kwani ushindi unahitajika n ahata tukipata alama moja itakuwa na faida kwetu ugenini lakini hatuanzi kufikiria alama moja kwa sasa tunahitaji alama tatu tukishindwa hapo tutaanza kufikiria alama moja.”
MWENYEKITI SIMBA HUYU HAPA
Murtanza Mangungu, Mwenyekiti wa Simba amesema kuwa kwa sasa mpango mkubwa ni kupata matokeo kwenye mechi zijazo hivyo masuala ya kufikiria nani atapata nini kwa sasa yawekwe kando na badala yake nguvu iwe kwenye kupata ushindi.
Ikumbukwe kwamba Simba ipo kwenye kundi ambalo lina ushindani mkubwa kwa timu tatu kuwa kwenye ubora katika mechi za kimataifa kusaka tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Licha ya Simba kuvuna pointi tisa ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi wakiwa nafasi ya pili vinara ni Costantine wenye pointi tisa mchezo ujao ni dhidi ya Bravos nafasi ya tatu na pointi 6.

Bravos ilipoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 1-0 Bravos bao la Jean Ahoua ambaye kwenye anga la kimataifa katupia mabao mawili na pasi mbili za mabao.
Mangungu amesema kuwa suala la kusema ni muda wa kutembea na calculator kwa sasa hilo inabidi liachwe na badala yake nguvu kubwa iwe kwenye kutafuta matokeo kwenye mechi zilizobaki.
“Kikubwa tumetoka kupata matokeo kwenye mchezo wetu uliopita ugenini na sasa mpango mkubwa ni kuona kwamba tunakwenda kupata matokeo ugenini,hilo ni jambo la msingi kuliko kuanza kufikiria sualala kutembea na calculator kwa sasa.
“Pongezi kwa wachezaji namna ambavyo wanapambana na kupata matokeo mazuri hili ni jambo la kujivunia na benchi la ufundi linastahili pongezi kutokana na kazi kubwa ambalo linaifanya.”
Mchezo ujao kwa Simba dhidi ya Bravos unatarajiwa kuchezwa nchini Angola, Januari 12 2025 saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki ukitajwa kuwa ni fainali kwa timu zote mbili kusaka pointi tatu.

