Fadlu DavidsFadlu Davids

WAKIMATAIFA kutoka ardhi ya Tanzania, Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids na Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Sead Ramovic watakuwa mzigoni kwenye msako wa pointi tatu muhimu ikiwa ni hatua ya makundi 2024 kila timu ikiwa kwenye karata yake ambapo Yanga ni Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba ni kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kazikazi ndani ya dakika 90 msako wa pointi tatu muhimu.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa amesema kuwa wanatambua wana mchezo mgumu mbele yao wakiwa ugenini watawakabili wapinzani wao TP Mazembe kwa umakini malengo ikiwa ni kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa TP Mazembe.

Yao
Yao beki wa kazi wa Yanga kwenye anga la kimataifa 2024. Source: Yanga.

Yanga inakibarua cha kusaka pointi tatu dhidi ya TP Mazembe mchezo wa hatua ya makundi unaotarajiwa kuchezwa Desemba 14 ikiwa ni mchezo wa tatu kwa Yanga ambayo ipo kundi A.

Kamwe amesema: “Wachezaji wapo tayari kwa mchezo wetu na tunatambua hautakuwa mwepesi kikubwa ni kuona kwamba tunapata pointi tatu muhimu. Mashabiki waliopo hapa na wale ambao wapo nje ya DR Congo tunaomba waendelee na dua kwani ushindi kwenye mchezo wetu ni muhimu na furaha kwa kila Mwananchi.”

HUYU HAPA MAXI

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli amesema kuwa wanatambua hawakupata matokeo kwenye mechi zilizopita lakini haitawafanya waingie kwenye mchezo wa leo dhidi ya TP Mazembe vichwa chini watapambana kupata matokeo mazuri.

Ipo wazi kwamba Maxi ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic kwenye mechi za ushindani yupo na kikosi nchini Dr Congo kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa saa 10:00 kwa saa za Afrika mashariki.

Maxi Nzengeli
Maxi Nzengeli kiungo wa Yanga 2024. Source: Yanga.

Katika mechi mbili ambazo ni dakika 180, Yanga ilipoteza mechi zote mbili ilikuwa Yanga 0-2 Al Hilal huu ulichezwa Uwanja wa Mkapa na  MC Alger 2-0 Yanga ni mabao manne Yanga imefungwa na safu ya ushambuliaji haijafunga bao.

Kiungo huyo amesema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kufika salama nchini DR Congo na wanaimani ya kupambana kupata matokeo dhidi ya TP Mazembe.

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama, tupo hapa Lubumbashi kwaajili ya kupambana, ni kweli hatujashinda mechi zetu za mwanzo lakini haimaanishi tukae vichwa chini, huu ni muda wa kurudi juu na kuwapa furaha wananchi, tunatambua ukubwa wa Mazembe lakini tutapambana kwaajili ya kushinda.

“Tunasema asante kwa mashabiki wa Yanga siyo rahisi kusafiri kwa basi mpaka hapa, haitakuwa rahisi lakini tunawahakikishia tutapambana sana kwaajili yao. Tunashukuru sana na tupo tayari kujitoa kwaajili yao.”

 

KOCHA HUYU HAPA RAMOVIC

Sead na Aziz
Kocha Mkuu wa Yanga 2024 Sead Ramovic akiwa na kiungo Aziz Ki. Source: Yanga.

“Malengo yetu ni kuonesha uwezo wetu na kufanya vizuri. Haijalishi wapinzani wetu wakoje, Sisi tunafahamu TP Mazembe ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri hivyo tutashuhudia mechi nzuri sana, nafahamu kuwa mchezo wa mwisho hapa Congo Yanga ilishinda lakini hatuwezi kuzungumzia yaliyopita, tunautazama mchezo kama mchezo mpya na tupo tayari kwa changamoto hii.

“Ni jambo kubwa sana ambalo mashabiki wa Yanga wamelifanya, kusafiri kwa basi kutoka Dar mpaka hapa Lubumbashi siyo rahisi, ni faraja kwetu na inatupa motisha ya kuwa tuna watu wanaotupa moyo na kutufanya tusiyumbe, kwakweli nachoweza kusema ni kwamba tupo hapa kwaajili ya kuwapa furaha, timu nzima inatambua umuhimu wa mashabiki wetu, panapo majaaliwa  tutapambana.”

SIMBA MZIGONI KWA MKAPA

Uongozi wa Simba umebainisha kuwa utaonyesha ubaya ubwela kwenye mchezo wao wa kimataifa dhidi ya SC Sfaxine kwa lengo la kufufua matumaini kutinga hatua ya robo fainali.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Desemba 15 ikiwa ni mchezo wa tatu kwa Simba katika anga la kimataifa ikiwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya CS Constantine licha ya kuanza kufunga bao la kuongoza dakika ya 24 kupitia kwa Mohamed Hussen.

Mohamed Hussen
Mohamed Hussen nahodha wa Simba aliyefunga bao kimataifa ugenini dakika ya 24. Source: Simba.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo huo na wanahitaji kupata ushindi.

“Ni ubaya ubwela kwenye mchezo wetu dhidi ya SC Sfaxine hakuna namna tumepoteza mchezo uliopita licha ya kwamba tulikuwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda ila matokeo yamepita na sasa ni hesabu kuelekea mchezo ujao.

“Tuna timu bora hivyo ni muda wa kila Mwanasimba kuinuka na kununua tiketi halafu asisahau aje uwanjani kwa kuwa huu ni mchezo muhimu na mgumu licha ya kwamba tutakuwa nyumbani kikubwa ni kuona kwamba tunapata matokeo na mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia burudani huku wakishangilia mwanzo mwisho Uwanja wa Mkapa.”

 

 

Share this: