YANGA inayonolewa na Kocha Mkuu, Sead Ramovic ambaye kakiongoza kikosi hicho kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo ni dakika 180 bila kupata ushindi ina kibarua kingine ugenini ambapo hesabu ni kupata pointi tatu muhimu ugenini.

Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa haijawa kwenye mwendo mzuri kimataifa hivyo inakibarua cha kufufua matumaini ugenini ili kuongeza nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
NENO LA SEMAJI
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa wanatambua ushindani ni mkubwa wanaamini watakwenda kupata matokeo ugenini kutokana na utayari wa wachezaji na benchi la ufundi kuwa na uhitaji wa kupata ushindi.
“Tumekuwa na matokeo ambayo sio rafiki kwetu hasa kupoteza mechi mbili hilo lipo wazi na halijatufurahisha, kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe maandalizi yapo vizuri na tunaamini kwamba tutakweda ugenini kupambania ushindi.”
HII HAPA ORODHA YA WACHEZAJI WA YANGA
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Desemba 14 2024 utakuwa ni watatu kwa Yanga kushuka uwanjani katika anga la kimataifa katika msako wa pointi tatu muhimu.
Kwenye orodha hiyo kuna makipa watatu, viungo 12, washambuliaji watatu na mabeki 7 hivyo ni msafara wa wachezaji 25 watakuwa DR Congo kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea kwenye mchezo huo muhimu.
MAKIPA
Djigui Diarra, Khomein, Aboutwalib Mshery.
MABEKI
Bakari Nondo, Dickson Job, Bacca, Yao, Nickson Kibabage, Kibwana Shomari na Boka.
VIUNGO

Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Jonas Mkude, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Dennis Nkane, Sure Boy, Farid Mussa, Sheikhan, Pacome, Clatous Chama, Aziz Ki.
WASHAMBULIAJI
Kennedy Musonda, Clement Mzize na Prince Dube.
MSIMAMO WA KUNDI
Kwenye kundi lao ambalo ni A ngoma ni nzito kutokana na kila timu kupambana kusaka tiketi ya kuting hatua ya robo fainali ipo wazi kuwa kwenye makundi ni msako wa pointi tatu na kila mmoja yupo vizuri hasa kwenye mechi za nyumbani.
Kundi A vinara ni Al Hilal wakiwa na pointi sita kibindoni wanafuatiwa na MC Alger wenye pointi nne, TP Mazembe ni pointi moja wakiwa nafasi ya tatu.
Kutoka Tanzania wawakilishi Yanga wapo nafasi ya nne wakiwa hawajakomba pointi baada ya kucheza mechi mbili ambazo ni dakika 180.
KETE YAO ILIYOPITA

Desemba 7 2024 wa kimataifa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika walipoteza kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa 5 July ukisoma MC Alger 2-0 Yanga.
Mabao yalifungwa na Ayoub Abdellaoui dakika ya 64, Soufiane Bayazid dakika ya 90. Ikumbukwe kwamba katika dakika 45 za mwanzo Yanga walicheza kwa kukaba kwa nguvu na kuziba njia za wapinzani wao.
Mchezo wa kwanza hatua ya makundi walipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan Uwanja wa Mkapa hivyo mchezo wa tatu hautakuwa mwepesi kwa tim zote mbili.
YANGA WAMEVUTA JEMBE JIPYA MAPEMA

Wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Desemba 15 2024 tayari Jangwani kuna ingizo jipya ambalo halipo kwenye msafara wa kimataifa ila tayari limeanza mazoezi na wachezaji wenzake.
Israel Mwenda ambaye ni beki ameibuka hapo akitokea kikosi cha Singida Black Stars alitambulishwa rasmi Desemba 11 2024 kuwa ni njano na kijani.
Amekutana na baadhi ya wachezaji ambao aliwahi kufanya nao kazi katika kikosi cha Simba ikiwa ni Mwamba wa Lusaka Clatous Chama, Jonas Mkude pia yupo Jean Baleke ndani ya Yanga hawa wote waliwahi kucheza ndani ya kikosi cha Simba.
Beki huyo akiwa na Singida Black Stars rekodi zinaonyesha kuwa alianza kikosi cha kwanza kwenye mechi tatu kati ya 12 ambazo timu hiyo ilishuka uwanjani ikikusanya pointi 24. Alipokuwa ndani ya Simba msimu wa 2023/24 alicheza jumla ya mechi 14 za ligi akikomba dakika 857.
Mwenda amesema ni furaha kwake kuwa kwenye changamoto mpya ndani ya kikosi cha Yanga kwa kuwa ni timu kubwa anaamini watafanya kazi kwa ushirikiano kupata matokeo mazuri.
“Ninafurahi kuwa hapa ndani ya Yanga kwa kuwa ni timu kubwa nina amini kwamba tutapata matokeo mazuri kwa ushirikiano.”

