NGOMA ni nzito kimataifa baada ya benchi la ufundi la Simba kubainisha kwamba mchezo wao kimataifa utakuwa mgumu ndani ya dakika 90 na wapo tayari kupambana kusaka ushindi katika mchezo wa mzunguko wa pili Kundi A Kombe la Shirikisho dhidi ya CS Constantine mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Chahid Hamlaoui nchini Algeria.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amebainisha kuwa hakuna kazi nyepesi kwenye anga la kimataifa kutokana na ushindani uliopo hivyo wapo tayari kukabiliana na wapinzani wao kusaka ushindi.
“Kikosi chetu kipo tayari na wachezaji wapo kwenye hali nzuri kwa ajili ya mchezo wetu ambao upo mbele yetu tunaamini itakuwa mechi ngumu tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo chanya.”
Ikumbukwe kwamba wawakilishi wa Tanzania kwenye anga la kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga waliangukia pua kwa kupoteza mchezo wa pili hatua ya makundi.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa kwenye Ligi Kuu Bara haijawa na mwanzo mzuri katika anga la kimataifa hasa kipindi cha pili ambapo rekodi zinaonyesha kuwa wamekuwa wakiruhusu mabao na kupoteza mechi hizo ndani ya dakika 180
SIMBA KAZINI
Timu zote mbili zimejikusanyia alama 3 katika michezo yao iliyopita katika kundi hilo, Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos ya Angola huku Constantine wakiishinda mchezo wao wa kwanza ugenini dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia kwa bao 1-0.
Wenyeji wa mchezo huo, CS Constantine wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria, Ligue 1 wakiwa na alama 19 katika michezo 11 msimu huu, huku wakipoteza mchezo mmoja tu kati ya michezo yao mitano ya mwisho, wakishinda jumla ya michezo mitatu na kutoa suluhu mchezo mmoja, wakifunga jumla ya mabao matano na kuruhusu mabao matatu.
Simba ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania wakiwa na alama 28 katika michezo 11 wakiwa na ushindi wa asilimia 100 katika michezo mitano ya mwisho wakishinda michezo yote wakifunga jumla ya mabao 10 bila kuruhusu bao kwenye mechi hizo za ushindani.
Aidha, katika mchezo mwingine wa kundi hilo, FC Bravos ya Angola itakuwa nyumbani kuwakaribisha CS Sfaxien ya Tunisia, huku timu zote zikitafuta ushindi wa kwanza katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa saa 1:00 kwa saa za Afrika Mashariki.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema kuwa wanamchezo mgumu dhidi ya wapinzani wao hivyo watapambana kupata matokeo chanya katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
KIKOSI KAZI CHA SIMBA

Mousa Camara, Chamou, Fabrince Ngoma, Jean Ahoua, Kapombe Shomari, Leonel Ateba, Hamza, Zimbwe Jr, Che Malone, Okejapha, Kibu D.
Hawa wachezaji wa akiba: Ally Salim, Kelvin Kijili, Nouma, Mzamiru Yassin, Mavambo, Awesu, Chasambi, Balua, Mukwala.
YANGA KURUDI BONGO

Baada ya Yanga kukamilisha kazi ugenini kwa kupoteza kwenye mchezo uliochezwa Desemba 7 2024 Uwanja wa 5 July uliposoma MC Alger 2-0 Yanga wameanza safari ya kurejea Dar kwa ajili ya maandalizi ya mechi zinazofuata.
Kwenye mchezo huo mabao yote yalifungwa kipindi cha pili kupitia kwa Ayoub Abdellaoui dakika ya 64, Soufiane Bayazid dakika ya 90. Katika dakika 45 za mwanzo Yanga walicheza kwa kukaba kwa nguvu na kuziba njia za wapinzani wao.
Mchezo wa kwanza hatua ya makundi walipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambapo katika mchezo huu uliochezwa Uwanja wa Mkapa mabao yote mawili yalifungwa pia kipindi cha pili.

Tayari msafara wa wachezaji pamoja na viongozi umeanza safari kurejea Dar miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye msafara huo ni Aziz Ki, Clement Mzize, Kennedy Musonda, Prince Dube, Clatous Chama.
SALAMU ZA PONGEZI KWA WAZIRI
Ikiwa ni muda mfupi baada ya taarifa kueleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amehamisha majukumu ya sekta ya habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yanga wametuma salamu za pongezi.
Taarifa ya uteuzi na mabadiliko ya viongozi, imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga. Taarifa hiyo imeeleza kuwa uapisho wa viongozi walioteuliwa Desemba 8 2024 utafanyika Ikulu Ndogo, Zanzibar Desemba 10, 2024.
Kupitia Insta Yanga wameandika namna hii: “Hongera Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.”

