KUELEKEA kwenye mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2025 wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamebainisha kuwa wapo tayari kupambana kwa ajili ya nembo ya Tanzania kupata matokeo mazuri uwanjani Septemba 4 2024 Uwanja wa Mkapa huku mkwanja mrefu ukiwekwa kwa kila bao ambalo litafungwa.
Ipo wazi kwamba Taifa Stars chini ya Kaimu Kocha Mkuu Hemed Morroco ina michezo miwili ya kucheza kwa ajili ya kuwania kufuzu AFCON 2025 nchini Morocco ambapo itaanza kutupa kete yake Septemba 4 2024 Uwanja wa Mkapa dhidi ya Ethiopia.
Agosti 26 2024 orodha ya wachezaji walioitwa Taifa Stars walitangazwa na benchi la ufundi huku baadhi ya mastaa wakiwekwa kando ikiwa ni pamoja na Mbwana Samatta, Simon Msuva ambao hawatakuwa kwenye mchezo ujao dhidi ya timu ya taifa ya Ethiopia.
KUHUSU MAANDALIZI

Taifa Stars wachezaji waliripoti kambini Agosti 28 2024 ikiwa ni maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Ethiopia. Miongoni mwa wachezaji waliowasili kambini Agosti 28 ni pamoja na Mohamed Hussein Zimbwe Jr, Wazir Junior, Edwin Balua, Ally Salim ikiwa ni tayari kwa kuanza mazoezi kuikabili Ethiopia na mchezo wa pili unatarajiwa kuchezwa Septemba 10 2024 itakuwa dhidi ya Guinea.
Mchezo huo dhidi ya Ethiopia utachezwa Uwanja wa Mkapa itakuwa saa 1:00 usiku ambapo mashabiki wameitwa kujitokeza kwa wingi kuwaongezea nguvu wachezaji watakaokuwa uwanjani kupambania bendera ya taifa ya Tanzania.
Juma Mgunda, Kocha msaidizi wa Taifa Stars amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri kwa wachezaji kuwa tayari kuelekea mchezo huo dhidi ya Ethiopia.
“Kuhusu mchezo wetu dhidi ya Ethiopia maandalizi yako vizuri ninaweza kusema kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 yamefikia tunaendelea kujiandaa ili kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu, wachezaji wapo tayari kuona wanafanya vizuri uwanjani.”
Mazoezi ya Stars yamekuwa yakifanyika kwenye viwanja tofauti ikiwa ni pamoja na Gymkhana hiyo ilikuwa ni Agosti 29 siku ya kwanza ya mazoezi kwa wachezaji walioripoti kambini na Agosti 30 ilikuwa kwenye Uwanja wa KMC, Complex, Mwenge.
WACHEZAJI HAWA HAPA

Edwin Balua amesema: “Kuitwa timu ya taifa ni jambo kubwa na hapo ni muhimu kupambana kwa ajili ya kupata matokeo kwani hii ni kazi ya taifa na muhimu kuona kwamba tunapata matokeo. Tupo tayari na tutashirikiana kwenye mechi zetu zote kutafuta matokeo mazuri.”
Feisal Salum amesema :”Tukutane Uwanja wa Mkapa Septemba 4 2024 tunakazi kubwa kwa ajili yakupambania nembo ya Tanzania, maandalizi yapo vizuri na tupo tayari kwa ajili ya mchezo wetu.”
HUYU HAPA OFISA HABARI WA TFF
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), Cliford Ndimbo amesema kuwa kikosi kinaendelea na maandalizi vizuri huku kila kitu kikiwa kwenye mpangilio hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Septemba 4 Uwanja wa Mkapa.
“Wachezaji wana ari kubwa kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Ethiopia na mechi wanaitaka hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa kushuhudia burudani kwenye mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2025.
“Kikosi kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya michezo yetu miwili iliyopo mbele yetu kuwania kufuzu AFCON, hili ni jambo letu na mashabiki tuna kila sababu ya kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa kushuhudia mchezo dhidi ya Ethiopia.”
DAU LAKE MASHARTI MOTO

Kwenye hamasa kwa wachezaji ili wapate matokoe mazuri maofisa wa timu mbalimbali Bongo wameungana na kuweka dau la kununua kila bao litakalofungwa na timu ya taifa ya Tanzania kwa milioni tano huku masharti ikiwa ni lazima yafungwa mabao matatu.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga, Ali Kamwe, Meneja wa Idara ya Habari Simba, Ahmed Ally, Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe wameweka wazi kuwa watatoa milioni tano kwa kila bao ambapo kutakuwa na bao la Yanga, Simba na Azam FC mezani.
Kamwe amesema hii yote ni kuonyesha kwamba wapo bega kwa bega na wachezaji pamoja na kurejesha shukrani kwa kuwa wao ni wanafaika wa bao la mama kwenye anga la kimataifa.
“Sisi ni wanufaika wa bao la mama kimataifa sasa ni jukumu letu kutoa kila bao ambalo litafungwa itakuwa ni milioni tano. Lakini ni lazima yafungwe yote matatu ili kutoa kitu kamili yaani bao la Yanga, Azam FC na Yanga. Wachezaji wanapaswa kutambua kwamba likifungwa bao moja hilo ni la Yanga, moja la Azam FC na moja la Simba, yasipotimia hela haitoki. Hii hela ngumu kidogo lazima iwe na masharti.”
ORODHA WACHEZAJI WA WA AFCON

Ally Salim Simba
Aboutwalib Mshery Yanga
Yona Amos Pamba Jiji
Lusajo Mwaikenda Azam FC
Nathaniel Chilambo Azam FC
Mohamed Hussein Simba
Dickson Job wa Yanga
Pascal Msindo wa Azam FC
Ibrahim Hamad Bacca wa Yanga
Bakari Nondo wa Yanga
Nickson Kibabage wa Yanga
Abdulmalick Zakaria wa Mashujaa
Adolf Mtasingwa wa Azam FC
Himid Mao wa Talaal El Geish ya Misri
Novatus Dismas wa Goztepe ya Uturuki
Mudathir Yahya wa Yanga
Hussein Semfuko wa Coastal Union
Feisal Salum wa Azam FC
Wazir Junior wa Dodoma Jiji
Cyprian Kachwele wa Vancouver Whitecaps ya Canada
Clement Mzize wa Yanga
Abel Josiah wa TDS TFF Academy

