
Kikosi cha klabu ya Simba ambao wamewahi kuwa na udhamini mnono wa Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa unaweza kusema wameanza ligi kwa staili ya namna yake wakizipiga mkwara timu zote nyuingine baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wao dhidi ya Tabora United.
Mchezo huo wa kwanza kwa Simba kwenye Ligi Kuu Bara 2024/25 uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex unaopatikana Mwenge, Dar es Salaam.
MCHEZO ULIKUWAJE?

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kila timu ilicheza kwa tahadhari kubwa kuhakikisha hazifanyi makosa, lakini ni Simba ndio ambao walikuwa na utawala mkubwa katika kipindi kirefu cha mchezo huo. Utawala huo wa mchezo ukawapa bao la kuongoza kupitia kwa mlinzi wa kati wa timu hiyo raia wa Cameroon, Che Fondoh Malone ambaye alifunga bao kwa kichwa dakika ya 13 baada ya kumalizia mpira wqa kona uliopigwa na kiungo Jean Charles Ahoua.
Bao hilo liliendelwea kudumu mapaka kipindi cha kwanza kinaisha, kipindi cha Simba walirudi kwa kasi wakifanikiwa kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Tabora, ambao walikuwa nyuma ya mpira kwa muda mrefu.
Ni straika mpya, Valentino Mashaka ndiye aliyeipa Simba bao la pili dakika ya 68 akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’. Bao la tatu la Simba liliwekwa kambani na kiungo wao mpya Awesu Awesu dakika ya 92 ambapo akiwa ndani ya 18 alifunga bao kali la kideoni.
MUTALE AUMIA ASHINDWA KUENDELEA NA MECHI
Licha ya ushindi huo taarifa mbaya kwa Simba ni kuona kiungo mshambuliaji wao mpya, Joshua Mutale akishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 31 baada ya kupata maumivu ya mguu ambapo mpaka sasa bado taarifa rasmi haijatolewa kuhusu ukubwa wa jeraha lake.
VIKOSI VYA MCHEZO HUO
SIMBA
Camara, Kapombe (Kijili 71′), Zimbwe Jr, Che Malone, Hamza, Mzamiru (Okajepha 71′), Balua, Fernandes, Mukwala (Mashaka 57′), Ahoua (Kibu 57′), Mutale (Awesu 31′)
TABORA UNITED
Mandanda, Maulid, Chuku, Pemba, Bikoko, Munganga, William, Yusuph (Seseme 78′), Mhesa, Jamal, Kiberege (Moses 81′)
KOCHA SIMBA ANAUTAKA UBINGWA

Uongozi wa Simba mara baada ya mchezo huo wameweka wazi kuwa safari ndiyo imeanza na wamejipanga kuhakikisha wanashinda michezo iliyo mbele yao na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda ubingwa msimu huu.
Akizungumzia kikosi chake kocha mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu Davids amesema: “Kikosi chetu kimepata wiki sita za mazoezi pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki pamoja zile za Ngao ya Jamii, hivyo kipo tayari kwa Ligi Kuu.
“Malengo yetu kuelekea mchezo huu dhidi ya Tabora ilikuwa kuhakikisha tunaanza vizuri ligi kwa kuanza na ushindi na tunashukuru kufanikisha hilo. Timu ipo tayari kwa Ligi Kuu, kikosi chetu kipo kwenye umbo bora la kiushindani na mawasiliano ndani ya uwanjani yameendelea kuimarika, Mchezo wa leo tuliupa umuhimu mkubwa na malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mechi ili kujiweka sawa kwenye harakati za kupigania taji la ubingwa,” amesema Kocha Fadlu.
Naye mlinda mlango wa timu hiyo, Hussein Abel amesema wao kama wachezaji wamejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi zote zilizo mbele yao na wapo tayari kuwapa furaha Wanasimba.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari, tunaamini ligi ni ngumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunapambana kushinda kila mchezo,” amesema Abel.
REKODI ZINASEMAJE?
Kabla ya mchezo wa ushindi wa mabao 3-0 leo, mchezo wa mwisho walipokutana msimu uliopita, mchezo ukipigwa Uwanja wa Azam Complex, Mei 6, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0. Katika mchezo huo mabao yao yalifungwa na Sadio Kanoute na Edwin Balua.
STRAIKA MPYA BADO KIDOGO TU
Akimzungumzia straika wake mpya, Lionel Ateba kocha, Fadlu amewelka wazi kuwa nyota huyo alikuwa chini ya uangalizi maalum wa programu za utimamu wa mwili kutokana na kuchelewa kujiunga na wenzake na atakapokuwa tayari basi Wanasimba wataanza kuona balaa lake uwanjani.
“Leonel Ateba amejiunga nasi siku chache zilizopita ambapo alifanyiwa vipimo vya afya na amefanya mazoezi kjidogo na wenzake kwahiyo inategemea na utimamu wake wa mwili juu ya lini ataanza kutumika rasmi,” amesema Fadlu.

