MABINGWA Yanga wenye mataji 30 kabatini ya ligi wakiwa na kibarua cha kutetea taji lao la ligi msimu mpya wa 2024/25 chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi wameanza msimu kwa rekodi ya kuwapa tabu wapinzani wao wote waliokutana ndani ya uwanja kwenye mechi mbili za Ngao ya Jamii.

Ipo wazi kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ilitwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2023/24 ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya kwanza na pointi zake 80 kibindoni baada ya kucheza jumla ya mechi 30.
MABINGWA MWENDO WAO NGAO YA JAMII
Kwenye hatua ya Ngao ya Jamii ikiwa ni mechi mbili zenye dakika 180 Yanga ilipata ushindi kwa timu zilizomaliza nafasi tatu za juu kwenye ligi msimu uliopita uliokuwa na ushindani mkubwa.
Yanga ilianza na hatua ya nusu fainali hapa ilimenyana na Simba Agosti 8 2024 Uwanja wa Mkapa. Kocha Mkuuwa Simba Fadlu Davids alikaa benchi na mwisho ilikuwa Simba 0-1 Yanga bao pekee la ushindi likifungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 44 kipindi cha kwanza kazi iliisha.

Kwa upande wa matajiri wa Dar, Azam FC inayonolewa na Yusuph Dabo hawa walikutana kwenye hatua ya fainali ya Ngao ya Jamii mwisho ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 4-1 Azam FC ilikuwa Agosti 11.
Ikumbukwe kwamba timu zote mbili Azam FC na Simba ziligongana kwenye alama ambazo walimaliza nazo kwenye ligi, Azam FC ikiwa nafasi ya pili na Simba nafasi ya tatu zote zilikuwa na pointi 69 tofauti mabao ya kufunga na kufungwa.
MABINGWA MASHINE ZAO HIZI HAPA
MAXI

Maxi Nzengeli kiungo wa kazi ndani ya Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali alipeleka maumivu kwa Simba dakika ya 44 akitumia pasi ya Prince Dube Uwanja wa Mkapa.
Kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Maxi alifunga bao pekee la ushindi ambalo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo.
AZIZ KI
Mwenye tuzo ya ufungaji bora ndani ya ligi msimu wa 2023/24 Aziz Ki baada ya kufunga mabao 21 hajaanza kwa kusuasua. Katika mchezo wa fainali ilikuwa mashine ya kazi kwa kufunga bao moja dhidi ya Azam FC.
MUDA
Kiungo wa kazi Mudathir Yaya kwenye hatua ya fainali dhidi ya Azam FC alitoa pasi maelekezo iliyokutana na Prince Dube ambaye alimaliza kwa kufunga mbele ya Azam FC ilikuwa ni dakikaya 14 na kuweka usawa bao ambalo lilifungwa na Feisal Salum wa Azam FC kwenye mchezo huo.
DUBE
Prince Dube, muuaji anayetabasamu anaingia kwenye orodha ya mashine za kazi kwa kuwa kwenye mabao matano ambayo Yanga imefunga katika Ngao ya Jamii yeye katupia moja ilikuwa dhidi ya Azam FC.
BOKA
Anaitwa Chadrack Boka beki wa kupanda na kushuka ana spidi akiwa uwanjani na uwezo wake wa kupandisha mashambulizi ni moja ya mashine ambazo zinatumiwa na Gamondi kusaka ushindi uwanjani. Azam FC wanakumbuka kazi yake kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii alipofunga bao moja katika mabao manne ambayo Yanga ilishinda.
MZIZE
Nyota Clement Mzize mshambuliaji mzawa anayepewa nafasi ya kufanya vizuri ndani ya Yanga akitokea benchi alifanya kazi yake aipendayo kwa kufunga bao moja dakika ya 90 likiwa ni bao la jioni kabisa
MABINGWA NA UKUTA
Ukuta wa Yanga unaoongozwa na Dickson Job, Bacca umekuwa imara ndani ya msimu mpya wa 2024/25 ambapo kwenye mbili ilizoshuka uwanjani ni bao moja pekee iliruhusu ilikuwa katika hatua ya fainali dhidi ya Azam FC.
Job amekuwa akifanya kazi kubwa kushirikiana na wachezaji wengine kuendelea kuiweka ngome ya mabingwa hao salama kwenye mechi kubwa ambazo wanacheza kwa kuwa Mzizima Dabi iliyokuwa fainali waliruhusu bao moja na kwenye nusu fainali dhidi ya Simba Kariakoo Dabi hawakuruhusu bao.
MAISHA MAPYA YA DUBE

Prince Dube amebainisha kuwa ni furaha kwake kuwa ndani ya Yanga hivyo anaamini kwamba watafanya kazi kubwa kufikia malengo kwenye mechi ambazo wanacheza kitaifa na kimataifa.
“Ni furaha kuona kwamba tunapata ushindi hili ni jambo la timu kwani tumekuwa tukishirikiana nina amini kwamba mazuri yanakuja kwenye mechi zetu ambazo tutakuwa tunacheza.”
Gamondi ameweka wazi kuwa utulivu wa wachezaji pamoja na kutumia nafasi ambazo wanazipata unawapa nguvu ya kufanya vizuri kwenye mechi zao na walianza na Ngao ya Jamii.
“Tumeanza na Ngao ya Jamii hii ni kubwa na pongezi kwa wachezaji kwani wamekuwa na utulivu mkubwa kwenye mechi zetu hata pale ambapo tulianza kufungwa bado walileta ushindi kwa kushirikiana.’

