
BOSI mpya wa Simba ambaye atakuwa ni Mtendaji Mkuu, (CEO) ametangazwa Julai 26 2024 anaitwa Uwayezu Francois Regis yeye ni raia wa Rwanda ambapo ataanza majukumu yake kwa asilimia 100 Agosti Mosi, 2024.
Taarifa iliyotolewa na Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohamed Dewji, (Mo) imeeleza kuwa wameridhia ombi la Imani Kajula kutoendelea na nafasi hiyo kama ambavyo aliomba.
Ikumbukwe kwamba Kajula aliomba kutoongeza mkataba ndani ya Simba muda wake utakapoisha jambo ambalo lilipitishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Simba na kubainisha kwamba watamtafuta CEO mpya.
Rasmi wamemtangaza CEO mpya atakayechukua mikoba yake muda wake utakapogota mwisho Julai 31 2024 zikiwa zimebaki siku tano pekee kukamilika kuanzia leo Julai 26 na Agosti 8 2024 Simba itamenyana na Yanga kwenye Kariakoo Dabi mchezo wa Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali.
Uwayezu alikuwa Makamu Mwenyekiti wa APR ya Rwanda na tayari ameagwa na viongozi wa klabu hiyo hivyo yupo huru kuanza majukumu yake mapya na timu hiyo ambayo itashiriki Kombe la Shirikisho msimu wa 2024/25.
Rekodi zinaonyesha kwamba Kajula alitambulishwa rasmi Januari 26 2023 kuwa CEO wa Simba ambayo kwa sasa ipo kwenye maandalizi kuelekea Simba Day inayotarajiwa kufanyika Agosti 3 2024 Uwanja wa Mkapa.
Kauli mbio inayotumika kwa sasa na Simba ni Ubaya Ubwela. Siku hiyo inatarajiwa kuwa rasmi kuwatambulisha wachezaji wa Simba waliokuwa na kikosi msimu wa 2023/24 na wale ambao ni wapya bila kusahau benchi la ufundi.
Ipo wazi kwamba Kajula alichukua mikoba ya Barbra Gonzalez aliyebwaga manyanga Desemba 10 2022 kwa kubainisha kuwa anahitaji kuwapa nafasi wengine katika uongozi. Julai 15 2024 taarifa ilitolewa na uongozi wa Simba kwamba wameridhia ombi la Kajula kuomba kutoongeza mkataba.
BOSI KWENYE KAZI
Bosi huyo wa Simba Kajula kuelekea kwenye maandalizi ya Simba Day amekuwa mstari wa mbele kutimiza majukumu yake ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa uzi mpya wa Simba utakaotumika msimu wa 2024/25.
Uzi huo ulizinduliwa kwenye hifadhi ya Mikumi ilikuwa ni Julai 24 ambapo mashabiki wengi kutoka pande mbalimbali za Tanzania walishuhudia historia mpya ikiandikwa kwa mara nyingine tena.
BOSI NA GUMZO LA KIBEGI

Ipo wazi kwamba uzi wa msimu wa 2023/24 ulizinduliwa juu ya Mlima Kilimanjaro na kibegi cha jezi ya Simba kilipata umaarufu mkubwa. Katika kilele cha Simba Day msanii Ali Kiba, King Kiba alitumbuiza na kwa mara nyingine tena anatarajiwa kutumbuiza Agosti 3 2024.
Kiba wimbo wake wa Unyama ni Mwingi uliingia kwenye orodha ya nyimbo zilizosikilizwa sana katika mitandao ya kijamii na kuwa namba moja kwenye Trendig kwa wakati huo katika mtandao maarufu wa You Tube.
SEMAJI LATEMA CHECHE

Wakati maandalizi yakizidi kupamba moto kuelekea Simba Day, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba maarufu kama semaji la CAF ametema cheche kuelekea Simba Day kwa kubainisha kuwa watafanya vurugu vibaya mno.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa kutakuwa na utofauti mkubwa kwenye tamasha hilo hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa kushuhudia burudani kubwa.
“Hilo tamasha la Simba Day litakuwa kubwa lenye mvuto vibaya mno kwa kuwa tumefanya maandalizi mazuri na unajua kwamba hatuna jambo dogo linapofika suala la maandalizi mazuri kwenye matamasha yetu.
“Tunaomba Mungu tufike salama Simba Day ni muda wa kuwa kwenye furaha kwani muda unakuja. Kila mmoja anapenda kuona tunapata matokeo mazuri hilo lipo wazi na inawezekana kwa kuwa muda upo na wachezaji wapo tayari kuona tunapata matokeo mazuri.”
KIBU D SAKATA LAKE BADO BICHI

Wakati Simba ikiwa kwenye mchakato wa kuelekea Simba Day, Agosti 3 bado sakata la kiungo mshambuliaji Kibu Dennis halijapata majibu yake kwa kuwa mchezaji bado hajaripoti kambini.
Taarifa ambayo ilitolewa na Simba Julai 23 ilieleza kuwa kiungo huyo Kibu bado hajaripoti kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2024/25.
Ilieleza kuwa kiungo huyo aliongeza mkataba wa miaka miwili ambayo itamfanya adumu hapo mpaka Juni 2026 lakini hajaripoti kambini nchini Misri. Kutokana na suala hilo uongozi ulibainisha kuwa utamchukulia hatua za kinidhamu Kibu na umma utapewa taarifa.

