
UNYAMANI kivumbi kinaendelea Simba ambapo kuna wachezaji watakutana na Thank You licha ya kuwa na mikataba na timu hiyo hivyo hawatakuwa ndani ya kikosi hicho msimu wa 2024/25.
Tayari benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wamewasili Misri kwa ajili ya maandalizi ya kambi huku baadhi ya wachezaji wakiwa hawajajiunga na timu hiyo. Miongoni mwao ni kipa Aishi Manula ambaye mkataba wake na Simba unagota mwisho 2025.
Ipo wazi kwamba ni Yanga walitwaa ubingwa wa ligi. Wapo waliokuwa wakichana mikeka na wapo ambao walikula kirahisi hata wewe unaweza jisajili ukawa na nafasi ya kushinda kwa kutabiri na kuweka mkeka wako na Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa. Tembelea www.sportpesa.co.tz
Ahmed Ally Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa kipa Aishi Manula bado ana mkataba na Simba licha ya kutokuwa kwenye msafara huo wa kwanza hivyo taarifa rasmi itatolewa.
Julai 8 2024 msafara wa Simba ulikwea pipa kuelekea Misri kwa kambi ya maandalizi ya msimu wa 2024/25 kipa Manula hakuwepo katika msafara huo.
Ally amesema: “Aishi Manula ana mkataba na Simba hivyo taarifa yake kuhusu kinachoendelea itatolewa rasmi na uongozi mashabiki wasiwe na presha kila kitu kipo sawa.”
ONANA KWENYE ORODHA

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Willy Onana mwenye zali la kufungua na kufunga ukurasa wa mabao chini ya Kocha Mkuu Juma Mgunda anatajwa kuwa kwenye orodha ya wale ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi kwa msimu wa 2024/25.
Wakati Simba ikikwea pipa kuelekea Misri Julai 8 mwamba Onana rasta hakuwa kwenye orodha ya wachezaji waliokuwa kwenye msafara huo pia.
Ikumbukwe kwamba Simba iligotea nafasi ya tatu msimu wa 2023/24 na pointi zake 69. Mechi za mzunguko wa pili ni Mgunda alikuwa kwenye benchi kukamilisha kazi na malengo makubwa ilikuwa ni kugotea nafasi ya pili ngoma ilikuwa nzito.
Ni mikoba ya Abdelhak Benchikha aliyebwaga manyanga huku mchezo wake wa mwisho kukaa benchi alishuhudia ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Yanga 2-1 Simba. Kwa sasa timu hiyo imemtambulisha kocha mpya ambaye ni Fadlu Davids.
Mgunda alikaa benchi kwenye mechi tisa akiambulia ushindi kwenye mechi 7 na sare mbili zote ilikuwa ugenini, Namungo 2-2 Simba ulikuwa mchezo wa kwanza kuongoza akishuhudia Willy Onana akifunga bao la kwanza akiwa benchi na sare ya pili ilikuwa Kagera Sugar 1-1 Simba ilikuwa sare yake ya pili, Uwanja wa Kaitaba.
Funga kazi ilikuwa ni Mei 28 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 2-0 JKT Tanzania huku mwamba Onana akifunga bao la pili kwenye mchezo huo ikiwa ni funga kazi mazima 2023/24.
Onana alifungua na alikuwa mchezaji wa mwisho kufunga bao ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023/24 uliogota mwisho. Kuna uwezekano kwamba nyota huyo mwenye uwezo wa kutumia mguu wa kulia hatakuwa ndani ya kikosi cha Simba.
Kuhusu hilo Ally amesema: “Kuna wachezaji wengine ambao hawapo kwenye msafara lakini wana mkataba ikiwa ni pamoja na Willy Onana taarifa zao zote zitatolewa hivi karibuni.
“Kikubwa tunatambua kwamba kuna wachezaji ambao wapo kwenye msafara na wengine watajiunga na timu moja kwa moja kambini hivyo muhimu kuendelea kuwa pamoja.”
KIUNGO MGUMU KANOUTE
Kiungo mkabaji raia wa Mali, Sadio Kanoute mkali wa mikato ya kimyakimya anaingia kwenye orodha ya nyota ambao nao huenda hawatakuwa kwenye kikosi cha Simba. Ipo wazi kwamba Kanoute kwenye eneo la ukabaji alikuwa chaguo namba moja ndani ya kikosi cha Simba.
Kwenye wachezaji ambao wamekwea pipa na kuweka kambi nchini Misri nyota huyo hayupo pia. Ilikuwa inaelezwa kuwa kiungo huyo alikuwa anahitaji kupata changamoto mpya ndani ya timu nyingine.
BABACAR SARRI
Ingizo jingine ambalo lilikuwa ndani ya Simba Sarri kiungo mkabaji naye anatajwa kuwa atakutana na Thank You licha ya kwamba bado mkataba wake haujagota mwisho.
Nyota huyo alikuwa anatajwa kuwa mbadala wa kiungo mkabaji Jonas Mkude ndani ya Simba lakini alikwama kuwa kwenye ubora wake kwenye mechi ambazo alipata nafasi ya kucheza.
Kuhusu Sarri, Ally amesema: “Sarri naye ana mkataba na Simba hivyo kutokuwa kwenye msafara huu kuelekea kambini Misri taarifa yake itatolewa.
PA JOBE KUKUTANA NACHO

Kiungo mshambuliaji Pa Jobe ambaye alikuwa anatajwa kuchukua mikoba ya Moses Phiri naye anaingia kwenye orodha ya nyota ambao watakutana na Thank You.
Nyota huyo hakuwa chaguo la kwanza ndani ya Simba na alikwama kuonyesha ubora wake kwenye mechi ambazo alipata nafasi ya kucheza.
Huenda mkataba wake ukasitishwa na mabosi wa Simba ili kuwapa nafasi wachezaji wengine ambao wamesaini kandarasi kuitumikia timu hiyo kuelekea msimu wa 2024/25.

