
VITA ya usajili kwa timu zilizo chini ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF), unazidi kupamba moto ambapo kila timu inapambana kuhakiksha inaandaa kikosi bora kwa ajili ya msimu mpya wa ligi 2024/25.
Licha ya kuwepo kwa sajili nyingi ambazo zinaendelea kufanyika, lakini mpaka sasa ni wazi kuwa usajili wa nyota wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chota Chama kutoka ndani ya Simba na kujiunga na Yanga wanaodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa ndio unatajwa kuwa usajili ambao umetikisa zaidi.
Yanga Julai Mosi mwaka huu, walimtangaza Chama kuwa mchezaji wao mpya kwa ajili ya msimu ujao wa 2024/25 ambapo inaelezwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja ndani ya timu ya Wananchi.
Swali kubwa baada ya utambulisho wa Chama lilikuwa je, ni lini nyota huyo atawaaga rasmi Simba na ni lini Simba watatoa ‘THANK YOU’ ya Chama, ambapo hatimaye leo Chama amewaaga rasmi Simba na kuwashukuru kwa mafanikio yote waliyoyapata pamoja na kuwatakia kila la kheri waajiri wake hao wa zamani, kwa sasa inasubiriwa kuona ikiwa Simba watatoa ‘Thank You’
HIZI HAPA MASHINE MPYA 3 ZA SIMBA
- Ahoua Jean Charles

Simba wametangaza kufanikiwa kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji, Ahoua Jean Charles raia wa Ivory Coast kwa mkataba wa miaka miwili.
Ahoua mwenye umri wa miaka 22 wamemsajili kutoka klabu ya Stella Club d’Adjamé ya nchini kwao Ivory Coast na ndiye anatajwa kuwa mrithi wa Chama kutokana na uwezo mkubwa alionao
Katika msimu wa 2023/24 Ahoua ameibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini Ivory Coast (MVP), na klabu yake huku akifunga mabao 12 na kutoa ‘assist’ tisa. Mchango wake wa mabao ni kama ilivyo kwa Chama ambaye pia amekuwa na uwezo mkubwa kufunga na kuasisti mabao.
Taarifa ya Simba imeeleza kuwa, Ahoua anasifika kwa kufunga mabao kutoka umbali mrefu, kuchezesha timu pamoja kutengeneza nafasi kwa wenzie.
Simba pia wameeleza kuwa wanategemea mambo makubwa kutoka kwa Ahoua kwa kushirikiana na nyota wengine waliowasajili, pamoja na wale waliokuwepo kikosini.
Kuelekea msimu wa Ligi 2024/25 Simba wamekuja na utaratibu mpya kwenye usajili wa kuingiza wachezaji bora wenye uwezo na umri mdogo ili kujenga timu imara ya muda mrefu.
Ahoua anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa baada ya Lameck Lawi, Joshua Mutale na Steven Mukwala.
- Steven Mukwala

Mshambuliaji, Steven Mukwala raia wa Uganda amejiunga na Simba baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kutoka Asante Kotoko ya Ghana.
Mukwala mwenye umri wa miaka 24 ni mshambuliaji kinara mwenye uwezo wa kufunga na Simba wameeleza kuwa wanategemea atakuwa msaada mkubwa kwa timu yao.
Msimu uliopita staa huyo amefunga mabao 14 na kuisaidia kupatikana kwa mengine mawili katika michezo 28 katika ligi kuu ya Ghana.
Mukwala ana urefu wa futi 5.9 na ana uwezo wa kufunga magoli ya aina yeyote lakini pia ni mzuri kwenye mipira ya juu na mipira ya krosi na pia hivyo anatarajiwa atakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo.
Moja ya eneo ambalo lilikuwa na mapungufu msimu uliopita ni katika safu ya ushambuliaji na ujio wa Mukwala utaongeza uimara wa timu akisaidiana na Fredy Michael.
Mukwala amewahi kuzitumikia timu za Vipers FC, Maroons FC zote za Uganda kabla ya kutimkia Asante Kotoko ya Ghana.
Simba wameeleza kuwa wanaendelea kufanya usajili kwa umakini mkubwa na kuimarisha kikosi chao katika idara zote ili msimu ukianza wawe kwenye ubora mkubwa.
- Joshua Mutale

Kiungo mshambuliaji, Joshua Mutale raia wa Zambia amejiunga na Simba baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Power Dynamos ya Nchini kwao.
Mutale mwenye miaka 22 anamudu kucheza nafasi nyingi Uwanjani tena kwa ufanisi wa hali ya juu.
Joshua anaweza kumudu nafasi ya winga ya kulia, kushoto na wakati mwingine anacheza nyuma ya mshambuliaji yaani namba 10.
Akiwa Power Dynamos msimu uliopita, Mutale amefunga mabao manane na kuisaidia kupatikana kwa mengine katika michezo 26.
Uwezo wake wa kumudu kucheza nafasi nyingi Uwanjani pamoja na umri ni miongoni mwa vigezo vilivyowavutia kumsajili mchezaji huyo, ikiwa ni mkakati maalumu wa kuboresha kikosi chao kwa kusajili damu changa na zenye ubora.

