
HATIMAYE hatua ya makundi ya mashindano ya EURO 2024 yanayoendelea huko nchini Ujerumani, imetamatika na kuingia hatua ya 16 huku rekodi kadhaa zikivunjwa na rekodi mpya kuandikwa .
Makala hii inakujia na rekodi kadhaa kali ambazo zimefanikiwa kuandikwa katika hatua hiyo ya makundi kama ifuatavyo.
Unaweza kujishindia fedha kwa kubashiri mechi mbalimbali za Euro kupitia Kampuni ya michezo ya SportPesa.
- Mchezaji mdogo zaidi: Lamine Yamal (Hispania) – miaka 16 siku 338

Nyota wa Uhispania, Lamine Yamal amefanikiwa kuweka historia ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kushiriki katika fainali za EURO hii ni baada ya kuanza kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Croatia kwenye mchezo wa kundi B la mashindano hayo.
Rekodi ya awali ilikuwa ikishikiliwa na, Kacper Kozłowski wa Poland, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 na siku 246 katika mchezo wa sare ya bao 1-1 dhidi ya Uhispania katika EURO 2020.
Akimzungumzia mchezaji huyo, kocha wa Hispania, Luis de la Fuente amesema: “Anaendelea kuvunja rekodi. Anahitaji kuendelea kukua na nina hakika siku moja atakuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi.”
- Kocha mdogo zaidi: Julian Nagelsmann (Germany) — miaka 36 na siku 327

Julian Nagelsmann atakuwa alifurahi sana kwenye mechi ya ufunguzi ya fainali hizi za EURO 2024, sio tu kwamba timu yake ya Ujerumani iliifunga Scotland 5-1 katika ardhi ya nyumbani mjini Munich, lakini kocha huyo wa zamani wa Leipzig na Bayern aliweka rekodi binafsi kwa kuwa kocha mdogo zaidi kuongoza timu ya taifa katika mashindano haya akiwa na umri wa miaka 36 siku 327.
Nagelsmann amemshinda kocha wa zamani wa Slovenia, Srečko Katanec kwa siku sita tu. Akizungumzia kikosi chake, Nagelsmann amesema: “Timu inanipa nguvu nyingi, ni furaha sana kuwa na kundi hili la wachezaji.”
- Nahodha mdogo zaidi: Dominik Szoboszlai (Hungary) – miaka 23 siku 243
Staa huyu ameonyesha wazi kuwa huna haja ya umri mkubwa kuwa kiongozi mzuri, Dominik Szoboszlai nahodha wa timu yake ya Hungary katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Uswizi aliiongoza timu hiyo akiwa na umri wa miaka 23 siku 243.
Kwa kufanya hivyo, alivunja rekodi ya nahodha wa zamani wa Italia, Giuseppe Bergomi, ya miaka 24 siku 171, wakati alipoiongoza timu hiyo dhidi ya Ujerumani mnamo 1988.
Akizungumzia majuku hayo makubwa, Szoboszlai amesema: “Nadhani nimebadilika zaidi kama mtu kuliko kama mchezaji. Katika nafasi yangu napaswa kuwa kioo na kuhakikisha natetea wenzangu”
- Mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga bao: Luka Modrić (Croatia) – miaka 38 siku 289

Katika moja ya mabao ya kukumbukwa zaidi ya mashindano hayo hadi sasa ni lile la nahodha wa Croatia, Luka Modrić ambalo alifunga dhidi ya Italia muda mfupi baada ya kukosa penalti.
Ingawa Azzurri waliishia kusawazisha bao hilo haimkuzuia, Modrić kuvunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Austria, Ivica Vastić aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo kwa umri wa miaka 38 siku 289.
- Mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi: Pepe (Portugal) – miaka 41 siku 117
Beki mkongwe wa Ureno, Pepe naye amejiandikia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika fainali za EURO aple alipohusika katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Czechia katika Kundi F.
Pepe aliipiku rekodi ya kipa wa Hungary, Gábor Király, ambaye alikuwa na umri wa miaka 40 siku 86 wakati alipokabiliana na Ubelgiji katika raundi ya 16 katika EURO 2016.
- Mchezaji aliyecheza Kampeni nyingi za mashindano hayo: Cristiano Ronaldo (Ureno) – 6

Modrić wa Croatia aliungana na, Cristiano Ronaldo na baadaye Pepe katika kuwa mmoja wa wachezaji pekee waliojitokeza katika mfululizo wa mashindano matano ya mwisho ya EURO wakati alipocheza mchezo wa kipigo cha mabao 3-0 kwa Hispania huko Berlin, lakini siku tatu baadaye Ronaldo alimzidi, akichukua uwanja kwa EURO sita tofauti, tangu alipocheza kwa mara ya kwanza mashindano hayo mnamo 2004.
Ronaldo pia ameongeza rekodi yake ya kucheza michezo mingi katika mashindano hayo ambayo jumla yake ni michezo 28 japo bado hajaongeza rekodi yake ya mabao 14 katika mashindano.
“Ninajivunia kuwa mchezaji wa kwanza kucheza katika mashindano sita ya EURO. Nimefurahi sana kwa hilo, kwani inaonyesha urefu wa maisha yangu ya soka.”

