SIMBA YAMSHUSHA MUTALE KIMYAKIMYA, KUSAINI MKATABA WA MIAKA 3

ByJoel Thomas

June 26, 2024
------------------------------------------------n------------------------------------------------n------------------------------------------------n
SIMBA
Joshua Mutale

UONGOZI wa Simba jana Jumanne ulimshusha rasmi nyota wa kimataifa wa Zambia, Joshua Mutale kwa ajili ya kukamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo ambapo inaelezwa atasaini mkataba wa miaka mitatu.

Mutale ambaye msimu uliopita akiwa na kikosi cha Power Dynamos ya Zambia alifanikiwa kuhusika kwenye mabao zaidi ya 20 anakuwa mchezaji wa pili kumalizana na Simba baada ya hapo awali mabosi wa timu hiyo kumtambulisha rasmi mlinzi wa kimataifa wa Tanzania, Lameck Lawi aliyejiunga na Simba kutokea Coastal Union.

Mabosi wa Simba wanaendelea na maboresho ya kikosi chao ambapo mpaka sasa panga kubwa linaendelea kupitishwa, huku pia baadhi ya mastaa wakiongezewa mikataba.

WALIOONGEZEWA MIKATABA SIMBA MPAKA SASA

  1. Kibu Denis
SIMBA
Kibu Denis

Kiungo mshambuliaji, Kibu Denis anatarajiwa kuendelea kusalia klabuni hapo mara baada ya kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya wa miaka miwili baada ya hapo awali kuhusishwa kuhamia Yanga wanaodhaminiwa na Kampuni ya michezo ya  SportPesa.

Taarifa ya Simba kumhusu Kibu imemuelezea kama mmoja wa wachezaji anayejitoa muda wote na mpambanaji uwanjani na anastahili kuwepo kwenye mipango ya timu kuelekea msimu ujao wa Ligi 2024/25.

Uongozi wa timu hiyo umeweka wazi kuwa mipango yao ni kuhakikisha wanasuka kikosi imara, kwa ajili ya mashindano mbalimbali na Kibu ni sehemu ya mpango wa timu yao.

Simba wanamuelezea Kibu kuwa ni mchezaji mzawa ambaye amejipambanua mwenyewe kutokana na jitihada kubwa anazofanya akiwa uwanjani, kwa ajili ya kuisaidia timu na hilo ndilo linamfanya kuwa kipenzi cha Wanasimba.

Uongozi wa timu hiyo umetamba kuwa umepanga kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi ili kuhakikisha wanarejesha makali ya kikosi chao na kuwa timu imara yenye kupigania mataji.

  1. Israel Mwenda

Mlinzi, Israel Patrick Mwenda amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu kuendelea kusalia katika kikosi cha Simba.

Israel ambaye anamudu kucheza kama mlinzi wa kulia na kushoto alijiunga na timu hiyo Julai, mwaka 2021 akitokea KMC.

Taarifa ya Simba kuhusu Israel Mwenda inamuelezea kama miongoni mwa wachezaji ambao wanaamini katika uwezo wake na katika kujenga timu mpya kuelekea msimu ujao wa 2024/25.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa ni mchezaji kijana ambaye bado ana nguvu ya kuitumikia timu na uwezo alionao wana matarajio makubwa juu yake kuwa ataendelea kusalia kwa miaka mitatu mingine.

  1. Mzamiru Yassin

Kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kusalia katika kikosi cha Simba.

Mkataba wa Mzamiru ulimalizika mwishoni mwa msimu huu na mapendekezo ya kiufundi yamependekeza mchezaji huyo kubaki kutokana na mchango wake, hivyo uongozi wa timu hiyo umemuongezea miaka mingine miwili ya kuendelea kusalia.

Mzamiru ni kati ya wachezaji waandamizi waliodumu ndani ya Simba kwa muda mrefu zaidi, akihudumu kwa miaka nane kwa kiwango bora na sifa yake kubwa ikiwa kujituma na usikivu.

WALIOPEWA ‘THANK YOU’ MPAKA SASA

  1. Henock Inonga
SIMBA
Henock Inonga

Simba imefikia makubaliano ya kumuuza aliyekuwa mlinzi wa kati, Henock Inonga Baka kwenda FA Rabat inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco.

Inonga ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alikuwa amebakisha Mkataba wa mwaka mmoja uliokuwa umalizike mwaka 2025, lakini kutokana na kile uongozi wa Simba ulichokieleza kuwa ni klabu yao kujali maslahi ya wachezaji, tumemruhusu beki huyo kuondoka kwenda kujiunga na FA Rabat.

Inonga alijiunga na kikosi hicho mwaka 2021 akitokea  DC Motema Pembe ya Congo. Katika kipindi cha miaka mitatu aliyodumu ndani ya kikosi hicho, Inonga amekuwa muhimili wa timu na makocha wote waliopita wamekuwa wakimpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Mwaka 2022, Inonga alichaguliwa mlinzi bora wa Ligi kuu ya Tanzania baada ya kuonesha kiwango bora katika msimu huo. Uongozi umemshukuru, Inonga kwa utumishi wake uliotukuka katika kipindi chote walichokuwanae na pia kumtakia kheri katika maisha yake mapya ya soka nje ya Simba.

  1. Kennedy Juma

Baada ya miaka mitano aliyodumu ndani ya timu hiyo mlinzi wa kati, Kennedy Wilson Juma ametangazwa kuwa hatokuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kuelekea msimu mpya baada ya mkataba wake kumalizika.

Kennedy alijiunga na Wanamsimbazi Julai 2019, akitokea Singida United. Taarifa ya Simba imemuelezea, Kennedy kama mmoja ya wachezaji watulivu na wasikivu ndani ya kikosi chao na amekuwa akifanya kila anachotakiwa ndani ya muda unaohitajika.

Taarifa hiyo iliendelea kusema pamoja na ubora na uwezo alionao, Kennedy lakini hayupo kwenye mipango ya kusuka kikosi imara kuelekea msimu ujao wa mashindano hivyo hawakuongeza nae mkataba.

Uongozi wa klabu unamshukuru Kennedy kwa utumishi wake uliotukuka na kumtakia kheri katika maisha yake mapya ya soka nje ya Simba.

Wengine walioachwa ni, Saido Ntibazonkiza, John Bocco, Luis Miquissone na Shaban Chilunda.

Share this:

ByJoel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.