
Uongozi wa Simba kupitia kwa meneja wao wa habari na mawasiliano, Ahmed Ally wametangaza rasmi siku ya Simba ‘Simba day’ ambayo kwa kawaida huwa siku yao rasmi kwa ajili ya kutambulisha mastaa wao wapya kwa msimu husika.
Uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa kuelekea msimu wa 2024/25 Simba day (tukio ambalo limewahi kudhaminiwa na Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa) inatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 3, mwaka huu.
Uongozi wa timu hiyo umeweka wazi kuwa kwa kawaida Simba Day hufanyika siku ya Agosti 8, ya kila mwaka lakini kutokana na kuwepo kwa michuano ya Ngao ya Jamii siku hiyo wameamua kuirudisha nyuma.
Ahmed amesema kabla ya kilele chake kutatanguliwa na wiki ya Simba ambayo inatarajiwa kuanza Julai 26, mwaka huu ambayo itakuwa na matukio mbalimbali.
Ndani ya wiki hiyo pia kunatarajiwa kuwa na matukio mbalimbali ya kijamii kama kuchangia damu, kuchangia wenye mahitaji maalum n.k.
Ahmed amesema katika siku hiyo ya kilele kunatarajiwa kuwa na matukio makubwa ya burudani kabla ya kuanza mchezo wenyewe, ambao wametamba kuutumia kutambulisha kikosi chao kuelekea msimu wa Ligi 2024/25.
ALICHOSEMA AHMED

“Sasa ni rasmi kilele cha Simba Day kinatarajiwa kuwa Agosti 3, mwaka huu na haitawezekana kufanyika Agosti 8, kama ilivyozoeleka kutokana na kalenda ya TFF ambayo siku hiyo tutaanza michuano ya Ngao ya Jamii.”
“Kabla ya siku ya kilele kutatanguliwa na wiki ya Simba ambayo itakuwa na matukio mbalimbali ya kijamii kama ambavyo tunafanya kila mwaka.” amesema Ahmed.
BAADHI YA MASTAA AMBAO WAMEMALIZANA NA SIMBA NI;
Lameck Lawi na Joshua Mutale
Uongozi wa timu hiyo Jumanne iliyopita inatajwa kuwa ilimshusha rasmi nyota wa kimataifa wa Zambia, Joshua Mutale kwa ajili ya kukamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo ambapo inaelezwa anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitatu.
Mutale ambaye msimu uliopita akiwa na kikosi cha Power Dynamos ya Zambia alifanikiwa kuhusika kwenye mabao zaidi ya 20, anatajwa kuwa kuwa mchezaji wa pili kumalizana na Simba baada ya hapo awali mabosi wa timu hiyo kumtambulisha rasmi mlinzi wa kimataifa wa Tanzania, Lameck Lawi aliyejiunga na Simba kutokea Coastal Union.
Mabosi wa Simba wanaendelea na maboresho ya kikosi chao ambapo mpaka sasa panga kubwa linaendelea kupitishwa, huku pia baadhi ya mastaa wakiongezewa mikataba.
WALIOLAMBA MIKATABA SIMBA MPAKA SASA
Kibu Denis
Kiungo mshambuliaji, Kibu Denis anatarajiwa kuendelea kusalia klabuni hapo mara baada ya kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya wa miaka miwili baada ya hapo awali kuhusishwa kuhamia Yanga wanaodhaminiwa na Kampuni ya michezo ya SportPesa.
Taarifa kumhusu Kibu imemuelezea kama mmoja wa wachezaji anayejitoa muda wote na mpambanaji uwanjani na anastahili kuwepo kwenye mipango ya timu kuelekea msimu ujao wa Ligi 2024/25.
Uongozi wa timu hiyo umeweka wazi kuwa mipango yao ni kuhakikisha wanasuka kikosi imara, kwa ajili ya mashindano mbalimbali na Kibu ni sehemu ya mpango wa timu yao.
Wamemuelezea Kibu kuwa ni mchezaji mzawa ambaye amejipambanua mwenyewe kutokana na jitihada kubwa anazofanya akiwa uwanjani, kwa ajili ya kuisaidia timu na hilo ndilo linamfanya kuwa kipenzi cha Wanasimba.
Uongozi wa timu hiyo umetamba kuwa umepanga kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi ili kuhakikisha wanarejesha makali ya kikosi chao na kuwa timu imara yenye kupigania mataji.
Israel Mwenda

Mlinzi, Israel Patrick Mwenda amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu.
Israel ambaye anamudu kucheza kama mlinzi wa kulia na kushoto alijiunga na timu hiyo Julai, mwaka 2021 akitokea KMC.
Taarifa ya kuhusu Israel Mwenda inamuelezea kama miongoni mwa wachezaji ambao wanaamini katika uwezo wake na katika kujenga timu mpya kuelekea msimu ujao wa 2024/25.
Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa ni mchezaji kijana ambaye bado ana nguvu ya kuitumikia timu na uwezo alionao wana matarajio makubwa juu yake kuwa ataendelea kusalia kwa miaka mitatu mingine.
Mzamiru Yassin
Kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kusalia katika kikosi hicho.
Mkataba wa Mzamiru ulimalizika mwishoni mwa msimu huu na mapendekezo ya kiufundi yamependekeza mchezaji huyo kubaki kutokana na mchango wake, hivyo uongozi wa timu hiyo umemuongezea miaka mingine miwili ya kuendelea kusalia.
Mzamiru ni kati ya wachezaji waandamizi waliodumu ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa muda mrefu zaidi, akihudumu kwa miaka nane kwa kiwango bora na sifa yake kubwa ikiwa kujituma na usikivu.

