KISHINDO kikubwa kinatarajiwa kuwa ndani ya Yanga kuelekea msimu mpya wa 2024/25 unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. Ipo wazi kwamba mabingwa hao wa ligi wanadhaminiwa na SportPesa.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amebainisha kwamba Julai Mosi 2024 wataanza kuwatangaza wale wachezaji ambao watakutana na Thank You. Pia watakaoongezewa mikataba na wapya.
Tayari dirisha la usajili limefunguliwa Juni 15 kwa timu kuingia sokoni kumalizana na wachezaji ambao wanawahitaji kwa kufuata utaratibu. Kuna orodha ya mastaa ambao wanatajwa kwamba watasepa ndani ya Yanga ikiwa ni pamoja na Metacha Mnata, Okra Magic, Joseph Guede huku Aziz Ki akitajwa kukubali kuongeza kandarasi mpya.

SEMAJI KUHUSU KUFUNGIWA NA FIFA
“Hatuna kesi inayotuhusu kwa sasa FIFA kwa kuwa tayari wachezaji wote ambao walikuwa wanatudai tumeshawalipa mapema. Juni 14 2024 tulikuwa tumekamilisha masuala ya malipo kwa wachezaji wote hivyo mpaka dirisha linafunguliwa Juni 15 tulikuwa hatuna deni.
Kamwe kupitia mahojiano na Azam TV alibainisha kuwa mashabiki wasiwe na hofu kwa kuwa kila kitu kipo sawa na watafanya usajili utakaokuwa na kishindo kikubwa bila kuongea sana zaidi vitendo vitafanya kazi.
“Mashabiki wasiwe na mashaka tunakwenda kufanya usajili wa kishindo. Julai Mosi 2024 tutaanza kuwatangaza wachezaji ambao tutaachana nao na wale ambao tutakuwa tumewaongezea mikataba.Wapo na wapya kwa kuwa tunahitaji kuwa na timu imara zaidi.”
WALIVYOBEBA TAJI LA LIGI

Chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi ilipofikisha pointi 71 ilijihakikishia kutwaa ubingwa kwa kuwa hakuna timu nyingine ambayo imefikisha pointi 71. Azam FC nafasi ya pili pointi 69, Simba nafasi ya tatu pointi 69 zote ilikuwa ni baada ya kucheza mechi 30.
Taji hilo linakuwa ni la 30 kwa Yanga huku ikiwapoteza watani zao wa jadi Simba misimu mitatu mfululizo wanapishana na taji la ligi. Ni Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga na Azam zitapeperusha bendera ya Tanzania huku Simba na Coastal Union kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya mechi 30 ni pointi 80 ilikusanya Yanga iliyotwaa taji la CRDB Federation kwa ushindi katika fainali dhidi ya Azam FC, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
YANGA WAMEKIMBIZA KINOMA

Ni namba moja kwa timu iliyoruhusu mabao machache ndani ya ligi. Kazi kubwa safu ya ulinzi chini ya nahodha Bakari Mwamnyeto, Dickosn Job ilifanywa kwa umakini wakishirikiana na wachezaji wengine.
Langoni mikono ya Djigui Diarra kipa namba moja wa Yanga ilikuwa ikifanya kazi. Mwisho wanatwaa taji la ligi wakiruhusu kufungwa mabao 14 ikiwa ni namba moja kwa timu iliyoruhusu mabao machache msimu wa 2023/24 baada ya kucheza mechi 30.
Mtibwa Sugar inayonolewa na Kocha Mkuu, Zuber Katwila ni namba moja kwa kuruhusu mabao mengi ambayo ni 54 baada ya kucheza jumla ya mechi 30.
Ngoma ilikuwa nzito kwenye upande wa kutupia ikiwa ni namba moja kwa makali. Mechi 30 mabao 71 yalikusanywa na safu ya ushambuliaji ya Yanga.
Taswira ilifunguka kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya KMC, baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Yanga 5-0 KMC mtupiaji wa bao la kwanza kwa Yanga akiwa ni beki Dickson Job.
MITAMBO YA MABAO
Kuna mitambo ya kutengeneza pasi imetulia ndani ya Yanga kuanzia viungo mpaka mabeki. Kwa upande wa viungo ni Aziz KI yeye katengeneza jumla ya pasi 8 akiwa ni namba moja kwenye eneo hilo.
Beki ni Yao Attohoula ambaye katengeneza jumla ya pasi 7 za mabao naye ni namba moja kwenye upande wa mabeki wenye pasi nyingi kiujumla ndani ya ligi.
Wapinzani walikuwa na kazi kubwa kwenye kuwazuia nyota hawa ambao ni mabingwa mara 30 ndani ya ligi.
WAKALI WA KUCHEKA NA NYAVU
Aziz KI mkali kwa kutumia mguu wa kushoto kafunga jumla ya mabao 17 kwenye ligi. Katumia mguu wa kulia kufunga mabao matatu na bao moja katupia kwa pigo la kichwa.
Maxi Nzengeli katupia mabao 11 na kutoa pasi mbili za mabao. Mudathir Yahya yeye katupia mabao 9 kwenye ligi. Mwamba huyu kafunga mabao sita Uwanja wa Azam Complex.
TATU ZA TATU BORA
Kazi kubwa kwenye msako wa pointi tatu ndani ya tatu bora ilikuwa kwa Yanga. Yanga dhidi ya Azam FC dakika 180 waligawana pointi tatutatu, mchezo wa mzunguko wa kwanza Yanga 3-2 Azam FC na ule wa mzunguko wa pili Azam FC 2-1 Yanga.
Ngoma ya Kariakoo Dabi ilikuwa Simba 1-5 Yanga, Yanga 2-1 Simba. Dakika 180 Yanga ilikomba pointi sita mazima za Simba na kuifanya ikombe pointi 9 ndani ya wababe waliopo tatu bora.
SARE ZA TOCHI
Yanga imeambulia sare kiduchu ambazo ni mbili ndani ya ligi ambazo ni dakika 180 na imepoteza mechi mbili pia kwa msimu wa 2023/24.
Mtibwa Sugar ambayo imeshuka daraja ni namba moja kwa kukusanya sare ambazo ni 19 kwenye mechi 30 ambazo ilicheza. Ni pointi 21 iligotea kukusanya timu hiyo inayotumia Uwanja wa Manungu kwa mechi za nyumbani.

