UTAKUMBUKWA 2023/24, MACHOZI, JASHO, KICHEKO

ByLunyamadizo Mlyuka

June 6, 2024
UTAKUMBUKWABocco
Ntiba
SAIDO Ntibanzokiza kiungo mshambuliaji wa Simba amefunga mabao 11 msimu wa 2023/24 kwenye ligi. Source:Simba.

UTAKUMBUKWA msimu wa 2023/24 kwa kuwatoa wachezaji jasho, machozi na kuwapa nyakati nyingine kicheko ndani ya dakika 90 kwenye msako wa pointi tatu kwa wanaume waliokuwa uwanjani na mwisho taji la ligi lipo mikononi mwa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa.

Timu 16 ndani ya ligi zilikuwa zinapambania kufikia malengo. Ipo wazi kuwa kila lenye mwanzo halikosi mwisho ilikuwa ni Mei 28 2024 msimu ukagota mwisho kwa dakika 2,700 kuyeyuka kwa kila timu kwenye mechi 30 ilizoshuka uwanjani.

Yapo mengi yaliongeza kasi ya ushindani ikiwa ni suala la tuzo ya ufungaji bora, kipa bora bado na msimu ulifungwa kwa fainali ya CRDB Federation Cup Juni 2 2024 ni Yanga tena waliibuka wababe mbele ya Azam FC, Uwanja wa New Amaan Complex kwa ushindi wa penalti 6-5 baada ya dakika 120 ngoma kuwa 0-0.

Kazi ilikuwa kubwa hapa tunakupitisha kwenye baadhi ya matukio yalikuwa na nguvu na ushindani mkubwa ndani ya uwanja namna hii:-

KIATU CHA UFUNGAJI BORA

AZIZ KI
Mfungaji bora msimu wa 2023/24, Aziz Ki mabao 21. Source: Yanga.

Nyota wawili walikuwa kwenye vita yao katika msako wa kiatu cha ufungaji bora ilikuwa ni Aziz Ki na Feisal Salum kila mmoja alikuwa kwenye mwendo wake kusaka kiatu cha ufungaji bora.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2022/23 ni Saido Ntibanzokiza wa Simba na Fiston Mayele wa Yanga walitwaa tuzo ya ufungaji bora kwa kila mmoja kutupia mabao 17. Rekodi hiyo imevunjwa na mfungaji bora msimu wa 2023/24.

Ni Aziz Ki wa Yanga kafunga msimu kwa mabao 21 kibindoni akimaliza kwa kufunga hat trick mbele ya Tanzania Prisons. Ni hat trick mbili anazo ya kwanza alifunga dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Mkapa mzunguko wa kwanza na ile ya pili ni dhidi ya Prisons, Uwanja wa Azam Complex.

Fei wa Azam FC ni namba mbili kwa wafungaji bora akiwa katupia mabao 19 na katika mabao hayo 19 alifunga hat trick moja ilikuwa Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Tabora United.

SIMBA NA AZAM FC VITA YAO

Ilikuwa kama utani lakini mwisho ikawa vita kweli, Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo dhidi ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda.

Azam FC mchezo wa mwisho walifunga kazi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Gold na Simba ilifunga kazi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania. Pointi wote ni 69 huku safu ya ushambuliaji ya Azam FC ikifunga mabao 61 ile ya Simba mabao 57.

Ukuta wa Azam FC uliruhusu mabao 21 na ule wa Simba ni mabao 25 uliruhusu hivyo kipande cha mabao ya kufunga na kufungwa kimewatenganisha Simba na nafasi ya pili ambapo watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika na Azam FC itakuwa ni Ligi ya Mabingwa Afrika.

MWENDO UMEGOTA MWISHO

Mtibwa Sugar ya Morogoro imemaliza mwendo ndani ya ligi pamoja na Geita Gold kwa kushuka daraja hivyo kuna kazi nyingine kwa wababe hao wawili kurejea kwa mara nyingine wakitokea katika Championship.

Mtibwa Sugar ni nafasi ya 16 pointi 21 huku Geita Gold nafasi ya 15 kibindoni ina jumla ya pointi 26 zote ni baada ya kucheza mechi 30 mashuhuda Yanga wakitwaa taji la ligi na pointi 80 kibindoni.

MLETE MGUNDA

Mgunda na Matola
Juma Mgunda na Seleman Matola makocha wa Simba msimu wa 2023/24. Source: Simba.

Juma Mgunda mrithi wa mikoba ya Abdelhak Benchkikha kwenye mechi ambazo amekaa benchi hajaonja ladha ya kupoteza pointi tatu mazima zaidi ya kuambulia sare mbili mbele ya Kagera Sugar kwa kufungana bao 1-1 na Namungo kwa kufungana mabao 2-2.

Simba 2-0 Mtibwa Sugar, Uwanja wa Azam Complex. Simba 2-0 Tabora United, Uwanja wa Azam Complex. Azam FC 0-3 Simba, Uwanja wa Mkapa. Dodoma Jiji 0-1 Simba, Uwanja wa Jamhuri na Simba 4-1 Geita Gold, Uwanja wa Azam Complex. Simba 1-0 KMC Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na Simba 2-0 JKT Tanzania. Mei kafunga kwa kutwaa tuzo ya kocha bora akiwashinda Miguel Gamondi wa Yanga na Bruno Ferry wa Azam FC.

WAAMUZI KWENYE MAAMUZI

Licha ya kazi kubwa ambayo wamefanya waamuzi kutokana na maamuzi yao kuna mechi ambazo zilizua gumzo. Miongoni mwa maamuzi yaliyoleta gumzo ni mchezo wa Simba dhidi ya Tabora United mpira wa Najims Musa kutafsriwa haujavuka lango na bao alilopewa Maxi Nzengeli mchezo dhidi ya Ihefu lilionekana halijavuka mstari.

Kuna kadi nyekundu mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na Yanga ilifungwa na kadi ya mchezo wa Yanga dhidi ya Coastal Union, kuna mengi ya kufanyia kazi msimu ujao wa 2024/25 ili kuwa bora zaidi.

 

Share this: