
TUZO moja ipo mikononi mwa kocha wa mpira Juma Mgunda akisepa nayo mbele ya wababe wawili ambao aliingia nao fainali ndani ya Mei 2024 ambao ulikuwa ni mwendo wa lala salama ndani ya Ligi Kuu Bara.
Ni Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba kasepa na tuzo hiyo baada ya kukiongoza kikosi hicho kwenye mechi 7 za ushindani ndani ya ligi wakisaka pointi tatu ambapo kama angepata ushindi mechi zote ni pointi 21 Simba ingekomba.
Katika mechi 7 ambazo ni dakika 630 Mgunda akishirikina na Seleman Matola pamoja na wachezaji walikomba jumla ya pointi 19 ndani ya uwanja. Ni ushindi katika mechi sita na sare moja ugenini ilikuwa Uwanja wa Kaitaba alipokomba pointi moja.
HIZI HAPA MECHI ZA MEI

Mechi ndani ya Mei kwa Simba chini ya Mgunda ilikuwa ni Simba 2-0 Mtibwa Sugar hii ilipigwa Uwanja wa Azam Complex, Simba 2-0 Tabora United, mechi hii ilichezwa Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo huu ulileta utata kutokana na shuti la kiungo Najim Mussa kuonekana kuvuka mstari lakini mwamuzi aliamini haukuvuka mstari wakati wachezaji wa Tabora United wanapambana kuzungumza na mwamuzi Simba walifanya shambulizi la kushtukiza wakafunga bao la pili.
Azam FC 0-3 Simba, mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Mkapa. Miongoni mwa mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa huku Simba walikuwa wanapewa nafasi ndogo ya kushinda kutokana na uimara wa kikosi cha Azam FC.
Ikumbukwe kwamba mkali wa kucheka na nyavu ndani ya Azam FC ni Feisal Salum ambaye alimaliza msimu wa 2023/24 akiwa na mabao 19 alipata nafasi ya penalti kwenye mchezo huo lakini iligonga mwamba.
Mabao ya Simba kwenye mchezo huo yalifungwa na Sadio Kanoute, Fabrince Ngoma na Duchu ambaye huyu alifunga bao lake la kwanza akiwa na Simba kwenye ligi alianzia benchi kusoma ramani za namna Mzizima Dabi ilivyokuwa ikienda kwa kasi.
Simba 4-1 Geita Gold kwenye mchezo huu mapema kabisa Geita Gold walianza kupata bao ambapo Hussen Abel alijichanganya kwenye kuokoa hatari mpira ukampokonyoka na kujigonga mguuni jambo lililowapa nafasii Geita Gold kufunga.
Mwisho walipindua matokeo kibabe na ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukasoma Simba 4-1 Geita Gold, pointi tatu zikiwa ni mali ya Simba kwa mara nyingine tena kwenye mchezo huo.
Simba 1-0 KMC, katika mchezo huu ngoma ilikuwa ni ngumu pale Arusha ambapo KMC walikuwa imara mwanzo mwisho kosa moja la kipa lilitumiwa na kiungo mshambuliaji Saido Ntibanzokiza kufunga bao dakika ya tatu na lilidumu mpaka mwisho wa mchezo.
Simba 2-0 JKT Tanzania, hii ilikuwa funga kazi kwa Simba ndani ya msimu wa 2023/24. Katika mchezo huu Simba ilipata mabao dakika za jioni kupitia kwa Ntibanzokiza ambaye alifunga penalti na kiungo mshambuliaji Willy Onana ambaye alifunga bao dakika ya 90.
Ikumbukwe kwamba penalti ilisababishwa na Onana dakika ya 88 na alifunga bao moja. Hivyo ilikuwa ni super sub kwa kuwa Onana kwenye mchezo huo alianzia benchi alipokuwa akisoma ramani namna mwendo unavyokwenda kwenye msako wa pointi tatu.
HAPA RAMANI ZILIVURUGIKA
Inatajwa kuwa miongoni mwa mchezo uliovuruga ramani za Simba kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa asilimia kadhaa ilikuwa ni dhidi ya Kagera Sugar kwa kuwa walikuwa kwenye nafasi nzuri kuvuna pointi tatu wakaishia kupata moja.
Ni Simba walianza kupata bao kwenye mchezo huo mwisho ubao wa Uwanja wa Kaitaba ukasoma Kagera Sugar 1-1 Simba. Bao la usawa kwa Kagera Sugar lilifungwa na mshambuliaji Obrey Chirwa.
KAWASHINDA HAWA HAPA MGUNDA

Mgunda amechaguliwa kuwa kocha bora ndani ya Mei akiwashinda Miguel Gamondi wa Yanga. Ipo wazi kwamba Yanga inayodhamiwania na SportPesa ni mabingwa wa ligi msimu wa 2023/24 wakifunga msimu waiwa na pointi 80.
Bruno Ferry wa Azam FC huyu ana uhakika pia timu yake kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa ni nafasi ya pili timu hiyo imegotea ikiwa sawa na Simba kwenye upande wa pointi tofauti mabao ya kufunga na kufungwa ambapo kibindoni ni pointi 69 wababe hao wanazo.
Bruno na Gamondi hawa Mgunda aliingia nao fainali kwa mujibu wa taarifa kutoka Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF). Hivyo kawashinda akiwa ni kocha bora ndani ya Mei 2024.
AZIZ KI NA FEISAL MBABE WAO

Upande wa mchezaji bora ni Reliants Lusajo mshambuliaji wa Mashujaa ya Kigoma ambapo aliwashinda Feisal Salum wa Azam FC na Aziz Ki wa Yanga. Hivyo kawashinda wababe hao kwenye msako wa mchezaji bora Mei.
Ndani ya Mei Lusajo alitimiza majukumu yake vema katika mechi nne akiwa chachu ya ushindi kati ya mechi sita ambazo Mashujaa ilishuka uwanjani.
Mashujaa ilikomba pointi 12 na ilipanda katika msimamo wa ligi ikimaliza nafasi ya 8 msimu wa 2023/24.
Mwamba huyo rekodi zinaonyesha kuwa alikomba dakika 432 katika mechi 6 alifunga mabao matano na pasi mbili za mabao akihusika kwenye mabao 7.

