LALA Salama-Ligi kuuazizi-ki-pic
Yanga bingwa
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara Yanga msimu wa 2023/24. Source: Yanga.

LALA salama Ligi Kuu Bara inazidi kushika kasi ambapo timu zimekuwa kwenye kazi kubwa ndani ya dakika 90 kusaka pointi tatu muhimu uwanjani kwenye mechi zao za mwisho msimu wa 2023/24.

Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ni mabingwa msimu wa 2023/24 wakiwa wamekusanya pointi 77 baada ya kucheza jumla ya mechi 29. Mchezo wao uliopita walikomba pointi tatu ugenini na kukabidhiwa taji la ligi kwa shangwe kubwa.

Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amebainisha kuwa ni furaha kwa timu hiyo kukamilisha malengo ya kutwaa ubingwa na wanatambua kila mchezaji alifanya kazi kubwa na ushirikiano kutoka kwa viongozi na mashabiki.

“Ilikuwa ni kazi kubwa kwenye mechi zetu zote mpaka hapa tulipofika lakini pongezi kwa mashabiki bila kusahau wachezaji kwa namna ambavyo walijituma kwenye kutimiza majukumu yao ndani ya uwanja.”

MATOKEO YA MZUNGUKO WA 29

 

Fei
KIUNGO Feisal Salum wa Azam FC mwenye mabao 18 ndani ya ligi. Source: Azam FC.

Ngoma ilikuwa nzito mzunguko wa 29 ambapo kila timu ilikuwa ikivuja jasho kusepa na pointi tatu uwanjani ilikuwa Mei 25 2024. Lala salama kila timu ilikuwa inapambana kufanya kweli kukamilisha vema hesabu za mzunguko wa 29.

Mchezo mmoja ulikusanya mabao mengi kwa timu moja ulichezwa Dar uliwahusisha matajiri wa Dar, Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo ambapo walikomba pointi tatu mazima dhidi ya Kagera Sugar.

Kwenye mchezo huo dakika 45 za mwanzo ngoma ilikuwa ngumu kwa timu zote mbili kushindwa kufunga. Kipindi cha pili hali ilibadilika kwa kila timu kucharuka na mwisho yakapatikana mabao sita ndani ya dakika 90.

Ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Azam FC 5-1 Kagera Sugar. Kwenye mabao hayo kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum alifunga mabao mawili ilikuwa dakika ya 72 na 79 huku Gibril Silla akifunga bao la utangulizi dakika ya 50, Kipre Junior alifunga bao moja dakika ya 65 na msumari wa tano ulifungwa na Nado dakika ya 90.

Bao pekee la kufutia machozi kwa Kagera Sugar kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa lilifungwa na Mbaraka Yusuph dakika ya 51. Ilikuwa ni dakika moja mbele baada ya kutoka kufungwa na Azam FC lakini walikwama kuongeza nguvu kwenye ulinzi wakaruhusu mabao manne.

Singida Fountain Gate 2-1 Geita Gold walikomba pointi tatu mbele ya Geita Gold huku Namungo wakigawana pointi mojamoja na Prisons kwa kufungana mabao 2-2 dhidi mchezo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa.

Ihefu wakiwa nyumbani Uwanja wa Liti walipoteza pointi tatu mazima kwa kushuhudia ubao ukisoma Ihefu 0-2 Dodoma Jiji.

Kutoka mwisho wa reli Kigoma, Mashujaa 3-2 Mtibwa Sugar. Mabao yalifungwa na Relliats Lusajo dakika ya 3 na 26 na bao moja lilifungwa na Mundhir Vuai dakika ya 33 huku Mtibwa Sugar wakifunga kupitia kwa Seif Karihe dakika 15 na Samson Madeleke alijifunga dakika ya 55.

Coastal Union ya Tanga walitoshana nguvu bila kufungana na JKT Tanzania kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa mwisho ubao ulisoma 0-0.

YANGA NA SIMBA ZAKOMBA TATU

Aziz KI Yanga
Aziz KI kiungo mshambuliaji wa Yanga mwenye mabao 18 ndani ya msimu wa 2023/24. Source Yanga.

Yanga wakiwa Uwanja wa Mkapa walikomba pointi tatu kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United.Ni Joseph Guede alipachika bao dakika ya 19, Maxi Nzengeli dakika ya 48 na Aziz KI bao la tatu dakika ya 90 kwenye mchezo huo.

 

Saido Ntibanzokiza
Saido Ntibanzokiza ki kiungo mshambuliaji wa Simba mwenye mabao 10 msimu wa 2023/24. Source Simba.

Simba ilikomba pointi tatu dhidi ya KMC kwenye mchezo wa mzunguko wa pili, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 1-0 KMC ambapo bao la ushindi lilifungwa na Saido Ntibanzokiza dakika ya tatu kwenye mchezo huo.

AZIZ KI NA FEI TOTO VITA BADO MBICHI

Mbio za kiatu cha ufungaji bora ndani ya ligi inayokwenda kugota mwisho mzunguko wa pili zimeanza upya kwa mara nyingine tena.

Miamba wawili wanapambania kiatu hicho kwa sasa hivyo mchezo wa mwisho kwa kila mchezaji utaamua nani atakuwa nani. Fei alifunga mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar akafikisha mabao 18 akiwa ni mzawa mwenye mabao mengi Bongo.

Kwa upande wa Aziz KI kiungo wa Yanga, raia wa Burkina Faso alipachika bao moja kwenye mchezo dhidi ya Tabora United ilikuwa dakika ya 90 akifikisha mabao 18 pia kwenye chati ya ufungaji.

Nyota hawa wote wawili ni marafiki kwa kuwa Feisal kabla hajaibuka ndani ya Azam FC alikuwa akicheza Yanga hivyo wanatambua vizuri ni marafiki kwenye vita yao mpya kuwania ufalme kwenye kufunga ndani ya ligi.

Ipo wazi kuwa kila mchezaji ameweka wazi kuwa hafikirii kuhusu tuzo hiyo zaidi ni kuona timu inapata mafanikio kwa kufikia malengo yao muhimu. Yanga wametwaa ubingwa msimu wa 2023/24 huku Azam FC ikipambania kumaliza nafasi ya pili ili kupeperusha bendera ya Tanzania, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aziz amesema: “Kwenye kila mchezo ambao ninacheza kikubwa ni kuona kwamba timu inapata matokeo mazuri na kufikia malengo yake hilo ni jambo la kwanza kwenye upande wa kufunga mimi siipi kipaumbele zaidi ni kuona kwamba tunapata matokeo.

Fei amesema: “Ninafurahi pale ambapo tunashinda kwa kuwa kila mmoja anafurahia kuona tukipata matokeo mazuri. Kuhusu tuzo ya ufungaji hilo sifikirii sana ikitokea nitamshukuru Mungu kikubwa ni kuona tunapata matokeo mazuri kwenye mechi zetu.”

Share this: