
ITAFAHAMIKA mbivu na mbichi ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 kwa kila timu kutambua wapi itagotea baada ya dakika 90 kwenye kukamilisha ngwe ya mwisho katika msako wa pointi tatu ndani ya dakika 90 uwanjani.
Ile vita ya ubingwa muda wake umekwisha na sasa ni vita ya kiatu cha ufungaji bora,timu ambazo zitashuka daraja pamoja na nani kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi ambayo ushindani wake ni mkubwa mwanzo mwisho.
HIVI NDIVYO ITAKAVYOKUWA RATIBA

Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda itakuwa na kibarua kusaka pointi tatu dhidi ya JKT Tanzania inayonolewa na Malale Hamsini ndani ya dakika 90 za machozi na jasho.
Ipo wazi kwamba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza ugenini baada ya dakika 90 ubao ulisoma JKT Tanzania 0-1 Simba. Bao la kiungo Clatous Chama lilitosha kupeleka pointi tatu mazima Msimbazi kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mwanzo mwisho.
Uwanja wa Mkapa mchezo huo unatarajiwa kuchezwa. Simba kwenye msimamo ni nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 29 imekusanya pointi 66 kibindoni. Inakutana na JKT Tanzania ambayo ina pointi 32 ikiwa nafasi ya 12 kwenye msimamo.
GEITA GOLD V AZAM FC

Geita Gold itakuwa nyumbani ikiwa haijawa kwenye mwendo mzuri kwenye mechi zake za mzunguko wa pili chini ya Kocha Mkuu, Dennis Kitambi. Geita itawakaribisha Azam FC inayolewa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo.
Ikumbukwe kwamba kwenye mzunguko wa 29 Azam FC iliandika rekodi ya kuwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi kuliko timu zote ubao wa Uwanja wa Azam Complex uliposoma Azam FC 5-1 Kagera Sugar na mwamba Feisal Salum alitupia mabao mawili kwenye mchezo huo.
Geita Gold ipo nafasi ya 15 na pointi 25 ikiwa inakamilisha mzunguko wa pili ipo kwenye hatari ya kushuka daraja ikiwa itapoteza mchezo dhidi ya Azam FC ndani ya dakika 90. Azam FC ni nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 66.
MABINGWA YANGA KAZINI
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa haina cha kupoteza kwa kuwa tayari ni mabingwa wa msimu wa 2023/24 na walikabidhiwa taji lao kwenye mchezo wa mzunguko wa 29 dhidi ya Tabora United.
Kwenye mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 ambapo Aziz KI alifunga bao moja akifikisha mabao 18 kwenye chati ya ufungaji Bongo.
Watakuwa uwanjani kumenyana na Tanzania Prisons iliyo nafasi ya 6 na pointi zake 34 kibindoni mchezo wake uliopita iligawana pointi mojamoja na Namungo Uwanja wa Majaliwa.
NAMUNGO V TABORA UNITED
Namungo inayotumia Uwanja wa Majaliwa kwenye mechi za nyumbani itakabiliana na Tabora United iliyotoka kupoteza pointi tatu mchezo wake uliopita dhidi ya Yanga, Uwanja wa Mkapa.
WAGOSI WA KAYA V KMC
Coastal Union iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na uhakika wa kushirikisha mashindano ya kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika itakabiliana na KMC.
Ikumbukwe kwamba KMC ilitoka kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Simba kwa kufungwa bao 1-0 lililofungwa na Saido Ntibanzokiza. Kwenye msimamo Coastal Union ipo nafasi ya nne na pointi 42 huku KMC ikiwa nafasi ya tano na pointi 36.
IHEFU KAZINI
Ihefu yenye pointi 33 nafasi ya 10 kwenye msimamo itakuwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar yenye pointi 21 nafasi ya 16 kwenye msimamo uwezekano wake kubaki ndani ya ligi msimu wa 2023/24 kwa Mtibwa Sugar ni mdogo kwa kuwa imekaa kwenye hatari ya kushuka daraja muda mrefu.
MASHUJAA KWENYE HESABU
Mashujaa watakuwa Uwanja wa Lake Tanganyika wakikamilisha hesabu dhidi ya Dodoma Jiji kutoka makao makuu ya Tanzania kwenye mchezo wa 30 msimu wa 2023/24.
SINGIDA V KAGERA SUGAR
Singida Fountain Gate itakuwa na kazi ya kusaka ushindi kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar ambayo imetoka kupoteza pointi tatu dhidi ya Azam FC kwa kufungwa mabao 5-1 Uwanja wa Azam Complex.
MEZA ZINAPINDULIWA

Kwenye upande wa kazi ya kufunga kila timu inatambua kwamba kuna vita ya kupindua meza ndani ya dakika 90. Mwamba Aziz KI na Feisal Salum kila mmoja anamvutia kasi mwenzake nani atakuwa nani kwenye mchezo wa mwisho.
Viungo hawa washambuliaji kila mmoja ni namba moja kwa utupiaji ambapo Aziz KI kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tabora United alifunga bao moja akifikisha jumla ya mabao 18 kwenye ligi na ametoa pasi 8 za mabao.
Wakati meza yake ikisoma hivyo mwamba Feisal Salum ndani ya Azam FC kafunga jumla ya mabao 18 na pasi 7 za mabao hivyo wachezaji hawa wamekuwa na kasi kwenye kucheka na nyavu msimu wa 2023/24 ambao unakwenda kugota mwisho.
NAFASI YA PILI KUFAHAMIKA
Wababe wawili wenye wachezaji wazuri kila upande wanakwenda kutambua nani atakuwa nafasi ya pili kwenye msimu wa 2023/24 kutokana na kushabihiana kwenye pointi zao na mechi tofauti ikiwa ni idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam FC kete yao ya mwisho itakuwa ugenini dhidi ya Geita Gold wao wapo nafasi ya tatu na pointi 66. Safu ya ushambuliaji ya Azam FC imefunga jumla ya mabao 61 na ile safu ya ulinzi imeruhusu mabao 21.
Kwa upande wa Simba nayo ina pointi 66 nafasi ya tatu ambapo safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 57 huku ile ya ulinzi ikiruhusu mabao 25 msimu wa 2023/24.

