YangaPacome
Aziz KI
KIUNGO wa Yanga Aziz KI kwenye mazoezi. Source: Yanga.

YANGA moto hauzimi ndani ya uwanja dakika 90 za msako wa ushindi kutokana na mwendelezo wakupata matokeo kwenye mechi za ushindani 2023/24. Kabatini wana mataji 29 ya ligi wakiwa wanafukuzia taji moja kukamilisha mataji 30.

Ipo wazi kwamba timu hiyo inayodhaminiwa na SportPesa ni mabingwa watetezi wa ligi na CRDB Federation Cup ambapo wametinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 3-0 Tabora United kwenye mchezo wa hatua ya robo fanali.

 

YANGA DHIDI YA IHEFU

Yanga inakwenda kukutana na Ihefu katika mchezo wa hatua ya nusu fainali katika msako wa timu ambayo itatinga hatua ya fainali ndani ya CRDB Federation Cup ambapo watani zao wa jadi Simba waligotea hatua ya 16 bora.

Kwenye mechi mbili ambazo wamekutana na Ihefu ilikuwa ni dakika 180 nyumbani na ugenini hivyo wanakwenda kukutana mara ya tatu msimu wa 2023/24 na Ihefu inayofundishwa na Mecky Maxime.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza ilikuwa Ihefu 2-1 Yanga na ule wa mzunguko wa pili Uwanja wa Azam Complex ilikuwa Yanga 5-0 Ihefu.

Ushindi wa Yanga 3-0 Tabora United katika robo fainali CRDB Federation Cup inawapelela Yanga hatua ya nusu fainali watamenyana na Ihefu katika msako wa timu itakayotinga fainali.

Mabao ya Yanga katika robo fainali Uwanja wa Azam Complex yalifungwa na Aziz KI, Kennedy Musonda na Joseph Guede.

 

HUYU HAPA GAMONDI

Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa kikubwa ambacho kinahitajika kwenye mechi ambazo wanacheza ni kupata ushindi pamoja na kutoa burudani kwa mashabiki wanaojitokeza uwanjani.

“Wachezaji wanajituma kwenye kutimiza majukumu yao hilo ni muhimu na tunakazi yakuendelea kufanya vizuri kwa mechi zinazofuata kutokana na kila mpinzani kuwa na hesabu za kutafuta ushindi.

“Muda ni sasa kufanyia kazi makosa ambayo yametokea kwenye mechi zetu, muhimu ni kuwa imara kutokana na utayari ambao upo hivyo mashabiki waendelee kuwa pamoja nasi katika mechi zetu zote,”.

AZIZ KI KATIKA UBORA WAKE

Guede na Aziz
Guede na Aziz nyota wa Yanga wakishangilia moja ya bao uwanjani. Source:Yanga

Mwamba Aziz KI kiungo mshambuliaji wa Yanga yupo kwenye ubora wake kutokana na kazi yake anayofanya ndani ya uwanja kila akipata nafasi kitaifa na kimataifa.

Kwenye ligi ni namba moja katika utupiaji akiwa amefunga jumla ya mabao 15 anafuatiwa na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ambaye yeye katupia mabao 14.

Aziz KI ni chaguo la kwanza ndani ya kikosi cha Gamondi akiwa ni mtaalamu wa mapigo huru pia katika penalti pamoja na faulo huku mguu wake wenye nguvu ukiwa ni ule wa kushoto.

Kafunga mabao 13 akitumia mguu wa kushoto na mabao mawili amefunga ndani ya ligi akitumia mguu wa kulia. Miongoni mwa timu ambazo kazitungua ni pamoja na watani zake wa jadi Simba.

 

MABORESHO MAKUBWA YANAKUJA

Kibabage
Kibabage beki wa kupanda na kushuka ndani ya kikosi cha Yanga. Source: Yanga

Licha ya kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa inaukimbiza ubingwa wa 30 ndani ya Ligi Kuu Bara bado inaelezwa kuwa kuna maboresho makubwa yanakuja ndani ya kikosi hicho.

Taarifa zinaeleza kuwa wapo wachezaji ambao wameshamalizana na timu hiyo kwa kusaini dili jipya kuendelewa kuwa ndani ya timu hiyo inayonolewa na Gamondi.

Moja ya mpango mkubwa unaofanyika ni kuboresha mikataba ya wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho na kufanya mazungumzo na wachezaji wapya wa kitaifa na kimataifa.

Kazi imeanza ambapo moja ya wachezaji waliokamilisha dili la kusaini mkataba mpya ni Nickson Kibabe beki aliyekuwa hapo kwa mkopo akitokea Singida Fountain Gate. Nyota huyo amekuwa na mwendelezo mzuri ndani ya uwanja kutokana na ubora wake.

Kibabage beki wa kupanda na kushuka alikuwa anatajwa kupigiwa hesabu na Simba jambo ambalo lilifanya mabosi wa Yanga kumalizana mapema na anatajwa mkataba wake umegharimu milioni 100.

Upande ambao unafanyiwa kazi kubwa ni eneo la ushambuliaji ambapo inatajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji ambao wapo kwenye hesabu hivyo watafanya kazi kubwa kuongeza wachezaji wengine kwenye eneo hilo.

 

Yanga imepanga kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wenye uzoefu na uwezo wa kucheza michuano ya kimataifa na ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu wa 2023/24 kugotea hatua ya robo fainali.

 

Guede
Guede mshambuliaji wa Yanga kwenye moja ya mchezo wa CRDB Federation Cup. Source:Yanga

Ipo wazi kwamba ni Mamelodi waliwaondoa Yanga kwa changamoto ya penalti baada ya kutoshana nguvu ndani ya dakika 180. Kuondolewa kwenye hatua ya robo fainali kumewapa hasira mabosi wa Yanga ambao wanataka kuja kivingine kabisa.

 

Kwenye msimamo wa ligi Yanga ni nafasi ya kwanza na pointi 62 baada ya kucheza mechi 24 safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao 55 ikiwa ni namba moja kwa safu kali za ushambuliaji.

Share this: