
MTIBWA SUGAR 2023/24 wanajitafuta wakulima hao wa miwa katika kupata matokeo ndani ya uwanja jambo ambalo linafanyiwa kazi na benchi la ufundi kwa ukaribu ili timu hiyo kusalia ndani ya ligi kwa kuwa haijawa kwenye mwendo mzuri.
Ipo wazi kwamba timu hiyo haijawa kwenye mwendo mzuri kutokana na kushindwa kupata pointi tatu katika mechi zake za ushindani kwenye msako wa pointi tatu ndani ya ligi ambapo mabingwa watetezi ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa jambo linaloifanya iwe kwenye nafasi iliyopo kwa sasa.
Mchezo wake wa kwanza wa msimu ilikuwa nyumbani ilikuwa dhidi ya Simba ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Manungu ukisoma Mtibwa Sugar 2-4 Simba. Ikiwa nyumbani iliacha pointi tatu mikononi mwa mnyama.
Hiyo ilikuwa ni 2023, Agosti 17 ambapo mwamuzi wa kati kwenye mchezo huo alikuwa ni Nassoro Mwinchui na kikosi cha Simba kilikuwa kinanolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ambaye alipewa mkono wa asante.
Simba kwa sasa inanolewa na Kocha Mkuu Juma Mgunda akishirikiana na Seleman Matola ambao mchezo wao wa kwanza unatarajiwa kuwa dhidi ya Namungo Aprili 30 2024 Uwanja wa Majaliwa.
Haya yote yanatokea baada ya Abdelhak Benchikha mrithi wa mikoba ya Oliveira kuomba kuondoka ndani ya kikosi hicho kinachopambania malengo yake kwenye ligi hivyo kuna mengi yamebadilika lakini mwendo wa Mtibwa Sugar bado haujawa imara.
MWENDO WAKE APRLI UNASHTUA

Aprili haijawa njema kwa Mtibwa Sugar kutokana na mwendo wake kushtua kwa kukwama kupata matokeo katika mashindano ambayo ilishiriki kwa nyakati tofauti kuanzia CRDB Federation Cup na Ligi Kuu Bara.
Haijalishi iwe inacheza nyumbani ama ugenini ngoma ilikuwa ngumu kwa kuwa mambo hayakuwa mazuri katika kupata matokeo ndani ya dakika 90 uwanjani chini ya Kocha Mkuu, Zuber Katwila akishirikiana na Awadhi Juma wanaokinoa kikosi hicho kinachotumia wachezaji wengi wazawa kikosi cha kwanza.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa CRDB Federation Cup ikiwa ugenini ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Azam FC 3-0 Mtibwa Sugar. Hivyo safari yao kwenye mashindano hayo hapo ilikuwa ni mwisho mpaka wakati mwingine tena.
Aprili 13 ilikuwa mchezo wa Ligi Kuu Bara wakiwa Uwanja wa Manungu ulisoma Mtibwa Sugar 2-2 Geita Gold wakagawana pointi mojamoja. Katika mchezo huo Mtibwa Sugar walikuwa na nafasi ya kupata matokeo mazuri lakini ikawa tofauti.
Pointi moja waliyopata iliwaongezea nguvu kwenye pointi kibindoni lakini walibaki palepale kwenye nafasi yao ambayo ni hatari kama msimu utakamilika ikiwa hapo itashuka daraja mazima na kushiriki Championship.
Aprili 16 2024 ilikuwa Mtibwa Sugar 0-1 KMC katika mchezo huu bahati haikuwa kwa Mtibwa Sugar kwa kuwa walipata pigo la penalti ikaokolewa na KMC, hivyo walipoteza pointi tatu mazima.
Ndani ya dakika 180 kwenye msako wa pointi sita waliambulia pointi moja ikiwa tano wakizipoteza jambo ambalo linawaumiza mashabiki na viongozi wa timu hiyo.
Mchezo wa kukamilisha Aprili kuelekea Mei Mosi ilikuwa ni Aprili 28 2024 walipokuwa ugenini baada ya dakika 90 ubao wa Meja Isamuhyo ulisoma JKT Tanzania 2-1 Mtibwa Sugar.
Mtibwa Sugar imefunga Aprili kwa kupoteza pointi tatu ina kazi kubwa kwenye mechi zinazofuata kusaka ushindi kuongeza kasi ya kupata matokeo ndani ya uwanja.
MIKONONI MWA MNYAMA

Baada ya kumalizana na JKT Tanzania ugenini kituo kinachofuata ni dhidi ya Simba ikiwa ni mzunguko wa pili kwa kuwa mzunguko wa kwanza walikuwa nyumbani na kupoteza pointi tatu mazima.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili ambapo Mtibwa Sugar wanapambana kupata pointi tatu na Simba inapambana kurejea kwenye ubora wake.
NENO LA MTIBWA SUGAR
Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Juma ameweka wazi kuwa hakuna tatizo ambalo linawakabili bali ni hali ya kisaikolojia ambayo inapaswa kufanyiwa kazi kwa kupata matokeo kwenye mechi zake za ushindani.
“Hakuna ambacho kinatusumbua kwa wakati huu zaidi ni saikolojia ya wachezaji kuwa sawa kwa kupata matokeo katika mechi zetu ikiwa hivyo tutarejea kwenye mwendo mzuri.
“Ari ya wachezaji ni kubwa na wanafanya vizuri kwenye uwanja wa mazoezi hivyo malengo yetu ni kuona kwamba tunapata matokeo chanya ndani ya uwanja na inawezekana,”.
