
KOCHA Abdelhakh Benchikha, kocha wa kazi amesema kuwa malengo makubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni kucheza hatua ya nusu fainali na kutwaa ubingwa lakini ilishindikana kwa kuwa haikuwa mipango ya Mungu timu hiyo kufikia hayo msimu wa 2023/24.
Aprili 28 2024 Simba ilitoa taarifa rasmi kuwa wamefikia makubaliano ya pande mbili kuvunja mkataba kati ya Simba na kocha Benchikha pamoja na Wasaidizi wake wawili Kamal Boujnam na Farid Zemit.
Sababu ya Benchikha kuweka mkataba uvunjwe ni matatizo ya kifamilia yanayomkabili nyumbani kwao Algeria na sasa timu ya Simba itakuwa chini ya Juma Mgunda na Seleman Matola hadi hapo Bodi ya Wakurugenzi itakapotoa uamuzi mwingine.
Benchikha amesema:” Malengo katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni kuona kwamba tunafika hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika lakini haikuwa mipango ya Mungu.
“Tumeondolewa na Al Ahly hii sio timu ndogo ni timu kubwa ambayo inafanya vizuri kwenye mashindano yake kitaifa na kimataifa, “.
KOCHA NA KOMBE LA MUUNGANO

Katika moja ya aliyowaachia Simba kwa kwenye benchi la ufundi ni Kombe la Muungano 2024 baada ya kufanikiwa kushinda kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Azam FC.
Kwenye mchezo wa fainali Aprili 27 2024 ubao wa Uwanja wa New Amaan Complex ulisoma Azam FC 0-1 Simba na bao la ushindi likifungwa na kiungo mkabaji Babacarr Sarri.
Bao hilo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho likiwa ni taji pekee ambalo amelitwaa akiwa kwenye benchi la ufundi ndani ya Simba.
NENO LA SEMAJI

Muda mfupi baada ya taarifa rasmi kutolewa kuhusu kuondoka kwa kocha huyo katika majukumu yake ndani ya kikosi cha Simba, Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amebainisha kuwa kocha huyo ni moja kati ya kocha bora kuwahi kuwa ndani ya Simba.
“Haikua rahisi kumpata mwalimu wa kaliba yake na hakuna aliyeamini kama tungemudu kuwa na kocha wa aina hiyo. Kumpata mwalimu huyu ni ishara kuwa viongozi wetu walionesha dhamira ya dhati ya kuipeleka Simba kwenye kilele cha mafaniko makubwa zaidi.
“Ukubwa wa mwalimu Benchikha na gharama za kuwa na mwalimu wa aina yake ni dhahiri kuwa viongozi wetu wakiongozwa na Mo Dewji walijitoa mhanga kwa maslahi ya kuiboresha Simba yetu.
“Juhudi ya kwanza ilikua ni kumleta kocha jambo ambalo limefanyika kwa asilimia mia juhudi ya pili ilikua ni kubaki nae. Kocha kubaki kazini au muajiriwa yeyote kubaki kazini hutegemea pia na matakwa ya muajiriwa binafsi.
“Wana Simba tutulie tuwape muda viongozi wetu watafute kocha mwingine mzuri kwa maslahi ya timu. Kama waliweza kumleta Benchikha basi wanaweza kuleta yeyote mzuri kwa maslahi ya Simba yetu. Maisha yanaendelea.
NAFASI YA SIMBA

Kwenye Ligi Kuu Bara Simba ipo nafasi ya tatu baada ya kucheza jumla ya mechi 21 msimu wa 2023/24 imekusanya pointi 46 huku safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ikifunga jumla ya mabao 41.
Ndani ya tatu bora kwenye ligi ni namba tatu pia kwa safu ya ushambuliaji iliyofunga mabao mengi huku ile inayoongoza ni Yanga yenye jumla ya mabao 55 baada ya kucheza jumla ya mechi 24.
Ipo wazi kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ni mabingwa watetezi wakiwa nafasi ya kwanza na kukusanya jumla ya pointi 62 kibindoni.
Mchezo wao uliopita kwa Yanga inayofundishwa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ilikuwa dhidi ya Coastal Union ya Tanga ambapo baada ya dakika 90 walikomba pointi tatu mazima.
Bao pekee la ushindi kwenye mchezo huo lilifungwa na Joseph Guede hivyo wamezidi kuwaacha mbali wapinzani wao Simba kwenye msako wa ubingwa wa ligi.
Namba mbili kwa safu kali eneo la ushambuliaji ni Azam FC ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ni mabao 50 timu hiyo imefunga baada ya kucheza jumla ya mechi 24 kama ambazo Yanga imecheza.
Simba ina mechi tatu kuwafikia wapinzani wao ndani ya tatu bora na moja ya mchezo wao wanatarajiwa kukutana na Azam FC waliotoka kucheza kwenye fainali ya Kombe la Muungano.
MCHEZO WA MWISHO DABI
Mchezo wa mwisho kukaa kwenye benchi la ufundi Benchikha ndani ya ligi ilikuwa ni Kariakoo Dabi dhidi ya watani wa jadi Yanga ambapo baada ya dakika 90 alishuhudia ubao ukisoma Yanga 2-1 Simba.
Mabao kwenye mchezo huo yalifungwa na Aziz KI na Joseph Guede kwa upande wa Yanga na lile la Simba lilifungwa na Michael Fred.
Ndani ya dakika 180, Simba imedondosha pointi sita mbele ya watani zao wa jadi Yanga ambao wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi.

