
VITA inaendelea ndani ya kikosi cha Yanga kinachodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa kwenye msako wa pointi tatu ndani ya msimu wa 2023/24 licha ya kutoshana nguvu na wajeda JKT Tanzania kwenye mchezo wao wa ligi mzunguko wa pili ambao ulikuwa na ushindani mkubwa ndani ya dakika 90.
Katika mchezo huo kila timu hesabu ilikuwa ni kukomba pointi tatu mwisho hakuna ambaye alifanikisha malengo hayo zaidi ya kugotea kugawana pointi mojamoja. Matokeo hayo yanaifanya JKT Tanzania kufikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 23 huku wakipunguza idadi ya mabao waliyofungwa mzunguko wa kwanza na kufanikiwa kuambulia pointi kwa vinara hao wa ligi.
Licha ya matokeo hayo,
wameweka wazi kuwa wataendelea kupambania kufikia malengo huku JKT Tanzania wakibainisha kuwa walikuwa kwenye ubora wakiwapa tabu Yanga ambao bahati ilikuwa upande wao hawakufungwa.
Masau Bwire, Ofisa Habari wa JKT Tanzania amebainisha kuwa wachezaji walikuwa na ari kubwa kusaka ushindi kwenye mchezo huo wakiwa nyumbani mbele ya Yanga.
“Tulikuwa tunahitaji kupata pointi tatu mbele ya Yanga, wachezaji wamecheza vizuri lakini hatujapata matokeo mazuri tunaamini kwenye mechi zinazofuata tutaendelea kupambana ili kupata matokeo mazuri,”.
HAPA TATIZO LIPO
Bakari Mwamnyeto nahodha wa Yanga ameweka wazi kuwa moja ya sababu kubwa iliyofanya wakakosa ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania ni sehemu ya kuchezea kutokuwa rafiki.

Ipo wazi kwamba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza walipokutana na JKT Tanzania Uwanja wa Azam Complex, Yanga ilikomba pointi zote tatu mazima kwa ushindi wa mabao 5-0.
Mchezo wa mzunguko wa pili uliokuwa na ushindani mkubwa ulichezwa Aprili 24 ubao wa Uwanja wa Meja Isamuhyo ulisoma JKT Tanzania 0-0 Yanga hivyo wababe hawa wawili waligawana pointi mojamoja kwenye mchezo huo.
Mwamnyeto ameweka wazi kuwa ulikuwa ni mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa hawakuwa na namna kwa kuwa waliambiwa wacheze hivyo walitimiza majukumu yao kwa umakini.
“Kikubwa ilikuwa sehemu ya kuchezea haikuwa rafiki kwetu, uwanja ulijaa matope kwenye baadhi ya sehemu hivyo kutupa tabu kucheza lakini tunamshukuru Mungu tumepata pointi moja.
“Malengo ilikuwa ni kupata pointi tatu muhimu ila kwa hii pointi moja sio mbaya licha ya kwamba tumepoteza pointi mbili kwenye mchezo wetu,”.
MSIKIE GAMONDI

Masta wa mipango ndani ya Yanga, Miguel Gamondi ambaye ni Kocha Mkuu wa timu hiyo yenye maskani yake Jangwani, amebainisha kwamba kila mmoja ameona namna ilivyokuwa kwenye mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania hivyo hakuna ambacho kitabadilika.
Gamondi ametoka kuingoza timu hiyo kukomba pointi tatu kwenye mchezo dhidi ya Simba uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Aprili 20 2024 na dakika 90 ubao ukasoma Yanga 2-1 Simba hivyo walikomba pointi tatu.
Ipo wazi kwamba kwa msimu wa 2023/24 Yanga imekomba pointi sita mbele ya Simba kwa kuwa mchezo wa mzunguko wa kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 na mzunguko wa pili ilikuwa Yanga 2-1 Simba.
Jumla Yanga imewafunga Simba mabao 7 huku safu yao ya ulinzi ikifunga jumla ya mabao mawili ndani ya dakika 180 za Kariakoo Dabi iliyokuwa na ushindani mkubwa ndani ya uwanja kwa wababe hao.
Baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania Gamondi amesema kuwa wachezaji walijituma kutafuta matokeo lakini haikuwa bahati kwa upande wao kutokana na mazingira yalivyokuwa.
“Tulikuja kwenye mchezo kusaka ushindi yaani kupata pointi tatu lakini ilikuwa tofauti kutokana na mazingira namna ambavyo yalikuwa. Kila mchezaji alikuwa anajituma na ilikuwa hivyo mwanzo mwisho lakini hakuna namna.
“Kikubwa ambacho tunakitafuta kwenye mechi zetu zote ni pointi tatu ila kupata pointi moja sio haba kwani ni muhimu kuyafuata malengo yetu na bado kuna mechi ambazo tunapaswa kucheza tutajitahidi kupata matokeo mazuri,”.
NAFASI YA YANGA KWENYE LIGI
Yanga imecheza jumla ya mechi 23 kwenye ligi msimu wa 2023/24 imekusanya pointi 59 kibindoni ikiwa ni namba moja kwa timu iliyokusanya pointi nyingi na inaongoza ligi.
Mbali na kuongoza ligi, Yanga inaongoza kwa timu yenye safu kali ya ushambuliaji ambapo ni mabao 54 timu hiyo imefunga kwenye mechi zake za ligi ambazo ilishuka uwanjani kwenye msako wa pointi tatu.
Ushindi kwa Yanga ni kwenye mechi 19 ikiambulia sare mbili na kupoteza mechi mbili uwanjani dhidi ya Ihefu mchezo uliochezwa Uwanja wa Highland Estate, Mbeya na dhidi ya Azam FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Mwamba Aziz KI ni namba moja kwa mastaa wenye mabao mengi ndani ya ligi akiwa katupia jumla ya mabao 15 kibindoni na mguu wake wenye nguvu ni ule wa kushoto ambao umekuwa ukiwapa adhabu makipa wengi kwenye ligi ya Bongo.
Katumia mguu wa kushoto kufunga jumla ya mabao 13 akifunga mabao mawili kwa mguu wake wa kulia nyota huyo chaguo la kwanza la Gamondi kwenye mechi za ushindani kitaifa na kimataifa.

