Mitambo Mudathir YahyaMudathir Yahya
  • Habari njema kwa Yanga mitambo ya kazi ipo kamili kimataifa dhidi ya Mamelodi kwa Mkapa
  • Pacome ashusha presha kitaeleweka mchezo wa kimataifa mbele ya mashabiki wao
  • Mageti kufunguliwa mapema kwa ajili ya mashabiki kuingia kushuhududia burudani

MITAMBO ya kazi Yanga imerejea katika ubora ikiwa ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns. Itakuwa ni Uwanja wa Mkapa Machi 30 2024 kwa timu hizo mbili kupambana kusaka ushindi ndani ya uwanja.

Ipo wazi kuwa kuna wachezaji wa Yanga ambao walikuwa na timu ya taifa kwenye mechi za FIFA Series hao mapema waliwasili kambini tayari kuanza maandalizi ya mwisho ya mchezo huo mkubwa unaosubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki wa mpira kila kona.

Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa ndani ya Ligi Kuu Bara ina kazi ya kutetea taji hilo ikiwa na mtihani wa kufanya kazi nyingine kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali. Mchezo wa kwanza utachezwa Dar na ule wa pili itakuwa Afrika Kusini.

Baada ya kucheza mechi 20 ndani ya ligi imepoteza mechi mbili ilikuwa dhidi ya Ihefu ugenini na mchezo dhidi ya Azam FC ambao ulichezwa Uwanja wa Mkapa. Mchezo wao wa mwisho kabla ya kuwakabili Mamelodi walishuhudia ubao ukisoma Azam FC 2-1 Yanga hivyo wana hasira za kupoteza.

Katika mchezo dhidi ya Azam FC wachezaji wa Yanga chaguo la kwanza la Gamondi walipata maumivu kwenye mchezo huo na hawakufanikiwa kukamilisha dakika 90 kwenye mchezo huo na sasa wanapambania hali zao kurejea kwenye ubora ikiwa ni pamoja na Pacome Zouzoua, Yao Atohoula.

MAMELODI WATUMA UJUMBE HUU

Wapinzani wa Yanga kwenye hatua ya robo fainali Mamelodi Sundowns wametuma ujumbe kwa wapinzani hao kwa kubainisha kwamba wao wanaendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo na mpango mkubwa ni kuona kwamba wanapata matokeo mazuri.

Rhulani Mokwena, Kocha Mkuu wa Mamelodi mwenye sifa ya mpangilio mzuri wa mavazi pamoja na soka safi la kushambulia kwa kasi ameweka wazi kuwa anatambua uwezo wa kocha Miguel Gamondi pamoja na kasi ya Yanga hivyo wanajiandaa kukabiliana nao.

“Tunakwenda kukutana na timu ambayo inafanya vizuri kwenye mechi zake hilo lipo wazi tunatambua ni namna gani tunapaswa kufanya katika mchezo wetu, kikubwa ni kuona tunakuwa tayari kwa kuwa hatua tuliyopo ni muhimu kutafuta matokeo,”.

MITAMBO YAREJEA KAZINI

ALI Kamwe
OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe akitoa maelekezo kwenye moja ya mkutano na waandishi wa Habari. Source:Yanga

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe ameweka wazi kuwa wachezaji waliokuwa kambini na timu ya taifa tayari wamesharejea kambini na kujiunga na timu kwa maandalizi ya mchezo wao wa kimataifa.

Ni Mudathir Yahya, Ibra Bacca, Clement Mzize hawa hawakuwa na timu kwenye maandalizi ya awali kutokana na kuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa lakini kwa sasa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Mamelodi Sundowns.

“Wachezaji waliokuwa na timu ya taifa wamerejea kambini na kuanza maandalizi ya mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Mamelodi Sundowns hivyo kikosi kimekamilika na mitambo ya mabao imerejea kazini.

MITAMBO YA KAZI KAZINI TENA

Pacome Zouzoua
PACOME Zouzoua kiungo wa kazi ndani ya Yanga kwenye moja ya majukumu yake kimataifa. Source: Yanga

Kuhusu mitambo ya kazi ambayo haikuwa fiti kutokana na maumivu taarifa mpya zinaeleza kuwa tayari wachezaji wamezidi kuimarika ikiwa ni tayari kuelekea mchezo wao wa kimataifa.

Kamwe amesema: “Zawadi Mauya ameanza mazoezi, Kibwana Shomari asilimia 60 ya utimamu tayari ameanza mazoezi lakini bado hajaanza mazoezi na wenzake, Khalid Aucho yupo tayari kwa mchezo, Yao yeye ni nunusunusu kucheza ama kutokucheza mchezo huo kuhusu Pacome profesa wa mpira ni mashahidi yeye alipata nafasi ya kuwa kwenye benchi mchezo wa kirafiki akiwa na timu ya taifa ya Ivory Coast hivyo inamaanisha kwamba ameimarika.

“Tunaendelea kumuomba Mungu atujaalie hadi kufikia siku ya mchezo wachezaji wawe fiti kwa ajili ya kupambania nembo ya Yanga ndani ya dakika 90.

MUDATHIR DAY

Mudathir Yahya
Mudathir Yahya kiungo wa Yanga akishangilia moja ya bao kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Source: Yanga

Kiungo wa Yanga, Mudathiri Yahya amekabidhiwa mchezo kijana wa Kizimkazi kutokana na kazi kubwa ambayo ameifanya kwenye mechi za hivi karibuni na nembo ya Yanga iliyo kwenye kampeni za mchezo huo inaeleza kuwa kila mmoja apige simu kuwaita mashabiki.

“Simu ziite sasa, waambie hao wapinzani wetu kazi yao kutamba ni huko lakini hapa mwisho tunakwenda kufanya kweli. Tupo tayari na wachezaji wapo tayari,”.

 

 

Share this: