
MASTAA wanne wa kimataifa akiwemo Muivory Coast, Pacome Zouzoua na pacha wake Aziz Ki Stephanie rasmi kesho Jumatano wanatarajia kutua nchini na kujiunga na kikosi cha Yanga kujiandaa na mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Pamoja na Pacome, Yanga ilikosa huduma ya mastaa wao wanne wa kimataifa ambao ni kipa, Djigui Diarra aliyekuwa na majukumu ya timu ya Taifa ya Mali, mshambuliaji Kennedy Musonda wa Zambia na Aziz Ki aliyekuwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Burkina Faso.
MECHI KUPIGWA JUMAMOSI KWA MKAPA

Yanga Jumamosi ya Machi 30, mwaka huu wanatarajia kuwa wenyeji wa Mamelodi katika mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
PACOME ASHUSHA PRESHA MAJERUHI YANGA

Uongozi wa Yanga hivi karibuni ulitangaza kuwa mastaa wao watano hali zao za kiafya bado hazijaimarika kutokana na kupata majeraha na walikuwa katika hatari ya kukosekana katika mchezo huo.
Lakini taarifa mpya na njema kuhusu hilo ni kuwa sehemu kubwa ya majeruhi wamerejea na wako tayari kucheza mchezo huo akiwemo Pacome ambaye taarifa ni kuwa kwa sasa yuko fiti kwa zaidi ya asilimia 85.
Uwepo wa nyota hao waliokuwa na majeraha katika mchezo wa Jumamosi kunategemea na watakavyoimarika na namna ambavyo watazidi kuimarika.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa ndani ya Ligi Kuu Bara imekuwa na mwendelezo mzuri kwa kupata matokeo kwenye mechi zake ilizocheza ikipoteza mechi mbili na inaongoza ligi msimu huu wa 2023/24.
Baada ya kucheza mechi 20 ndani ya ligi imepoteza mechi mbili dhidi ya Ihefu ugenini na mchezo dhidi ya Azam FC ambao ulichezwa Uwanja wa Mkapa, ambao pia walikuwa ugenini.
WALIOTAJWA KUWA MAJERUHI YANGA
Zouzoua Pacome
Huyu ni kiungo mshambuliaji chaguo la kwanza la kocha, Miguel Gamondi. Nyota huyo alipata majeraha ya goti kwenye mchezo dhidi ya Azam uliochezwa Uwanja wa Mkapa Machi 17, ambapo alianza kikosi cha kwanza na kutolewa dakika ya 30 tu ya mchezo.
Licha ya majearaha hayo Pacome alikuwa miongoni mwa mastaa ambao waliitwa kwenye timu ya taifa ya Ivory Coast kufuatia majeraha ya kiungo Ibrahim Sangare anayekipiga huko England.
Khalid Aucho
Kiungo wa kimataifa wa Uganda ambaye hivi karibuni majeraha ya goti na kulazimika kufanyiwa upasuaji.
Zawadi Mauya
Kiungo mzawa ambaye pia hakuwa fiti lakini kwa sasa amepona kabisa hivyo kushusha presha kuelekea mchezo dhidi ya Mamelodi.
Yao Attohoula
Habari si nzuri sana kwa upande wake kwani Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Ali Kamwe ameweka wazi kuwa bado ana asilimia hamsini za kucheza na asilimia 50 za kutocheza.
Yao mpaka sasa kwenyre Ligi Kuu Bara ametoa pasi saba (7) za mabao alipata majeraha ya misuli ya paja.
Kibwana Shomari
Kiraka mwingine ambaye anasumbuliwa na majeraha ya enka ambayo aliyapata kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Kwenye mchezo huo Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo mshambuliaji Aziz KI akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya Geita Gold.
ALICHOSEMA ALI KAMWE

Ofisa Habari wa Yanga amewekà wazi kuwa hakuna cha kuhofia kuelekea mchezo wao huo dhidi ya Mamelodi na kwa sasa wamewekeza nguvu kwenye maandalizi.
“Tunashukuru kuwa taarifa ya madaktari kwenda kwenye benchi la ufundi inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya majeruhi wameimarika.
“Hatuhofii mchezo huu bali tunajiandaa kikamilifu, jambo la msingi ni kuwa pamoja kama timu kuanzia kwa viongozi, mashabiki, benchi la ufundi na wachezaji.
“Taarifa njema ni kuwa wachezaji wetu waliokuwa na majukumu ya kimataifa wanatarajiwa wote kuripoti siku ya Machi 27, mwaka huu ambapo watakuwa na vipindi vinne vya mazoezi ya pamoja na wenzao kujiandaa na mchezo huo.
“Tunaamini kuwa wachezaji wote watafika ndani ya muda sahihi kwa kuwa hayo ndiyo makubaliano yetu na wao na mashirikisho ya soka ya nchi wanazotoka, ambapo baada ya kuwa kamili maandalizi ya mwisho yatafanyika lakini niwahakikishie Wananchi kuwa Mamelodi Wanakufa kwa Mkapa,” amesema Ali Kamwe.
