KUELEKEA mchezo wao wa leo Jumatano dhidi ya Tanzania Prisons, uongozi wa Simba umetamba kuwa umejipanga kuendeleza shangwe kwa mashabiki wao kwa kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi.
Simba wanatarajia kuingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kukusanya pointi saba katika michezo yao mitatu Kanda ya Ziwa wakishinda michezo miwili na kutoa sare dhidi ya Azam FC.
Mabingwa hao mara 22 wa Ligi Kuu Bara pia wataingia katika mchezo huu wakiwa wametoka kupata matokeo bora ya ushindi wa kishindo wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy mchezo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Jumamosi iliyopita.
Ushindi huo uliwafanya Simba wakate tiketi ya kucheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo wamefanya hivyo kwa mara ya nne katika kipindi cha misimu mitano iliyopita.
MSIMAMO WA LIGI KUU MPAKA SASA

Mpaka sasa Simba ambao wamewahi kupata udhamini mnono wa SportPesa wanakamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kukusanya pointi 36 katika michezo 15 ambayo wamecheza mpaka sasa na mchezo wa leo unakuwa mchezo wa 16.
Vinara wa msimamo wa ligi mpaka sasa ni Yanga ambao wamekusanya pointi 43 baada ya kucheza michezo 16.
Nafasi ya pili inakamatiwa na Azam ambao pia wamekusanya pointi 43 katika michezo 19 ambayo wamecheza (Michezo mitatu zaidi) ambapo Yanga wanaongoza msimamo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
KOCHA WA SIMBA ANASEMAJE?

Kuelekea mchezo huu wa leo Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Matola amesema mara zote wanapokutana na Prisons mchezo unakuwa mgumu, ukizingatia kwa sasa wapo kwenye kiwango bora lakini wamejipanga kuwakabili.
Akizungumzia hali ya kikosi chao, Matola amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na wapo tayari kwa mtanange huo ambao lengo ni kuhakikisha wanapata ushindi.
“Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Prisons, mara zote tunapokutana inakuwa mechi ngumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Matola.
Matola ameongeza kuwa kiungo wao mkabaji, Sadio Kanoute hatakuwa sehemu ya kikosi kutokana na kuendelea kuuguza majeraha
MSAFARA WA KIKOSI

Kikosi cha Simba jana Jumanne kiliondoka kuelekea mkoani Morogoro tayari kwa mchezo wao huu wa leo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons, ambao unatarajiwa kupigwa Uwanja wa Jamhuri saa 10 jioni.
Kabla ya kuondoka kikosi kilifanya mazoezi ya mwisho asubuhi katika Uwanja wao wa Mo Simba Arena kwa ajili ya kujiweka tayari kwa mchezo huo.
Taarifa ya Simba ilieleza kuwa wameondoka na kikosi kamili kuelekea Morogoro, ambapo hakuna mchezaji yoyote ambaye amesalia isipokuwa nahodha, John Bocco anayeendelea kuuguza majeraha.
Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa kwa sasa kila mchezo wameupa umuhimu mkubwa na alama tatu ndio malengo yao, wakifahamu Prisons ipo kwenye kiwango bora kwa sasa lakini wamejipanga kuwakabili.
Kikosi cha Simba kilianza mazoezi pamoja na kuingia kambini kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu ya NBC ikiwemo mchezo huu dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa leo Jumatano katika Uwanja Jamhuri mkoani Morogoro.
MENEJA WA SIMBA, AHMED AWAITA MASHABIKI

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema sasa ni rasmi watatumia Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro kwa mechi zao za nyumbani na mechi dhidi ya Prisons itakuwa ya kwanza.
Ahmed amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo huo na lengo lao litakuwa kupata pointi tatu muhimu.
Ahmed amewaomba mashabiki wao kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi leo Jumatano kwa ajili ya kuispoti timu.
“Tumemaliza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika sasa tunarejea kwenye Ligi Kuu na leo Jumatano tutashuka dimbani kuikabili Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao utapigwa katika Uwanja wa Jamhuri.”
“Kikubwa tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani, tunahitaji furaha tuliyopata Jumamosi tuendelee nayo,” amesema Ahmed.
