yangasc------------------------------------------yangasc------------------------------------------

KUELEKEA mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga dhidi ya CR Belouizdad ambao unatarajiwa kupigwa kesho Jumamosi, habari ya mjini kwa sasa ni mtindo wa kupaka rangi nywele yaani ‘bleach’ kuienzi ‘PACOME DAY’

Yanga ambao wanadhaminiwa na Kampuni ya SportPesa kesho Jumamosi wanatarajiwa kuvaana na CR Belouizdad katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kipigo cha mabao 3-0, ambacho walikipata katika mchezo wa mkondo wa kwanza ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Julai 5, huko nchini Algeria.

KUHUSU MSIMAMO WA KUNDI
Mpaka sasa Yanga ambao wamepangwa kundi D la mashindano hayo wanakamatia nafasi ya tatu wakiwa wamekusanya pointi tano sawa na CR Belouizdad wakizidiwa kwa tofauti ya idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mabingwa watetezi wa mashindano hayo, Al Ahly wao wanaongoza msimamo baada ya kujikusanyia pointi sita huku, Medeama ya Ghana wao wakiwa wanabuluza mkia na pointi zao nne.

----------------------------------------------n
Msimamo wa kundi la Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika 

KWANINI ‘BLEACH’?
Yanga kupitia kwa Ofisa habari wa timu hiyo, Ally Kamwe msimu huu walitambulisha mfumo rasmi wa kuongeza hamasa ya kikosi chao kwa kuipa majina ya wachezaji kwenye michezo yao yote ambayo watacheza kwenye Uwanja wa nyumbani.
Katika mfululizo wa utaratibu huo tayari wachezaji watatu walipewa heshima katika michezo mitatu tofauti ambayo Yanga walicheza wakianza na Maxi Day kwa heshima ya kiungo wa kimataifa wa DR Congo, Maxi Nzengeli (Hii ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya ASAS FC ya Djibout).
Baada ya Maxi ikafuata Aziz Ki Day kwa heshima ya kiungo wa kimataifa wa Burkina Faso, Stephanie Aziz Ki kwenye mchezo dhidi ya Al Merrikh ya Sudani. Baada ya hapo ikafuata Bacca Day kwa heshima ya mlinzi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Abdullah kwenye mchezo dhidi ya Mabingwa watetezi wa mashindano hayo Al Ahly.
Hivyo, Pacome anakuwa mchezaji wa nne kupewa heshima hiyo kwenye mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya Waarabu hao Belouizdad, ambapo ikumbukwe pamoja na kutumia majina ya wachezaji pia mashabiki na viongozi hutumia wakati huo kuigiza baadhi ya tabia za mastaa hao ambapo kwa Pacome ni upakaji wa rangi kichwani yaani ‘Bleach’.

yangasc bleach player
yangasc——————————————

BELOUIZDAD WAIHOFIA YANGA
Wageni hao wa Yanga wameonekana kuuhofia ubora wa mchezo huu dhidi ya Yanga kutokana na ubora wa wenyeji wao ambapo akizungumzia maandalizi yao kuelekea mchezo wa kesho straika wa Belouizdad, Lamin Jallow alisema: “Tunafahamu Yanga ni kubwa kama zilivyo Al Ahly au Mamelodi na ndio maana wachezaji wote tuliokuja kwa ajili ya mchezo huu tuna ari ya kutafuta ushindi wa wa kihistoria hapa Tanzania.

“Hali ya hewa kwetu sio changamoto, unajua Afrika ni kama eneo moja, Mimi nimezaliwa Gambia na hii ndio mara yangu ya kwanza kufika ndani ya Tanzania lakini najihisi kama vile nipo kwetu.”

KUHUSU ‘BLEACH’ NA MAANDALIZI YANGA WANASEMAJE?

Licha ya kukamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi D la mashindano hayo, uongozi wa Yanga umeweka wazi kutinga hatua ya makundi liikuwa lengo lao mama, lakini sasa hesabu zao ni kucheza Robo fainali ya mashindano hayo.

Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema: “Tunafahamu mchezo huu utakuwa mgumu zaidi kwetu kulinganisha na michezo iliyopita ya mashindano haya msimu huu, kwa kuwa hapa tunahitaji ushindi tu ili kufufua matumaini ya kufuzu Robo Fainali.

“Tunajua kuwa kundi bado lipo wazi lakini ni pale tu kama tutaweza kutumia faida ya mchezo huu. Tunaheshimu ubora wa wapinzani wetu ila hata sisi pia tumekuwa na kikosi bora na tunajiamini, mafanikio ya kucheza fainali ya Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu yameongeza ari na sasa tunataka kuhakikisha tunakwenda kucheza Robo Fainali ya mashindano haya.

“Tumesahau matokeo ya michezo iliyopita tunaanza mapambano upya, benchi la ufundi limefanyia kazi mapungufu yetu ili kuandika rekodi mpya.”

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.