Kesho Jumanne ya Mei 9, 2023 katika dimba la Santiago Bernabeu nchini Uhispania utapigwa mchezo kabambe wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya kombe la klabu bingwa Ulaya kati ya Real Madrid dhidi ya Manchester City kutoka England.
Real Madrid ambao ndio mabingwa wa kihistoria wa UCL (14) na Man City zilianza kukutana kwenye mechi za kimashindano kuanzia mwaka 2012 na sasa zimecheza mara kadhaa na rekodi inaonyesha katika michezo 8 waliyokutana,timu hizi zinalingana katika matokeo kwani kila timu imeshinda mechi 3, imepoteza mechi 3 na sare ikijitokeza kwenye michezo miwili.
Licha ya kwamba Man City imetunisha msuli dhidi ya Real Madrid lakini kwa bahati mbaya kwao wameshindwa kuwaondosha Los Blancos kwenye hatua kama hii(nusu fainali).
Msimu wa 2015/16 kwenye mchezo wa nusu fainali,Real Madrid waliibwaga Man City kwa kuwapa kipigo cha bao 1-0 ,enzi hizo The Citizen ilikuwa ikinolewa na Manuel Pellegrini.
Kama haitoshi mwaka 2022, Man City wakiwa chini ya Kocha Pep Guardiola wakakutana na kadhia ya kutupwa nje kwenye hatua ya nusu fainali na Real Madrid kwa jumla ya bao 6-5 baada ya dakika za nyongeza hivyo kwa rekodi hii ni wazi kwamba Los Blancos wana rekodi bora dhidi ya The Citizen kwenye hatua kama hii swali ni je rekodi itajirudia ?
Man City wanaingia katika mchezo huu wakiwa wana kiu ya kusaka taji kubwa la kwanza barani Ulaya tangu 1970 enzi hizo likiitwa European Cup Winners,ingawa 2021 walikaribia kutwaa UCL lakini wakakutana na kizingiti cha Chelsea waliowanyuka bao 1-0 huko nchini Ureno.
Ugumu wa mashindano haya kwa City umedhihirika kwani Pep Guardiola licha ya kutawala EPL ndani ya misimu yake mitano na ametwaa mataji manne lakini katika UCL bado analisaka katika mwaka wake wa 6 huu,ingawa amecheza nusu fainali 3 mfululizo hivi sasa.
Baada ya kufuzu hatua ya robo fainali na kufahamu kwamba wanakutana na Man City, Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alisema “Tumefika kwenye hatua nzuri,tulishinda robo fainali dhidi ya Chelsea na tulikuwa imara eneo la ulinzi kwa kutoruhusu bao,hay ni matokeo mazuri na tunafurahia kukutana na changamoto iliyo mbele yetu”.
Naye mchezaji wa Man City Rodrigo alisema “Hadi sasa sijui cha kuelezea nini kipo kwenye Klabu bingwa Ulaya ambacho kinatufanya sisi wachezaji kuonyesha kiwango cha kushangaza,tuseme tu ni michuano maalum”.
Upande wa Pep Guardiola ambaye aliiongoza Man City kuwachapa Bayern Munich bao 4-1 kwenye robo fainali amesema”Miaka mitatu mfululizo tupo nusu fainali ya Klabu bingwa,sio suala la kushinda bali ni kwenda kujaribu na kadri unavyojaribu mara nyingi labda unaweza kushinda mwishoni”.
Hadi wanafikia hatua hii Klabu hizi zimekuwa na takwimu za kuvutia ambapo kwa Man City katika michezo 10 waliyocheza msimu huu, wameshinda 6, sare 4 na hawajapoteza, wamefunga bao 26, wameruhusu bao 4, wana wastani wa asilimia 60 kumiliki mchezo,wana asilimia 90.3 ya kupiga pasi sahihi,hawajaruhusu bao katika mechi 6 kati ya 10, huku wakikimbia Km 1176.04 katika michezo yote.
Upande wa Real Madrid wao katika mechi 10 wameshinda 8, sare 1 na wamepoteza 1, wamefunga mabao 25 huku wakiruhusu 8, wana wastani wa asilimia 55.1 ya umiliki wa mchezo,wanayo asilimia 90.4 ya kupiga pasi sahihi,katika michezo 10,mitano kati ya hiyo hawakuruhusu bao huku wakikimbia takribani Km 1002.4 kwenye michezo yote.
Timu hizi zinaonekana zipo katika kiwango kizuri kwani Real Madrid licha ya kuonekana wameshindwa katika La Liga,lakini wamefanya vizuri katika Kombe la mfalme na wapo nusu fainali UCL,lakini kwa Man City wanaongoza EPL, wapo fainali ya FA na nusu fainali ya UCL ,tafsiri yake wanawania mataji matatu makubwa Ulaya(Treble).
The Citizen haijapoteza katika mechi 19 mfululizo katika mashindano yote,wameshinda 16 na sare 3,wakati Real Madrid nayo tangu April ilicheza mechi 8 mfululizo katika La Liga bila kupoteza kabla ya kunyukwa hivi karibuni na Real Sociedad.
Real Madrid wanapaswa kumchunga mshambuliaji kinara wa kupachika mabao katika michuano hii, Erling Braut Haaland mwenye bao 12 ambaye pia amefunga mara 2 katika mechi 3 dhidi ya mpinzani kutoka La Liga.
Vilevile Los Blancos wanapaswa kuwa makini na Kevin De Bruyne ambaye ndiye mchezaji wa pili kwa pasi za mabao(5) katika michuano hii.
Nao The Citizen wanapaswa kuwa makini na Vinicius Jr ambaye ndiye kinara wa kupachika mabao kwa Real Madrid katika michuano hii na pia ndiye kinara wa pasi za mabao (6) bila kumsahau mbrazil mwenzake Rodrigo mwenye bao 5 lakini mtu wa kuchungwa zaidi ni Karim Benzema ambaye amekuwa aki ziadhibu vilivyo Klabu za England.
Jambo la kukumbuka ni kwamba fainali ya Klabu bingwa Ulaya itapigwa Juni 10,2023 huko Instabul Ataturk Olympic Stadium.
Mshindi kati ya Real Madrid na Man City atacheza na mshindi wa mchezo kati ya Ac Milan na Inter Milan.
Tayari mechi hii ipo katika tovuti yetu. Kucheza ama kubashiri tembelea sportpesa.co.tz au piga *150*87#

