- Kizungumkuti mechi ya Kariakoo Dabi Yanga SC vs Simba SC, Juni 25 2025 chatanda ikiwa ni saa chache kabla ya muda wa mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa saa 11:00 jioni kufika.
- Mechi ipo au haipo? Simba SC watoa tamko kuhusu mchezo huo namba 184 Uwanja wa Mkapa.
- Juni 22 Simba SC ilicheza mchezo wake wa mwisho kwenye ligi dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa KMC Complex.
Kizungumkuti mechi ya Yanga SC vs Simba SC kimetawala ikiwa ni saa chache kabla ya mchezo. Yanga SC wameweka wazi kuwa wapo tayari kwa mchezo namba 184. Simba SC wamebainisha kuwa watatoa taarifa kuhusu mechi hiyo kama ipo ama haipo.

Soma hii: Yanga SC vs Simba SC Juni 25 2025 matukio makubwa mawili kufanyika
Ikumbukwe kwamba mchezo huo awali ulitarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 ukaahirishwa. Mara ya pili ulipangwa Juni 15 ukaahirishwa. Mara ya tatu ni Juni 25 2025 huku kukiwa na ukimya kwa wageni Simba SC. Juni 24 2025, nahodha na kocha wa Simba SC walipaswa kutokea kwenye mkutano wa mwisho kabla ya mchezo hawakutokea isipokuwa nahodha na kocha wa Yanga SC ambao walibainisha kuhusu maandalizi yao.
Ahmed Ally kuhusu mchezo wa Juni 25 2025
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Juni 22 2025 baada ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar aliweka wazi kuwa taarifa itatolewa. Ally alibainisha kuwa mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar ni mchezo wa mwisho. Pia aliwapongeza wachezaji na mashabiki kuwa bega kwa bega na timu.

Soma hii: Sakata la kuyeyuka Kariakoo Dabi Machi 8 2025, sababu zipo hivi – SportPesa Tanzania
“Kwanza tuanze kwa kuipongeza Simba SC kuwa na kiwango bora zaidi kwa sasa. Kila kitu bora kipo ndani ya Simba SC. Unapomzungumzia kocha bora unamzungumzia Fadlu Davids, ukizungumzia kiungo bora wa ligi labda unaweza kwenda nje kidogo ukampata Feisal Salum.
“Lakini ukizungumzia mchezaji bora, unamzungumzia Jean Ahoua ukizungumzia mfungaji bora unamzungumzia Jean Ahoua. Ukizungumzia msemaji bora wa NBC unamzungumzia Ahmed Ally. Hata ukienda kutazama timu ambayo inaongoza kwa mapato ni Simba SC.
“Sisi kwetu Wanasimba tumekuwa na msimu bora zaidi. Tumekuwa tukitumia Uwanja wa KMC kwa mechi zetu za nyumbani hivyo kwa maana hiyo hata kama kukiwa na mechi 8 mbele yetu hizo hatutacheza nyumbani. Ninawashukuru mashabiki wa Simba SC kwa kujitokeza.
“Tumemaliza msimu wa NBC msimu wa 2024/25 tukiwa nyumbani kwa mechi zetu zote hivyo tunawashukuru. Kwanza ieleweke kitu kimoja hakuna mahali popote ambapo ratiba ikitoka lazima uthibitishe kama utacheza ama hautacheza.

“Na mimi nichukue nafasi hii kuwaambia Wanasimba kwamba kama kutakuwa na lolote kuhusu mechi ya Juni 25 tutawaeleza. Ila kwa sasa ninaweza kusema kwamba tumecheza mchezo wetu wa mwisho wa ligi kwa msimu wa 2024/25.
“Kiu kubwa ya mashabiki wa Simba SC ni kuhusu tarehe 25. Nichukue fursa hii kuwaambia mashabiki wote wa Simba SC kuwa kama kuna lolote la kuwaambia kuhusiana na tarehe 25, tutawaambia.”
Mwenyekiti wa Simba SC, Mangungu
Kuhusu mchezo dhidi ya Yanga SC, Murtanza Mangungu Mwenyekiti wa Simba SC mara baada ya mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar Juni 22 2025 aliweka wazi kuwa watazungumza kuhusu mchezo wao dhidi ya Yanga SC wakati ukifika.

Soma hii: Simba SC 1-0 Kagera Sugar ni mchezo wa mwisho 2024/25
“Tunafanya maandalizi tangu mwanzo wa ligi, habari za kusema kuwa kuna mchezo fulani hilo sisi hatuangalii tutazungumza wakati ukifika. Mashabiki wa Simba SC hawana wasiwasi. Ukiona shabiki wa Simba SC ana wasiwasi huyo sio shabiki wa Simba SC.
“Kwanza sijawaona mashabiki wa Simba SC wakizungumzia kuhusu mchezo wetu na mwisho wa msimu. Mechi zote za ligi nis awa na kila mchezo tunauchukulia kwa umakini wake.
Mchezo wa mwisho kwa Simba SC
Mchezo wa mwisho kwa Simba SC ikiwa Uwanja wa KMC Complex msimu wa 2024/25 ilikuwa Juni 22 2025. Katika mchezo huo wa mzunguko wa pili baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba SC 1-0 Kagera Sugar. Bao la ushindi lilifungwa na Steven Mukwala.
Mchezo huo ulikuwa ni raundi ya 30 kwa Simba SC. Mukwala alipachika bao hilo dakika ya 17 akitumia pasi ya David Kameta. Ni mabao 13 anafikisha ndani ya ligi msimu wa 2024/25.
Matokeo ya Yanga SC raundi ya 30

Wakati Simba SC ikivuna pointi tatu raundi ya 30 na watani zao wa jadi Yanga SC nao walivuna pointi tatu. Ilikuwa Yanga SC 5-0 Dodoma Jiji FC kwenye mchezo wa mzunguko wa pili ambao ulichezwa Uwanja wa New Amaan. Katika mchezo huo Yanga SC walifungua ukurasa wa mabao dakika ya nne ya mchezo na kufunga ukurasa wa mabao dakika ya 90.
Clatous Chama alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 4 akitumia pasi ya Clement Mzize, Duke Abuya alipachika bao la pili dakika ya 50 akitumia pasi ya Chama, Ibrahim Bacca alipachika bao la tatu dakika ya 62 akitumia pasi ya Maxi Nzengeli.
Beki wa kati wa Dodoma Jiji katika harakati za kuokoa hatari iliyopigwa na Farid Mussa dakika ya 90+4 alijifunga bao la nne kwenye mchezo huo na Maxi Nzengeli alikamilisha kamba ya tano dakika ya 90+7 akitumia pasi ya Jonathan Ikangalombo.
Msimamo wa ligi Yanga SC vs Simba SC
Yanga SC ni vinara kwenye msimamo wakiwa na pointi 79. Ni mechi 29 Yanga SC imecheza kishinda 26, sare moja na kupoteza mechi 2. Safu ya ushambuliaji imetupia mabao 81.
Yanga SC ni timu namba moja kufunga mabao mengi. Ni mabao 10 timu hiyo imefungwa ikiwa ni timu ambayo imefungwa mabao machache. Prince Dube na Clement Mzize wamefunga mabao 13 ndani ya Yanga SC.
Simba SC ni nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 78. Safu ya ushambuliaji ya Simba SC imefunga mabao 69. Ni mabao 11 ukuta wa Simba SC umeruhusu msimu wa 2024/25.

