- Ibenge & Maxi watikisa taarifa mpya usajili bongo, ndivyo unavyoweza kusema wakati huu tetesi za usajili zikipamba moto.
- Azam wanataka kuwashangaza Simba na Yanga kwa kushindana nao vikali kuelekea msimu mpya wa ligi 2025/26.
- Ligi Kuu Bara (NBC Premier League), inakaribia tamati ambapo timu zimesaliwa na mechi 2 au 3 tu.
Tetesi za usajili wa dirisha kubwa kuelekea msimu ujao wa 2025/26 zinaendelea kupamba moto, huku saa chache zilizopita majina ya kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge na kiungo wa Yanga yakitikisa mmoja akitajwa kuibukia Azam na Maxi akiwa na uwezekano wa kuondoka.
Ibenge atua Bongo kimyakimya, akutana na mabosi wa Azam Chamazi

Taarifa zilizoripotiwa na mwandishi wa kimataifa wa michezo, Micky Jnr raia wa Ghana ni kuwa, Florent Ibenge yuko karibu kuwa kocha mkuu mpya wa Azam FC. Imethibitika kuwa, Ibenge alikuwepo Tanzania siku ya Jumamosi na kutembelea makao ya klabu hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Ibenge pia alifanya kikao na maafisa wa klabu ya Azam na kuonyeshwa miundombinu ya timu. Kocha Ibenge amevutiwa na mradi huo wa Azam na sasa kinachosubiriwa ni makubaliano ya kifedha pekee.
Uongozi wa Azam unataka kushindana vikali dhidi ya timu kongwe za Simba na Yanga kuelekea msimu mpya wa ligi 2025/26, huku pia wakiweka malengo makubwa ya kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
SOMA HII PIA: Baada ya Aziz Ki: Mzize na Aucho wanaondoka Yanga? Tetesi usajili bongo
Nini kinaendelea kuhusu Maxi Nzengeli na Yanga?

Katika hatua nyingine mwandishi, Micky ameripoti kuwa Yanga wanapambana kutaka kumbakisha kiungo wao Mkongomani, Maxi Nzengeli ambaye anaweza kuondoka, kwani anawindwa kwa karibu na baadhi ya timu kubwa kutoka nje ya Tanzania.
“Maxi Mpia Nzengeli anamilikiwa kikamilifu na AS Maniema, amekuwa kwa mkopo Yanga, na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwaka huu. Yanga walitoa ofa ya dola 200,000 kumsajili moja kwa moja lakini rais wa Maniema bado hajajibu.
“Yanga sasa wanataka mkopo mwingine wa miaka miwili, hata hivyo klabu ya Maniema imekuwa ikisikilizia ofa nyingine bora kutoka kwingineko. Maxi mwenyewe yuko huru kuendelea kubaki au kuhama huku klabu kutoka Afrika Kusini na Morocco zikiwa kwenye rada.
SOMA HII PIA: Fei Toto kusaini Simba au Yanga? Tetesi usajili bongo, ulaya
Dili la Sowah bado kidogo tu

Huku taarifa hizo zikipamba moto Yanga nao hawajabaki nyuma, kwani tayari wameanza harakati za kuboresha kikosi chao na tayari majina ya Straika, Jonathan Sowah, Arthur Bada na Offen Chikola wanatajwa kutua kuijenga Yanga mpya.
Imeelezwa kuwa Yanga baada ya kumuuza, Aziz Ki sasa wanataka kuboresha kikosi chao kwa kuwapa kandarasi mpya kiungo, Zouzoua Pacome, Maxi Nzengeli na nahodha wao Job.
Ikumbukwe Ligi Kuu Bara (NBC Premier League), inaelekea ukingoni ambapo timu zimesaliwa na mechi 2 au 3 tu, huku dirisha kubwa la usajili likitarajiwa kufunguliwa rasmi baada ya ligi kuisha, kwa ajili ya timu mbalimbali kufanya maboresho ya vikosi vyao.
Sowah ameanza kuivutia Yanga baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu, ambapo straika huyo amefanikiwa kuifungia Singida Black Stars zaidi ya magoli 11.
Sowah aliyejiunga na Singida kupitia dirisha dogo la usajili la mwezi Januari anatajwa kuwa straika hatari zaidi nchini kwa sasa kutokana na kasi yake ya kutupia kambani, akifikisha zaidi ya mabao 10 katika kipindi cha nusu msimu tu, tofauti na anaoshindana nao.
Sowah na Yanga ni pipa na mfuniko?
Katika nyakati kadhaa straika huyo amenukuliwa kuwa kwenye uhusiano wa karibu mithili ya pipa na mfuniko na mabosi wa Yanga hususani Rais wa timu hiyo, Hersi Said, hali ambayo inatoa matumaini makubwa kwa Yanga kumvalisha jezi ya Wananchi msimu ujao.
Taarifa nyingine ambayo imekuwa na moto kutoka ndani ya Yanga ni kuhusiana na Yanga kupokea ofa 3 zinazohitaji huduma ya straika wao, Clement Mzize ambazo ni JS Kabylie, Zamalek na Al Ittihad ya Libya huku ofa ya Zamalekh ikiwa ni kubwa kuliko.
Mzize naye ni suala la muda tu, mbivu, mbichi kujulikana
Yanga mara baada ya kufanya biashara ya kumuuza kiungo wa kimataifa wa Burkina Faso, Stephanie Aziz Ki kwenda Wydad wanaonekana kuwa karibu kumalizana na biashara nyingine ya straika wao, Clement Mzize.
Lolote linaweza kutokea katika dili hili na huenda uongozi wa Yanga ukatoa taarifa rasmi ya kumuaga Mzize hivi karibuni, akiwa ni staa wa pili baada ya hivi karibuni kuagana na Mbukinabe, Aziz Ki aliyetimkia Wydad AC.
Hitimisho la tetesi za usajili Aucho bado hakijaeleweka

Kuhusu kiungo wa kimataifa wa Uganda, Khalid Aucho taarifa kutoka ndani ya Yanga zimethibitisha kuwa, mpaka sasa hakuna mazungumzo ya mkataba mpya kati ya Yanga na Aucho. Ikumbukwe mkataba wa Yanga na Aucho unaisha mwishoni mwa msimu huu.

