Yanga SC imeichapa Namungo FC nje ndani kwa msimu wa 2024/25 kwenye mechi za ushindani katika msako wa pointi tatu uwanjani. Maxi Nzengeli mkononi ana tuzo ya mchezaji bora dhidi ya Namungo FC baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika dakika 90 ambazo alitumia uwanjani kwa kutoa pasi ya bao lililofungwa na Aziz Ki na kufunga bao moja kwenye mchezo huo.

Wakati ubao wa Uwanja wa KMC Complex ukisoma Yanga SC 3-0 Namungo FC, pointi tatu mazima zilibaki kwa Yanga SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi ikiwa ni ushindi wa pili mbele ya Namungo FC ndani ya dakika 180 msimu huu.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba 30 2024 ubao wa Uwanja wa Majaliwa ulisoma Namungo 0-2 Yanga, mabao ya Kennedy Musonda na Pacome yalitosha kuipa Yanga SC pointi tatu.
Inahusiana na hii: Yanga Novemba kufunga ugenini, dakika 270 ganzi
Yanga SC 3-0 Namungo FC
Mei 13 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma Yanga SC 3-0 Namungo FC. Kwenye msako wa pointi sita ndani ya msimu wa 2024/25 Yanga SC kakomba zote na safu ya ushambuliaji imetupia mabao matano.

Kipa namba moja wa Yanga SC Djigui Diara kwenye dakika 90 mbele ya Namungo FC alitoka na hati safi akifikisha jumla ya hati 15 za kukaa langoni bila kufungwa.
Vita yao inazidi kuwa nzito dhidi ya kipa namba moja wa Simba SC, Moussa Camara ambaye yeye ana hati safi 16 akivunja rekodi ya kipa bora msimu wa 2023/24, Ley Matampi.
Mabao ya Yanga SC yalifungwa na Aziz Ki dakika ya 26, Prince Dube dakika ya 30 na Maxi Nzengeli dakika ya 71. Ushindi huo unaipa Yanga SC pointi tatu wakifikisha jumla pointi 73 kibindoni nafasi ya kwanza kwenye msimamo.
Inahusiana na hii:Yanga SC vs Namungo FC Mei 13 2025 KMC Complex
Vita ya ufungaji inazidi kuendelea
Bao la Prince Dube kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC linaendeleza vita ya kiatu bora cha ufungaji ambapo anafikisha mabao 13 sawa na mshambuliaji mwingine wa Yanga SC, Clement Mzize.Kinara kwa sasa ni Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC ambaye yeye katupia jumla ya mabao 15 kwenye ligi.
Msimamo ulivyo kwa sasa
Yanga SC ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 73 baada ya mechi 27. Safu ya ushambuliaji imetupia mabao 71 huku ukuta ukiruhusu mabao 10 yakufungwa ndani ya ligi. Imepoteza mechi mbili ushindi kwenye mechi 24 ndani ya ligi.

Namungo FC ni nafasi ya 10 kwenye msimamo baada yakucheza mechi 28 kibindoni ina poiti 31. Safu ya ushambuliaji imetupia mabao 23 na ukuta umeruhusu mabao 36.
Kuhusu mechi zilizobaki kwa Yanga SC 2024/25
Kuhusu mechi ambazo zimebaki kwa Yanga SC Kamwe ameweka wazi kuwa kwa mujibu wa ratiba waliyonayo wao ni mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 zimebaki baada ya kucheza dhidi ya Namungo FC, Mei 3 2025.
Katika mchezo huo ambao unakuwa ni wa 27 kwa Yanga SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 3-0 Namungo FC pointi tatu zikibaki Jangwani.
Ikumbukwe kwamba kila mzunguko kuna michezo 15 kwa timu ambapo Yanga hilo ilikamilisha mzunguko wa kwanza na mzunguko wa pili ni mechi 12 imecheza nakufanya icheza jumla ya mechi 27 zikibaki mechi tatu.
Mechi ya tatu ni dhidi ya watani zao wa Jadi Simba SC ambayo awali ilitarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 ikaahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB), wametoa ratiba ambayo inaonyesha kuwa mchezo huo wa Yanga SC vs Simba SC ambao ni namba 184 utachezwa Juni 15 2025.
Kamwe amesema kuwa kwa mujibu wa ratiba ambayo wanayo wao wamebakiwa na mechi mbili za ligi na nyingine ni kwenye CRDB Federation Cup ikiwa wataendelea kwenye hatua inayofuata.
“Tuna mechi mbili ambazo zimebaki kwenye ligi ambapo kuna mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji baada ya hapo tutakuwa tumemaliza mechi za ligi kwa upande wetu na kile ambacho tunakitambua sisi.
“Kwa upande wa CRDB Federation Cup tuna mchezo dhidi ya JKT Tanzania ambao ni nusu fainali ikiwa tutapita hapo tutakuwa na mchezo mmoja wa fainali hivyo itafanya kwa msimu wa 2024/25 tuwe na mechi nne ambazo zimebaki.”

