Steve Mukwala v KMC FCSteve Mukwala v KMC FC
  • Joshua Mutale kiungo mshambuliaji wa Simba SC ametakata kwenye mechi nne za ligi ambazo ni dakika 360, atwaa tuzo ya mchezaji bora mbele ya KMC FC
  • Jean Ahoua hakamatiki kwenye eneo la ufungaji akiwa kinara, hat trick yake ya kwanza dhidi ya Pamba Jiji yamfanya afikishe jumla ya mabao 15.
  • Rashid Chambo wa KMC FC amempa mateso makubwa kipa namba moja wa Simba SC, Moussa Camara akiiba mbinu za Jaffary Kibaya wa Mashujaa.

Simba SC imepata ushindi kwenye mechi nne za viporo huku Joshua Mutale, Jean Ahoua, Leonel Ateba, Fabrince Ngoma, Yusuph Kagoma wakiwa ni miongoni mwa wachezaji waliotakata kwenye mechi hizo. Ni dakika 360 Simba SC ilishuka uwanjani kete yake iliyopita ilikuwa dhidi ya KMC FC wakipata ushindi wa mabao 2-1 wakiwa ugenini katika kukamilisha dakika 360.

Mukwala vs KMC
Mukwala vs KMC

Simba SC 2-1 Mashujaa, Mei 2 2025

Mchezo huu ulichezwa Uwanja wa KMC Complex matokeo ilikuwa Simba SC 2-1 Mashujaa FC, mabao ya ushindi kwa Simba SC yote yalifungwa na Leonel Ateba kwa penati na bao la Mashujaa FC lilifungwa na Jaffary Kibaya alimtungua Moussa Camara kipa namba moja wa Simba SC akiwa nje ya 18 kwa mguu wake wa kushoto dakika ya 6.

Camara Moussa
Camara Moussa, kpa wa Simba SC. Source: Simba SC.

JKT Tanzania 0-1 Simba SC, Mei 5 2025

 Mei 5 2025, ubao wa Uwanja wa Isamuhyo  ulisoma JKT Tanzania 0-1 Simba SC. Bao la ushindi kwenye mchezo lilifungwa na Fabrince Ngoma dakika ya 45 akiwa ndani ya 18 kwa pasi ya Steven Mukwala. Ngoma kwenye mchezo huo alichaguliwa kuwa mchezaji bora.

Inahusiana na hii:JKT Tanzania yapigwa nje ndani na Simba SC 2024/25

Simba SC 5-1 Pamba Jiji, Mei 8 2025 

Mei 8 2025, Simba SC 5-1 Pamba Jiji, unaingia kwenye orodha ya ushindi mkubwa katika mechi za viporo. Kiungo mshambuliaji Jean Ahoua alifunga mabao matatu ikiwa ni hat trick yake ya kwanza ndani ya ligi alianza kufunga dakika ya 15 kwa mkwaju wa penati, dakika ya 36 kwa pigo la faulo, dakika ya 47 kwa pigo la kichwa. Anafikisha mabao 15 akiwa kinara wa utupiaji ndani ya ligi.

Mabao mawili yalifungwa na Leonel Ateba dakika ya 79 na dakika ya 84 huku bao la kufutia machozi kwa Pamba Jiji likifungwa na mshambuliaji Mathew Tegisi dakika ya 86 ambaye alikuwa mviziaji tangu mwanzo wa mchezo na alikutwa kwenye mtego wa kuotea dakika ya 25,33. Mwisho alifanikiwa kufunga bao la kufuta machozi.

Inahusiana na hii: Simba SC yaipiga Pamba Jiji 5-1 Ligi Kuu Bara KMC Complex

KMC FC 1-2 Simba SC, Mei 11 2025

Mei 11 2025 kwenye mchezo wa nne ambao unakamilisha dakika 360 za viporo vya Simba SC baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma KMC 1-2 Simba SC. Pointi tatu zikawa mali ya Simba SC. Rashid Chambo wa KMC FC alianza kumpa tabu kipa wa Simba SC, Moussa Camara dakika ya 8 akiwa nje ya 18 kwa mguu wa kulia uliopeleka maumivu kwa kipa huyo. Mabao ya Simba SC yalifungwa na Steven Mukwala huku kiungo Yusuph Kagoma wa Simba SC akiokoa hatari iliyokuwa inakwenda langoni dakika ya 78.

Pointi 12 kibindoni kwa Simba SC

Kwenye msako wa pointi 12 ndani ya uwanja katika mechi nne ambazo zilikuwa ni viporo Simba SC ilivuna zote kwa kupata ushindi katika mechi ambazo walikuwa uwanjani dhidi ya wapinzani wao.

Hesabu hizo zinaifanya Simba SC kucheza jumla ya mechi 26 msimu wa 2024/25 ushindi ni kwenye mechi 22, sare mechi tatu na kichapo waliambua kwenye mchezo mmoja ilikuwa dhidi ya watani zao wa jadi Yanga SC mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa. Safu ya ushambuliaji ya Simba SC imetupia jumla ya mabao 62 huku ukuta ukiruhusu mabao 11. Mabao yote hayo langoni alianza kipa namba moja wa Simba Moussa Camara.

Mabao 10 yakufunga kwa Simba SC yafungwa mabao matatu

Jean C- Ahoua
Jean Ahoua kiungo wa Simba SC mwenye mabao 15. Source: Simba SC.

Kwenye nne ambazo Simba SC imecheza safu ya ushambuliaji imetupia mabao 10 huku ukuta ukiruhusu mabao matatu yakufungwa. Ni mchezo mmoja pekee Simba SC walitoka na hati safi ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania ugenini.

Ni mshambuliaji Leonel Ateba kafunga mabao manne, kiungo mshambuliaji Jean Ahoua kafunga mabao matatu, kiungo mshambuliaji Fabrince Ngoma katupia bao moja na mshambuliaji Steven Mukwala kafunga mabao mawili. Mchezo dhidi ya Pamba Jiji ni mastaa wawili walifunga Jean na Ateba wakipata ushindi wa mabao 5-1.

Mutale wa Simba SC gari limeweka

Joshua Mutale Budo
Joshua Mutale Budo kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania. Source: Simba SC

Kiungo mshambuliaji wa Simba SC Joshua Mutale ambaye ni ingizo jipya gari limeweka kutokana na kasi yake katika mechi za mzunguko wa pili. Mutale alifungua ukurasa wake wa kutoa pasi za mabao kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.

Dakika ya 14 walipokuwa wakigongeana pasi na Kibu Dennis, ni Steven Mukwala alimalizia kazi kutoka kwa miguu ya Joshua ikiwa ni pasi yake ya kwanza ndani ya ligi na pasi ya pili alitoa dakika ya 47 alitoa pasi ya pili ya bao kwa Mukwala.

Baada ya dakika 90 kwenye mchezo huo Joshua alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo. Ni tuzo ya kwanza kwake kiungo huyo ambaye ameweka wazi kuwa ni furaha kuona timu inapata matokeo kwenye mechi ambazo wanacheza.

“Sikuanza msimu vizuri kutokana na kusumbuliwa na majeraha ila kwa sasa nipo vizuri. Nina furaha kutokana kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo hii ni kubwa na nina amini tutaendelea kufanya vizuri.”

Share this: