- Simba SC yaibamiza Pamba Jiji mabao 5-1 na kusepa na pointi tatu mazima ndani ya dakika 90 za ushindani.
- Jean Ahoua, Leoen Ateba wafunga mabao yakushangaza wakiwa nje ya 18 Uwanja wa KMC Complex wapeleka kilio Pamba Jiji.
- Camara atibuliwa rekodi yake dakika za jioni na mviziaji wa Pamba Jiji
Kasi ya Simba SC kwenye kulisaka taji la Ligi Kuu Bara ndani ya msimu wa 2024/25 inazidi kupanda kutokana na kupata ushindi kwenye mechi tatu mfululizo ambazo ni dakika 270. Huku ikiipiga Pamba Jiji ya Mwanza mabao 5-1 ukiwa ni ushindi mkubwa katika mechi za viporo ndani ya Mei.

Mei 8 2025 baada ya dakika 90 kugota mwisho ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma Simba SC 5-1 Pamba Jiji. Ilikuwa ni dakika 90 za burudani kwa timu zote mbili kusaka ushindi kwenye mchezo huo muhimu.
Pamba Jiji haina bahati na Simba SC msimu wa 2024/25 kwa kuwa imefungwa nje ndani. Mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba ilikuwa Pamba Jiji 0-1 Simba SC bao likipachikwa na Leonel Ateba dakika ya 22 kwa mkwaju wa penati.
Dakika 270 Simba SC yavuna pointi 9
Kwenye mechi tatu za ligi ambazo ni dakika 270 Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids imevuna pointi tisa mazima kwa kupata ushindi katika mechi hizo ambazo ni viporo vilivyotokana na Simba SC kuwa kwenye mashindano ya kimataifa.

Mei 2 2025, ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma Simba SC 2-1 Mashujaa FC, mabao ya ushindi kwa Simba SC yote yalifungwa na Leonel Ateba kwa penati na bao la Mashujaa FC lilifungwa na Jaffary Kibaya ambaye alimtungua Moussa Camara kipa namba moja wa Simba SC akiwa nje ya 18 kwa mguu wake wa kushoto.
Mei 5 2025, ubao wa Uwanja wa Isamuhyo ulisoma JKT Tanzania 0-1 Simba SC. Bao la ushindi kwenye mchezo lilifungwa na Fabrince Ngoma dakika ya 45 akiwa ndani ya 18 kwa pasi ya Steven Mukwala. Ngoma kwenye mchezo huo alichaguliwa kuwa mchezaji bora.
Mei 8 2025, Simba SC 5-1 Pamba Jiji. Kwenye mchezo huo Jean Ahoua alifunga mabao matatu ikiwa ni hat trick yake ya kwanza ndani ya ligi alianza kufunga dakika ya 15 kwa mkwaju wa penati, dakika ya 36 kwa pigo la faulo, dakika ya 47 kwa pigo la kichwa.
Mabao mawili yalifungwa na Leonel Ateba dakika ya 79 na dakika ya 84 huku bao la kufutia machozi kwa Pamba Jiji likifungwa na mshambuliaji Mathew Tegisi dakika ya 86 ambaye alikuwa mviziaji tangu mwanzo wa mchezo na alikutwa kwenye mtego wa kuotea dakika ya 25,33.
Kadi mchezo wa Simba SC vs Pamba Jiji
Mwamuzi wa kati Shomari Lawi alitoa adhabu ya kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa mchezaji wa Pamba Jiji Hamad Majimengi ambaye aliingia kipindi cha pili dakika ya 67 akichukua nafasi ya Zabona Mayombya.
Majimengi alionyeshwa kadi hiyo dakika ya 90 zikiwa zimepita dakika nne atoe pasi ya bao lililofungwa kwa Pamba Jiji dakika ya 86 likiwa ni lakufutia machozi.
Mbali na Majimengi kuonyeshwa kadi nyekundu, ni Mohamed Camara kipa wa Pamba Jiji alifungua ukurasa wa kuonyesha kadi na mwamuzi ilikuwa dakika ya 45 alipoonyeshwa kadi ya njano.
Kwa upande wa Simba SC ni beki Hamza Jr alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 45 na huyu hakumaliza dakika 90 aligotea dakika ya 45 nafasi yake ilichukuliwa na Che Malone.
Camara katunguliwa mabao mawili
Moussa Camara kipa namba moja wa Simba SC kwenye mechi tatu za mzunguko wa pili ni mabao mawili katunguliwa yote ikiwa ni Uwanja wa KMC Complex. Dhidi ya Mashujaa FC nje ya 18 na Pamba Jiji akiwa ndani ya 18.

Camara anaongoza kwa kuwa na hati safi ndani ya ligi baada ya kukaa langoni kwenye mechi 23 akikomba dakika 2,070 katuguliwa mabao 10 akiwa na hajafungwa kwenye mechi 16 ndani ya ligi.
Katika mechi tatu, Simba SC imefunga jumla ya mabao 8, mabao matatu ni mapigo ya penati huku Ateba akifunga penati mbili, Ahoua penati moja.
Nafasi kwenye msimamo
Simba SC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 66 baada ya mechi 25 ikipata ushindi kwenye mechi 21, sare tatu na ilipoteza mchezo mmoja ndani ya uwanja.
Pamba Jiji inabaki nafasi ya 13 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 27 ikipata ushindi kwenye mechi 6, sare 9 huku ikipoteza mechi 12 ni pointi 27 wanazo kibindoni msimu wa 2024/25.

