PSG vs Arsenal (-)PSG vs Arsenal (-)

PSG 2-1 Arsenal UEFA Champions League, ndivyo ubao wa matokeo ‘score board’ ya uwanja wa Parc des Princes ilivyoonyesha mara baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi –na kuashiria PSG wakifuzu fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya 2024/25.

Arsenal walipambana vikali kutafuta namna ya kupindua meza, lakini ubora wa Paris Saint-Germain uliwapa faida kubwa na kuibuka na ushindi muhimu uliowapeleka PSG Fainali.

PSG 2-1 Arsenal UEFA Champions league ‘live’ mchezo ulikuwaje?

PSG 2-1 Arsenal
Mastaa wa PSG wakishangilia ushindi baada ya mpira kuisha

Mabingwa hao wa Ufaransa wamefanikiwa kutinga fainali kwa matokeo ya jumla ya ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Fabián Ruiz na Achraf Hakimi huku bao la kufutia machozi la Arsenal likifungwa na Bukayo Saka.

Ushindi huo umewafanya PSG kuandikisha ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na sasa PSG watakutana na Inter Milan kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa ya msimu wa 2024-25 itakayopigwa Mei 31, mwaka huu.

David Raya aliokoa penalti ya Vitinha wakati PSG walikuwa mbele 1-0 kipindi cha pili, lakini juhudi hizo hazikutosha kwani ndoto ya Arsenal ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa msimu huu iliishia mjini Paris.

Ousmane Dembélé, ambaye alikuwa na mabao 25 katika mechi 25 alizoichezea PSG mwaka 2025 kabla ya mchezo wa jana aliingia akitokea benchi na kutoa asisti muhimu ya bao la Achraf Hakimi.

SOMA HII PIA: PSG Vs Arsenal UEFA CL: H2H, Vikosi, uchambuzi, utabiri

Arsenal nusura wapindue meza kipindi cha kwanza

PSG walianza vizuri mechi ya kwanza katika uwanja wa Emirates, lakini safari hii Arsenal ndio walioanza kwa kasi na kukaribia kupindua meza dakika za awali za kipindi cha kwanza.

Jurriën Timber alishinda mpira wa juu upande wa kulia na kutoa krosi kamili kwa Declan Rice ndani ya dakika tatu za kwanza, lakini kichwa cha Rice kilikwenda pembeni.

Arsenal walipaswa kufunga mapema kupitia mipira ya kurushwa ya Thomas Partey ambayo ilikaribia kuzaa matunda kupitia Gabriel Martinelli na Martin Ødegaard, lakini Donnarumma aliokoa vizuri mara zote mbili.

Kwa jumla, Arsenal walipiga mashuti matano ndani ya dakika 10 za kwanza, ikiwa ni mara ya kwanza msimu huu kufanya hivyo ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa.

PSG yajibu mapigo

PSG 2-1 Arsenal UEFA Champions League
Wachezaji wa PSG wakishangilia bao la uongozi

PSG walitulia baada ya dakika 15 na kuanza kujibu mapigo ambapo, Khvicha Kvaratskhelia alikaribia kuongeza bao kwa wenyeji baada ya kushirikiana na Désiré Doué, lakini shuti lake likagonga mwamba.

Paris walipata bao dakika ya 27 baada ya mpira wa adhabu kuokolewa nusu nusu na Partey, ukamkuta Ruiz ambaye alidhibiti mpira na kufyatua shuti kali lisilozuilika ambalo liliingia wavuni.

PSG walipaswa kuwa mbele kwa mabao 2-0 muda mfupi baadaye kupitia Kvaratskhelia lakini pasi yake kwa Barcola ilikuwa ndefu kidogo na shuti la Barcola likazuiliwa na Raya.

Arsenal walikaribia kusawazisha kabla ya dakika ya 60 kupitia kona ya Saka, lakini Timber hakuweza kuelekeza mpira golini. Saka naye alikaribia kufunga dakika chache baadaye lakini Donnarumma aliokoa.

SOMA HII PIA: Barcelona vs Inter Milan 30/4/2025: Vikosi, Rekodi, Uchambuzi, Yanayotarajiwa

VAR yazua gumzo

PSG walijenga shambulizi kupitia kwa Hakimi na kulazimisha uokozi kutoka kwa kipa Raya. Dakika chache baadaye, VAR ilimwambia refa Felix Zwayer aangalie tukio kwenye skrini ambapo mpira wa Hakimi ulimgonga Myles Lewis-Skelly mkononi na kuamuru penalti.

Vitinha alipiga penalty hiyo lakini Raya akaiokoa na kuipa Arsenal matumaini. Kocha, Luis Enrique aliamua kumuingiza Dembélé na kumtoa Barcola, na ndani ya dakika mbili tu, alitoa asisti ya bao la Hakimi.

Dembele aweka rekodi mpya ya mabao

Dembélé sasa amehusika kwenye mabao 12 katika Ligi ya Mabingwa msimu huu (mabao 8, assist 4), idadi kubwa zaidi kwa mchezaji yeyote wa PSG ndani ya msimu mmoja huku kwa Wafaransa, ni Karim Benzema pekee aliyefanya vyema zaidi (2021-22: mabao 15, assist 2).

Arsenal walipata bao lao kupitia kwa Saka ambaye alipokea mpira ambao ulishindwa kuondolewa vyema na walinzi wa PSG kufuatia shambulizi la kiungo Leandro Trossard.

Saka naye ni mwendo wa rekodi tu

------------------------------------------------n
Wachezaji wa Arsenal wakishangilia ubingwa

Bao hilo la Saka lilikuwa bao la 10 katika Ligi ya Mabingwa ndani ya mechi 18 alizocheza na kwa wachezaji wa Uingereza ni nahodha wao Harry Kane pekee aliyefikisha mabao 10 kwa haraka zaidi (mechi 12).

Saka alipaswa kuongeza lingine baada ya krosi ya Calafiori kumpita Donnarumma, lakini alipiga juu.

PSG waliweza kutuliza mchezo na kusimamia matokeo, na sasa wana nafasi ya kushinda taji lao la kwanza kabisa la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye fainali mjini Munich.

Dondoo muhimu za PSG 2-1 Arsenal

Katika mchezo huo PSG 2-1 Arsenal UEFA Champions League live, Arsenal walipiga mashuti 19, ikiwa ni idadi yao kubwa zaidi katika mechi ya mtoano tangu walipopiga 20 dhidi ya Barcelona Machi 2016.

Arsenal sasa wamefeli kufuzu katika nusu fainali nne mfululizo za mashindano makubwa (2020-21 Europa, 2021-22 League Cup, 2024-25 League Cup, 2024-25 Champions League) rekodi yao mbaya zaidi.

PSG wamefuzu kwa fainali yao ya nne ya Ulaya baada ya 1996, 1997 (Cup Winners’ Cup) na 2020 (Champions League).

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.