- Simba SC yaichapa JKT Tanzania nje ndani msimu wa 2024/25.
- Fabrince Ngoma aacha kilio kwenye kambi ya jeshi huku Simba SC wakisepa na kicheko
- Kocha JKT Tanzania abainisha mpango kazi ujao kwenye mechi za kazi
JKT Tanzania imepigwa nje ndani na Simba SC kwenye mechi mbili za ligi ambazo ni dakika 180 kwenye msako wa pointi sita wakifungwa mabao mawili ndani ya uwanja msimu wa 2024/25.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa ushindi waliopata dhidi ya JKT Tanzania una maana kubwa kwenye mbio za kusaka ubingwa kutokana na ugumu wa mchezo wenyewe.
Ipo wazi kwamba Mei 5 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Isamuhyo ulisoma JKT Tanzania 0-1 Simba SC pointi tatu zikielekea Msimbazi kwa mara nyingine mzunguko wa pili.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC Complex baada ya dakika 90 ulisoma Simba 1-0 JKT Tanzania kwa bao la Jean Ahoua ambaye ni kinara wa utupiaji ndani ya kikosi cha Simba SC akiwa katupia jumla ya mabao 12 na pasi 7 za mabao.
Ally amesema kuwa mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania walitambua kuwa utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao jambo ambalo liliwafanya wawe makini kwenye mchezo huo mwanzo mwisho.
“Unajua JKT Tanzania sio timu yakubeza hata kidogo ni miongoni mwa timu ngumu kupata ushindi na hili mwenye macho ameona namna hali ilivyokuwa uwanjani.
“Ila haya yametokana na ubora wa timu ambayo tupo nayo wachezaji wetu wamepambana mwanzo mwisho kupata ushindi na hatimaye tumevuna pointi tatu muhimu.
Huyu hapa kocha wa JKT Tanzania

Ahmed Ally, Kocha Mkuu wa JKT Tanzania amesema kuwa sababu kubwa iliyofanya wapoteza mchezo wao dhidi ya Simba SC ni makosa yao wenyewe huku suala la waamuzi akiwaachia wenye mamlaka husika.
Kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Ishamuhyo Mei 5 2025, JKT Tanzania ikiwa nyumbani ilishuhudia ubao ukisoma JKT Tanzania 0-1 Simba kwa bao la ushindi la Fabrince Ngoma dakika ya 45 akiwa ndani ya 18.
Kocha Ally ameweka wazi kuwa walikuwa wanatambua aina ya timu ambayo wanakutana nayo uwanjani ubora wake na udhaifu wake jambo ambalo liliwafanya waandae mpango kazi kuwakabili kwa umakini ndani ya dakika 90 na mwisho wakapoteza pointi tatu.
“Haukuwa mpango wetu kuona kwamba tunapoteza mchezo wetu hasa tukiwa nyumbani tulifanya maandalizi yote kwa umakini ili kupata matokeo na mwisho tumepoteza pointi tatu kilichotokea tunakwenda kufanyia kazi makosa kwa ajili ya mechi zijazo.
“Kuhusu waamuzi mimi siwezi kuzungumzia hilo na mara nyingi huwa tunafanya yale ambayo yanatuhusu sisi kwa kuwa ni majukumu yetu na kila mtu anatimiza majukumu yake.
“Nilikuwa nina kazi ya kuwaambia wachezaji watulie kwa kuwa niliona wanacheza kwa presha kubwa na maamuzi yanapotokea wao wanaanza kulalamika hivyo ili upate ushindi ni lazima kucheza kwa umakini na kutafuta matokeo ndani ya uwanja hivyo ilikuwa namna hiyo.”
Mtupiaji bao la ushindi

Fabrince Ngoma kiungo mshambuliaji wa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids alipeleka kilio kwenye kambi ya jeshi huku kicheko kikiwa kwao wakisepa na pointi tatu. Ni mchezo wa mzunguko wa pili pointi tatu kwa Simba SC na ule wa mzunguko wa kwanza Simba SC ilikomba pointi tatu na kupata ushindi nje ndani.
Baada ya dakika 90 Ngoma alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo na Simba ilikomba pointi tatu mazima kwenye mchezo wa pili ndani ya dakika 180 kwa ushindi wa bao mojamoja.
Ngoma amesema kuwa walikuwa wanatambua mchezo utakuwa mgumu na waliingia uwanjani kwa tahadhari ili kupata matokeo mazuri.
“Tunatambua kwamba ushindani ni mkubwa jambo ambalo linafanya tufanye kazi kubwa kusaka pointi tatu ndani ya uwanja, tupo tayari na tunafuata maelekezo ya benchi la ufundi kwenye mechi zetu zote ambazo tunacheza ili kupata matokeo mazuri.”
Hesabu za bao zilivyokwenda
Ngoma alipachika bao la ushindi dakika ya 45 baada ya Simba SC kupata kona muda mfupi kabla ya mapumziko na mpigaji alikuwa ni Jean Ahoua pasi yake ilikwenda kwa Joshua Mutale ambaye alipiga krosi kuelekea ndani ikakutana na Steven Mukwala.

Mukwala ambaye ni mshambuliaji alipiga pasi iliyokwenda kukutana na kiungo Ngoma akiwa ndani ya sita akapachika bao ambalo likadumu mpaka mwisho wa mchezo huo na Simba SC ikisepa na pointi tatu ugenini.
Simba SC kwenye msimamo wa ligi ni namba mbili ikiwa na pointi 63 baada ya mechi 24 JKT Tanzania ni namba 7 kwenye msimamo ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 27.

