- Uongozi wa Simba kupitia kwa mdhamini mwenye haki ya mauzo ya jezi zao kampuni ya Jayrutty wameingia mkataba na kampuni ya kimataifa ya vifaa vya michezo ya Diadora
- Kampuni Diadora imewahi kufanya kazi na baadhi ya timu kubwa ikiwemo AS Roma ya Italy
- Simba wapo Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Stellenbosch utakaopigwa Jumapili 27/4/2025
Simba SC watangaza jambo zito Afrika Kusini usiku huu, hii ni mara baada ya kutangaza kuingia makubaliano ya mashirikiano na Kampuni kubwa ya uzalishaji wa vifaa vya michezo duniani inayoitwa Diadora.
Ikumbukwe Simba wapo nchini Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wao mkataba Huku wakiendelea na maandalizi ya mchezo wao wa marudiano Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch utakaopigwa siku ya Jumapili.
HAWA HAPA MABOSI SIMBA WALICHOSEMA KUHUSU MKATABA HUO

“Ushirikiano huu kati ya Simba, Jayrutty na Diadora unaonyesha ni kiasi gani klabu ya Simba inatamani kufikia malengo yake ya kuwa timu bora barani Afrika.” – Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru.
“Diadora ni brand kubwa duniani na jezi zake zimewahi kuvaliwa na klabu kubwa duniani kama AS Roma na Simba inaendelea kukua ndio maana tumeamua kuvaa brand kubwa kama hii. Tutawapa ushirikiano wa kutosha na tunamuomba Mungu kuendelea kushirikiana nao kwenye maslahi ya pande zote mbili.” Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu.
“Wakati tunatangazwa kuingia mkataba huu na kutengeneza vifaa vya Simba kuanzia msimu ujao niliahidi. Kutokana na ukubwa wa Simba ni wakati wa kwenda kimataifa na leo tupo makao makuu ya Diadora ukanda wa SADC na kwa mara ya kwanza tunakwenda kutangaza ushiriki wa pamoja kati ya Simba, Jayrutty na Diadora.” – Afisa Mtendaji Mkuu wa Jayrutty (Kampuni yenye dhamana ya usambazaji wa jezi za timu hiyo) Joseph Rwegasira.
“Tunakushukuru sana Jayrutty kwa kutuheshimisha kwa kwenda kutuletea brand ambayo inatambulika kimataifa na umeamua kutongezea thamani zaidi jezi ya Simba kwa kutuletea brand kubwa ya Diadora ili timu yetu kuendelea kufahamika zaidi.”- Semaji Ahmed Ally
DIADORA WANASEMAJE USHIRIKIANO WAO NA SIMBA?
“Tumefurahi kupata nafasi hii ya kuwa sehemu ya udhamini wa miongoni mwa klabu kubwa Afrika na tunahidi kwenda kutengeneza bidhaa bora kama ilivyokuwa kwa timu tulizowahi kuzivalisha kwa muda mrefu ikiwemo AS Roma ya Italy.”- Afisa Mtendaji Mkuu Diadora South Africa, Mr. Yusuf Vadi.
SERIKALI YAIPONGEZA SIMBA

“Nimekuja nikiwa na furaha kushuhudia utekelezaji wa mkataba kati ya Simba na Jeyrutty walioingia wiki mbili zilizopita nikiwa mgeni rasmi na nimeshangazwa na jambo hili kutekelezwa kwa haraka kama ilivyoahidiwa. Hongera sana Jeyrutty kwa kuanza mapema utekelezaji..
“Nimekuja kuiwakilisha serikali hapa Afrika Kusini kwa ajili ya kuendelea kuwapa ushirikiano Klabu ya Simba kuhakikisha wanacheza wanafanya vizuri kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili na kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).
“Niwatakie kila la kheri na ushindi mnono kwenye mechi ya Jumapili ambayo itachezwa kule Durban na katika kipindi cha hivi karibuni hakuna timu inatamani kukutana na Simba na serikali imewapa ushirikiano mkubwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.”- Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma.
Unapoona klabu kama Simba inapata jezi na vifaa vingine bora kutoka kwenye kampuni kubwa ulimwenguni kama Diadora basi klabu hii inaendelea kukuwa na kujitangaza ulimwenguni kote kupitia michezo.”- Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana.
MAANDALIZI KUWAVAA STELLENBOSCH YAPAMBA MOTO
Kuelekea mchezo wao dhidi ya Stellenbosch ambao utapigwa siku ya Jumapili, Simba wakiwa Afrika Kusini wameendelea na tizi la maana tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao umebeba tiketi ya kucheza fainali ya mashindano hayo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya mashindano ya klabu.
Ikumbukwe mashindano makubwa zaidi kwa klabu ni Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba inahitaji angalau matokeo ya sare ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Fainali ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu yalipoboreshwa.

