Aziz v PambaAziz v Pamba
  • Aziz Ki ana deni la kuvunja rekodi yake ya mabao 21 aliyofunga 2023/24, deni la pasi moja ya bao kufikia rekodi yake.
  • Feisal ngoma imekuwa nzito upande wakucheka na nyavu msimu wa 2024/25 akiwa na mabao manne kibindoni.
  • Simba hali ni tete nyota wao mmoja aibuka kwenye msitu wa mastaa wa Yanga na Azam FC.

WAKATI wafungaji wakiwa wanapambania tuzo ya ufungaji bora kuna mitambo yakutengeneza pasi za mwisho ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni namba nne kwa ubora nao wanatimiza majukumu yao 2024/25.

Fei Azam ushindi
Kiungo wa Azam FC Feisal Salum akiwa na wachezaji wenzake wa Azam FC wakishangilia kwenye moja ya mchezo wa ushindani. Source: Azam FC.

Ipo wazi kwamba mbio za ubingwa wa ligi Bongo kwa sasa upo kwenye mikono ya timu mbili ambazo ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ikiwa inaongoza ligi na pointi zake 70 kibindoni baada ya mechi 26.

Namba mbili ni Simba ambayo ina pointi 57 ikiwa imecheza mechi 22 ikiwa itapata matokeo kwenye mechi zake nne zilizobaki itakuwa kwenye mwendelezo wa kusaka ubingwa na ikikwama nayo itakuwa imejiondoa mazima kama ilivyo kwa Azam FC.

Azam FC ni mechi 27 ilicheza ikiwa na pointi 54 ni mechi tatu zimesalia kukamilisha mzunguko wa pili ambazo ni pointi 9 hizi ikivuna zote itafikisha jumla ya pointi 63 hazitaifanya kutwaa ubingwa kwa kuwa tayari Yanga ameshazipita pointi hizo.

MITAMBO YA PASI ZA MWISHO

Kwenye eneo la watengeneza pasi za mwisho hapa balaa ni zito huku mzawa Feisal Salum nyota anayekipiga ndani ya kikosi cha Azam FC kinachotumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi za nyumbani akiwa ni namba moja.

Feisal Salum katengeneza jumla ya pasi 13 za mabao na pasi yake ya kwanza alitoa kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex ilikuwa dakika ya 19 alimpa mshikaji wake Idd Nado ambaye ni mfungaji wa bao la kwanza ndani ya kikosi cha Azam FC kwenye ligi msimu wa 2024/25.

Fei mbali nakutengeneza pasi za mwisho ana uwezo pia kwenye kufunga ambapo mguu wake ule wenye nguvu ni wakulia akiwa katupia jumla ya mabao manne. Azam FC imetupia jumla ya mabao 43 hivyo kahusika kwenye mabao 17.

Kwa msimu wa 2023/24 Feisal yeye alifunga jumla ya mabao 19 akiwa ni mzawa namba moja kufunga mabao mengi msimu uliopita ana deni kufunga mabao 15 kufikia rekodi yake jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kwa kuwa mechi zinakaribia kugota mwisho.

PACOME

KIUNGO
Pacome, kiungo mshambuliaji wa Yanga mwenye pasi 9 za mabao msimu wa 2024/25.

Kiungo mshambuliaji wa Pacome Zouzoua anaingia kwenye orodha ya wakali kwenye kutengeneza pasi za mwisho akiwa nazo pasi 9. Sio kwenye kutoa pasi za mabao tu bali hata kufunga yumo.

  Pacome kibindoni ana mabao 9 hivyo kahusika kwenye mabao 18 kati ya 68 yaliyofungwa na timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi.

MAXI

Maxi Nzengeli wa Yanga huyu anashikilia rekodi ya kuwa nyota wa kwanza kufunga bao ndani ya kikosi cha Yanga alifanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Kaitaba na mwisho ubao ukasoma Kagera Sugar 0-2 Yanga, bao la pili lilifungwa na Clement Mzize ambaye alianzia benchi.

Maxi Nzengeli
Maxi Nzengeli kiungo mshambuliaji wa Yanga ambaye anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji wa bao la kwanza 2024/25 katika kikosi hicho. Source: Yanga.

Maxi katengeneza jumla ya pasi 8 za mabao katika kikosi cha Yanga kinachoongoza ligi na pointi zake 70 kibindoni ni mabao 68 kimekusanya uwanjani kwenye mechi za ushindani.

ARTHUR

Kuna mwamba anatoka ndani ya wakulima wa alizeti wanaotumia Uwanja wa Liti kwa mechi za nyumbani kusaka ushindi anaitwa Josephath Arthur wa Singida Black Stars yeye katengeneza pasi 8 za mabao.

Singida Black Stars kwenye msimamo ni nafasi ya nne ikiwa na pointi 53, safu ya ushambuliaji imetupia mabao 40 kinara anaitwa Jonathan Sowa akiwa na mabao 11.

DUBE

Dubeee
Dube nyota ambaye amehusika kwenye mabao 20 kati ya 68 yaliyofungwa na Yanga msimu wa 2024/25. Source: Yanga.

Prince Dube wa Yanga katengeneza jumla ya pasi 8 za mabao katika kikosi hicho akiwa katupia mabao 12. Amehusika kwenye mabao 20 kati ya 68 yaliyofungwa na Yanga ndani ya ligi. Huyu anaingia kwenye rekodi ya kuwa nyota wa kwanza kufunga hat trick ilikuwa dhidi ya Mashujaa kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex.

AHOUA

Jean Ahoua wa Simba katengeneza jumla ya pasi 7 za mabao na kafunga mabao 12. Kahusika kwenye mabao 19 kati ya 52 yaliyofungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo.

AZIZ KI

Ki Aziz wa Yanga katengeneza pasi 7 za mabao msimu wa 2023/24 alitoa pasi 8 za mabao hivyo bado deni la pasi moja kuifikia rekodi yake mwenyewe kwenye mechi za ushindani.

Share this: