Fadlu SimbaFadlu Simba

MCHORA ramani ndani ya kikosi cha Simba 2024/25 Fadlu Davids amebainisha kuwa wanakazi kubwa kwenye mechi za kimataifa kutokana na ushindani uliopo hivyo anaamini kwamba mechi walizocheza katika hatua ya makundi zimewaamirisha wachezaji wa kikosi hicho ambacho kipo hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

Fadlu Davids
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba, mchoara ramani wa timu hiyo kitaifa na kimataifa. Source: Simba.

Ipo wazi kwamba Simba kwenye ardhi ya Tanzania wanapeperusha bendera katika anga la kimataifa wakiwa kwenye hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Coastal Union iliyokuwa kwenye safari moja katika Kombe la Shirikisho Afrika walimaliza mwendo mapema.

 Azam FC na Yanga inayodhaminiwa na SportPesa hizi zilikuwa kwenye hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika ziliondolewa kwenye mashindano. Hivyo kwenye timu nne ambazo zilikuwa na kazi katika anga la kimataifa, mbili zilitolewa katika hatua za mwanzo huku Yanga ikigotea hatua ya makundi.

Fadlu amebainisha kuwa walianza wakiwa na wachezaji ambao walikuwa hawajacheza kwa muda mrefu mechi za kimataifa jambo ambalo lilikuwa linawapa ugumu ila kwa kucheza mechi nyingi kumewaongezea uzoefu hivyo wanaingia kwenye mchezo mkubwa wakiwa na wachezaji ambao wamecheza mechi za kimataifa.

“Tulianza mechi za kimataifa tukiwa na wachezaji ambao hawajacheza mechi nyingi za kimataifa na wengine walikuwa hawajacheza kabisa jambo ambalo lilikuwa linaleta ugumu, kucheza kwao kwenye mechi za hatua ya makundi kumeongeza nguvu na uzoefu kwa wachezaji hivyo tunaamini kwamba tutakuwa kwenye mwendo mzuri kutafuta matokeo kwenye mchezo wetu ujao.

“Wapinzani wetu tunawaheshimu kutokana na ugumu uliopo kwenye haya mashindano hivyo tunafanya maandalizi mazuri kuona kwamba tunapata matokeo chanya katika mechi zetu kwani malengo ni kuona kwamba tunavuka hatua ambayo tupo kwa sasa.”

MTAMBO WA MABAO BADO HAUJAWAKA

 Uongozi wa Simba umebainisha kuwa  kinara wa kucheka na nyavu ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika Jean Ahoua kwa msimu wa 2024/25 akiwa ni chaguo la kwanza la kocha Fadlu bado hajawaka hivyo anaendelea kuimarika taratibu.

Ahoua Namungo
Ahoua kiungo wa Simba mwenye mabao 12 ndani ya ligi msimu wa 2024/25. Source: Simba.

Ndani ya kikosi cha Simba kiungo huyo rekodi zinaonyesha kuwa amecheza jumla ya mechi 21 akiyeyusha dakika 1,550 na mguu wake wenye nguvu ni ule wa kulia kwa kuwa mabao yote aliyonayo kibindoni kafunga kwa kutumia mguu huo.

Ikumbukwe kwamba Ahoua ni mkali kwenye mapigo ya penati kwenye mabao 12 aliyonayo ni matano alifunga kwa penati huku akiandika rekodi yakufunga penati mbili kwenye mchezo dhidi ya Namungo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa langoni alikuwa kipa Jonathan Nahimana.

Ahoua ndani ya ligi katupia mabao 12 akiwa na pasi 7 za mabao hivyo kahusika kwenye mabao 19 kati ya 52 yaliyofungwa na Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Kwa mwendo alionao kwenye ligi anawastani wakuwa na hatari ndani ya uwanja kila baada ya dakika 81 anashikilia rekodi ya kuwa kiungo wa kwanza kutoa pasi ya bao ndani ya Simba ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate uliochezwa Uwanja wa KMC Complex alitoa pasi hiyo kwa Che Malone.

HILI HAPA SEMAJI LIKITAMBA

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wachezaji waliopo ndani ya kikosi cha Simba wanatimiza majukumu yao kwa ushirikiano huku kiungo wao Jean Ahoua akizidi kuimarika taratibu kwa kuwa licha yakufunga mabao bado hajafikia kwenye viwango vya juu.

Ahmed
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba. Source: Simba.

“Ahoua ni mashine ya kazi nah apo unaona kwa namna anavyotimiza majukumu yake bado hajafikia asilimia 100 ya ubora wake, kuna muda unakuja mzuri zaidi Wanasimba watafurahi kwani anajua mpira akiwa uwanjani, wengi wanasema hivi na vile lakini kijana yupo kwenye mwendo.

“Unamuona akiwa na mpira anakuwa na maamuzi halafu anafikiria ushindi bado kuna yale ambayo yanazungumzwa juu yake kazi inaendelea ni hakika furaha itakuwa kwa mashabiki wakipata burudani kutoka kwa mnyama, huu ni ubaya ubwela .”

MNYAMA KAMBINI

Tayari wawakilishi wa Tanzania kwenye anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba wameingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa hatua ya robo fainali dhidi ya Al Masry ya Misri.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Aprili 2 2025 nchini Misri na ule wa pili unatarajiwa kuchezwa Aprili 9 2025 ambapo Simba watakuwa nyumbani kukamilisha kete ya mwisho ya dakika 180 za kusaka mshindi atakayetinga hatua ya nusu fainali.

Kwa sasa kikosi kimeingia kambini kwa maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Big Man Machi 27 2025 ambao huu ni wa CRDB Federation Cup utachezwa Uwanja wa KMC, Complex.

Share this: