SIO vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara pekee ndani ya msimu wa 2024/25 kuna kazi nyingine katika kuwania kiatu cha ufungaji bora ambapo wachezaji wa Yanga, Simba, Azam FC, Kagera Sugar mpaka Ken Gold wanavuja jasho kinomanoma ndani ya uwanja kusaka ushindi ndani ya dakika 90.

Ikumbukwe kwamba mabingwa watetezi wa ligi ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ilisepa na taji hilo msimu wa 2023/24 na nafasi ya pili ilikuwa mikononi mwa matajiri wa Dar Azam FC ambao nao wapo kwenye mbio za kulisaka taji la ligi.
Namba tatu walikuwa ni Simba ambayo kwa sasa ipo nafasi ya pili na imetinga hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya wapinzani wao Al Masry kutoka Misri na mchezo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa Aprili 2 ugenini na ule wa pili itakuwa Aprili 9 Simba watakuwa nyumbani.
VITA YA UFUNGAJI BORA
Vita sio nyepesi kwenye eneo la ushambuliaji ambapo mabingwa watetezi Yanga wao pointi zao kibindoni ambazo ni 58 ni saw ana idadi ya mabao ambayo wamefunga huku wakifuatiwa na Simba yenye mabao 52 kibindoni.
Timu zote zimeshuka uwanjani kwenye mechi 22 ndani ya msimu wa 2024/25 katika msako wa pointi tatu muhimu huku kwenye mzunguko wa kwanza walipokutana wababe hawa ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga.

Mzunguko wa pili ngoma ilitarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 ikayeyuka baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kutangaza kuwa wataupangia mchezo huo tarehe nyingine ambayo kwa sasa inasubiriwa na mashabiki na timu hizo mbili.
Kwenye eneo la kufunga,Yanga imekuwa na kasi kubwa ikiwapoteza watani zao wa jadi Simba kwa tofauti ya mabao sita ambapo wote wamecheza jumla ya mechi 22 ambazo ni dakika 1,980 huku Yanga ikiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 34 na Simba wakiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 38.
Jean Ahoua ni namba moja kwa utupiaji akiwa ametupia mabao 12 na ametoa pasi 7 za mabao, yupo zake ndani ya kikosi cha Simba kilicho nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku. Katika mabao ambayo amefunga Ahoua ni matano alifunga kwa penati akiwa ni mkali kwenye eneo hilo.
Simba ndani ya 2024/25 ni penati 10 walipata kwenye mechi za ushindani ambapo tano alipiga Leonel Ateba ambaye yeye alifunga nne na moja iliokolewa na kipa wa Namungo, Jonathan Nahimana kwenye mchezo wa ligi mzunguko wa pili.
Ateba ni mkali wakucheka na nyavu ndani ya kikosi cha Simba akiwa ametupia mabao 8 kibindoni kwa msimu wa 2024/25 ambapo kwenye mechi za hivi karibuni kwenye ligi kasi yake imeonekana kupungua tofauti na mwanzo alivyoanza.
YANGA MWENDO WA 10
Kutoka Yanga mastaa wao wakali kwenye kucheka na nyavu wametupia mabao 10 kila mmoja ikiwa ni Prince Dube na Clement Mzize hawa wamekuwa kwenye mwendo wao ndani ya uwanja kwa kucheka na nyavu wanapopata nafasi.
Mbali na kufunga, Dube katengeneza pasi 7 za mabao ni mchezaji bora ndani ya ligi kwa Februari alitwaa tuzo hiyo alipowashinda wachezaji wenzake aliongia nao fainali ikiwa ni Aziz Ki wa Yanga na Seleman Bwezi wa Ken Gold inayopambana kubaki ndani ya ligi.
MZEE WA WAA NDANI

Steven Mukwala mzee waw aa, mshambuliaji mrefu kuliko goli huyu ni namba mbili kwa wakali wenye mabao mengi ndani ya kikosi cha Simba akiwa ametupia mabao 9 kibindoni kwenye mechi za ushindani.
Yupo sawa na mshambuliaji wa Singida Black Stars, Elvis Rupia mwili jumba ambaye huyu alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Kariakoo ambao ni Yanga kwenye dirisha dogo la usajili.
Peter Lwasa kutoka Kagera Sugar inayonolewa na Kocha Mkuu Juma Kaseja yeye katupia mabao 8 kibindoni sawa na Ateba wa Simba iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
MWENYE KIATU CHAKE HUYU HAPA
Msimu wa 2023/24 kiatu cha ufungaji bora ni Aziz Ki wa Yanga alikitwaa baada ya kufunga mabao 21 na alitoa pasi 8 za mabao. Kiungo huyo ambaye mguu wake wenye nguvu ni ule wa kushoto jina lake lilitajwa kwenye kikosi bora, alitwaa tuzo ya kiungo bora na mchezaji bora.
Ni mabao 7 katupia kwenye ligi sawa na idadi ya mabao ambayo kafunga, akiwa anadaiwa pasi moja kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita na mabao 14 kuifikia rekodi yake mwenyewe.

