KWENYE idara ya kutengeneza pasi za mwisho ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni ligi namba nne kwa ubora Afrika kiungo mshambuliaji kutoka Azam FC, Feisal Salum, Fei Toto amekimbiza akiwapiga bao mastaa kutoka Yanga na Simba.

Kiungo huyo amekuwa kwenye ubora wake ndani ya 2024/25 ni nyota wa kwanza kutoa pasi ya bao katika kikosi cha Azam FC ilikuwa dakika ya 19 kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex na alimpa pasi mshikaji wake Idd Nado.
Azam FC kwenye msimamo ipo nafasi ya tatu baada ya mechi 23 ambazo ni dakika 2,070 imekusanya jumla ya pointi 48 na safu ya ushambuliaji imetupia mabao 36 ikiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 57. Vinara wa ligi ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa.
Nyota huyo kawakimbiza mastaa wa Simba na Yanga ambapo kwa upande wa timu hizo wakali wakutengeneza pasi za mwisho wamefikisha 7 tofauti ya pasi tano za mabao kwenye mechi za ushindani.
FEI TOTO AVUNJA REKODI YAKE
Kiungo Fei Toto tayari amevunja rekodi yake ambayo aliandika msimu wa 2023/24 akiwa na uzi wa Azam FC kwa kutoa pasi 7 za mabao mpaka msimu ulipogota mwisho.
Tayari idadi hiyo amefikia na kuivunja akiwa namba moja kwenye chati hivyo ubora wake umezidi kuwa imara na kasi yake haijapoa kwenye upande wa kutoa pasi za mwisho na kazi bado ipo kwenye eneo la kufunga.

Ni mabao 19 Fei alifunga msimu uliopita baada ya kucheza jumla ya mechi 29 akikomba dakika 2,442 ndani ya uwanja mshindani wake mkubwa alikuwa ni Aziz Ki wa Yanga ambaye huyu alitoa pasi 8 za mabao na alitupia mabao 21 akiibuka kuwa mchezaji bora na mfungaji bora baada ya kucheza jumla ya mechi 27.
HAWA HAPA WANAFUATA
Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba yeye katoa pasi 7 za mabao kati ya mabao 52 ambayo yamefungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 22.
Simba inanolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids mtambo wao mkubwa wa mabao ni Ahoua kwa kuwa amehusika kwenye mabao mengi zaidi kuliko wachezaji wengi ndani ya ligi kiujumla.

Ahoua ukiweka kando kutoa pasi 7 ni mabao 12 katupia kwenye eneo hili akiwa ni namba moja hali inayomfanya ahusike kwenye mabao 19 kati ya 52 ambayo yamefungwa na timu hiyo.
Katika mabao 12 Ahoua kafunga mabao matano kwa penati akiwa ni miongoni mwa wapigaji penati namba moja ndani ya kikosi cha Simba ambacho mpaka sasa ni jumla ya penati 10 walipata na katika hizo tano alipiga Leonel Ateba ambaye alipata nne na moja iliokolewa kwenye mchezo dhidi ya Namungo.
Kwa upande wa Yanga ni Prince Dube mshambuliaji wa Yanga, Aziz Ki, Maxi Nzengeli hawa wote wametengeneza pasi 7 kila mmoja ndani ya ligi. Dube katupia mabao 10 akiwa ni nyota wa pili kuhusika kwenye mabao mengi ndani ya Bongo ikiwa ni mabao 17 kati ya 58 yaliyofungwa na Yanga.
Kiungo wa kazi Pacome huyu katoa jumla ya pasi sita za mabao akiwa sawa na mwamba Josephat Arthur anayekipiga ndani ya Singida Black Stars inayotumia Uwanja wa Liti kwa mechi za nyumbani.
Singida Black Stars kwenye msimamo ipo nafasi ya nne baada ya mechi 23 ambazo ni dakika 2,070 ni mabao 32 safu ya ushambuliaji imetupia kinara akiwa ni Elvis Rupia mwenye mabao 9 kibindoni.
Ni wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 64 kwenye mechi za ushindani ambazo wanacheza kwenye ligi namba nne kwa ubora Afrika ambayo ushindani wake unazidi kuwa mkali kila leo.
Yanga ni vinara kwenye msimamo baada ya mechi 22 wamekusanya pointi 58 ikiwa ni idadi saw ana pointi zao kibindoni ni wastani wa dakika 34 upo kwa Yanga kwenye kufunga bao baada ya kukomba dakika 1,980.

